Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-18 16:01:50    
Mabango ya matangazo ya bidhaa za China yaliyowekwa barani Afrika

cri

Ingawa bidhaa zilizotengenezwa nchini China zinaonekana hapa na pale duniani, lakini kutokana na kuwa bidhaa nyingi za China zinazouzwa katika nchi na sehemu mbalimbali duniani ni bidhaa nyepesi, tena hazina chapa maarufu, hivyo ni nadra kuona mabango ya matangazo ya bidhaa zilizotengenezwa nchini China nje ya China. Kutokana na kujiendeleza kwa wafanyabiashara wa China katika soko la Afrika, mabango ya matangazo ya bidhaa za China yameanza kuonekana barani Afrika.

Nchini Kenya, Ikweta ni mahali penye umaalum wa kipekee, makampuni maarufu mengi ya kimataifa kama vile kampuni ya Coca cola na kampuni ya Fuji yameweka mabango yao ya matangazo kwenye eneo hilo. Kampuni ya dawa ya Huali ya China inayoshughulikia biashara ya dawa za kutibu malaria barani Afrika pia imeweka bango lake la matangazo kwenye sehemu ya Ikweta ambayo ina vivutio vya utalii. Kwenye bango la matangazo ya bidhaa ya Huali lenye rangi ya manjano, mtoto mmoja wa kike wa China na watu kadhaa wa Afrika wanatabasamu kwa furaha. Kwenye bango hilo, kuna maneno "Unapita Ikweta" yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, na nyuma ya maneno ya "Huali" yaliyoandikwa kwa Kichina ni maneno "kutoka China" yaliyoandikwa kwa Kiingereza, watalii wengi wanaotembelea sehemu hiyo ya Ikweta hupenda kupiga picha chini ya bango hilo la matangazo. Mbali na Ikweta, kampuni ya dawa ya Huali ya China pia imeweka mabango mengine mawili ya matangazo kando ya barabara inayoelekea kwenye uwanja wa ndege Jomo Kenyata jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

Malaria ni ugonjwa ulioenea sana barani Afrika na husababisha vifo vingi, wakazi wengi wa Kenya wamewahi kutumia "Cotecxin" dawa ya kutibu malaria inayotengenezwa na kampuni ya Huali. Katika miaka mingi iliyopita, "Cotecxin" imeokoa maisha ya watu zaidi ya milioni moja nchini Kenya. Kwa kuwa dawa ya "Cotecxin" inatengenezwa kutokana na raslimali ya mitishamba, madhara yake kwa afya ni madogo, hivyo inapendwa sana na wakazi wa huko, "cotecxin" ni moja ya chapa kadhaa za bidhaa za China zinazojulikana sana huko Kenya.

Chapa nyingine ya bidhaa ya China inayojulikana huko Kenya ni Haier, kampuni ya Haier ya China inajulikana duniani kwa kutengeneza bidhaa za elektroniki za nyumbani. Mabango ya matangazo ya "Haier" yanaonekana hapa na pale jijini Nairobi, kando ya njia muhimu. Kwenye mabango ya matangazo ya Haier yenye rangi ya waridi yameandikwa maandishi makubwa ya "HAIER", na "mtengenezaji mkubwa wa pili duniani wa vyombo vya umeme vya matumizi nyumbani" yaliyoandikwa kwa Kiingereza. Vyombo vya umeme vya matumizi nyumbani vilivyotengenezwa na kampuni ya Haier vinapatikana katika maduka mengi makubwa ya huko Kenya, na zinapendwa sana na wakazi wa huko kutokana na sifa ya vyombo na huduma bora za kampuni.

Matangazo ya magari ya QQ yaliyotengenezwa nchini China yanajulikana sana nchini Misri. Magari ya QQ yalipoanza kuingia nchini Misri, wakala wa magari hayo wa Misri alitumia dola za kimarekani zaidi ya laki tano kufanya matangazo, wakati huo picha za magari ya QQ zilionekana kwa wingi kwenye magazeti na televisheni, na kupata ufanisi mzuri sana. Vijana wengi wa Misri walikuwa wamevutiwa sana na magari ya QQ yenye sura nzuri na bei nafuu.

Kwa kweli ni bidhaa chache tu za China zilizotangazwa nchini Misri. Kwenye vituo vikubwa vya kuwekea mabango ya matangazo ya bidhaa kando ya madaraja ya juu, majengo marefu karibu na uwanja mkubwa wa Cairo, na barabara ya mwendo wa kasi inayopita jangwani ni nadra kuona mabango ya matangazo ya bidhaa za China. Sababu ni kwamba bidhaa nyingi za China zinazouzwa nchini Misri ni bidhaa nyepesi, na gharama ya kuweka mabango ya matangazo ya bidhaa ni kubwa. Kampuni ya Zhongxin ya China iliyoko nchini Misri iliwahi kupanga kuweka bango la matangazo kando ya madaraja ya juu, lakini ilipaswa kuacha mpango wake kutokana na gharama kubwa.

Ingawa bidhaa nyingi za China hazikutangazwa, lakini bado zinapendwa sana na wakazi wa Misri. Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Cairo Bwana Hamid Tahir aliwahi kuandika makala iitwayo "China nyumbani kwangu" akieleza kuwa, siku moja aligundua kwa mshangao kuwa, saa za mkononi, taa ya mezani na vitu vingine vingi vinavyotumiwa nyumbani kwake vilitengenezwa nchini China.

Jambo muhimu zaidi kuangaliwa ni kwamba, kwa watu wengi wa Misri, bidhaa za China zina sifa bora na bei nafuu. Bw. Ahmed anayefanya biashara ya maji ya kunywa alisema, zamani baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa nchini China hazikuwa na sifa nzuri, lakini katika miaka ya karibuni sifa ya bidhaa za China imekuwa nzuri siku hadi siku. Bwana Ahmed aliyepata shahada nchini Marekani alisema hivi sasa sifa ya bidhaa za China inaweza kulingana na ile ya bidhaa zilizotengenezwa na nchi za magharibi, lakini bei ya bidhaa za China ni nafuu zaidi kuliko ile ya nchi za magharibi.

Mwalimu mmoja wa chuo kikuu cha Misri alisema, bidhaa za China hazina haja ya kufanyiwa matangazo nchini humo, watu wote wanapenda kununua bidhaa zenye sifa bora na bei nafuu.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-18