Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-21 14:47:12    
Ni kwa nini Iran imeamua kufanya luteka kubwa kwa wakati huu?

cri

Tarehe 19 Agosti Iran ilianza kufanya luteka kubwa itakayodumu kwa wiki tano, ambayo inawashirikisha wanajeshi wa majeshi ya nchi kavu, majini na anga. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha taifa cha Iran, katika luteka iliyofanyika tarehe 20 jeshi la Iran lilirusha kwa majaribio kombora la masafa kati ya kilomita 80 na 250 dhidi ya shabaha ya ardhini, na majaribio mengine ya kurusha makombora dhidi ya manowari pia yatafanywa. Lakini ni kwa nini Iran inafanya luteka hiyo kubwa kwa wakati huu?

Msemaji wa jeshi la Iran Bw. Mohammad Reza Ashtiani alisema lengo la luteka hiyo ni kuonesha mtizamo mpya wa kujilinda wa Iran. Kutokana na hali ya wasiwasi inayotokea katika kanda hiyo, Iran inapaswa kuwa tayari kukabiliana na tishio lolote. Pia alikiri kuwa luteka hiyo inalenga kufuatia sera ya kidiplomasia ya Iran. Lakini wachambuzi wamesema kufanyika kwa luteka hiyo ya Iran kunatokana na mambo mawili.

Kwanza ni Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio namba 1701 wiki iliyopita, ambalo limefanikisha usimamishaji wa vita iliyodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja kati ya kundi la Hezbollah la Lebanon na Israel, na hapo baadaye mkutano mkubwa wa hadhara ulifanyika huko Tehran, mji mkuu wa Iran kwa kushangilia kushindwa kwa Israel na kuonesha uungaji mkono kwa Lebanon. Kwa maoni ya Iran usimamishaji vita huo ni ishara ya kushindwa kwa Israel. Nguvu za kijeshi kati ya Israel na Hezbollah zina tofauti kubwa, lakini baada ya mapambano ya zaidi ya mwezi mmoja, Israel hata ilishindwa kutimiza lengo lake la kupiga pigo kubwa kwa kundi la Hezbollah, zaidi ya hayo mashambulizi ya Israel yalilaaniwa na jumuiya ya kimataifa. Wachambuzi wanasema Iran imeamua kufanya luteka hiyo ya kijeshi ili kuonesha kwa mara nyingine tena uungaji mkono kwa Hezbollah na kuonesha nguvu yake kubwa kuionya Israel.

Tukio lingine muhimu zaidi ni kuwa Iran inakabiliwa na shinikizo kubwa katika suala la nyuklia. Azimio namba 1696 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linaitaka Iran isimamishe shughuli zake za kusafisha uranium nzito kabla ya tarehe 31 Agosti, na Iran yenyewe imeamua kutoa jibu rasmi kwa pendekezo lililotolewa na nchi 6 za Russia, Marekani, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani tarehe 22 Agosti. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Bw. Hamid-Reza Asefi tarehe 20 alisema nchi hiyo bado haina ratiba ya kusimamisha shughuli za kusafisha uranium nzito. Alisema azimio namba 1696 halina msingi wa kisheria, na Iran haitalipokea. Hata hivyo alisisitiza kuwa Iran inaona kuwa suala lake la nyuklia linapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.

Wachambuzi wanasema viongozi wa Iran wanaona kuwa kufanya luteka ya kijeshi kunasaidia kutekeleza sera kali ya nyuklia. Na Iran imeamua kufanya mazoezi hayo ya kijeshi kabla ya muda uliowekwa na azimio namba 1696 ili kuonesha kuwa, ina nguvu ya kijeshi ya kupambana na Israel, hata Marekani, na Iran iko tayari kukabiliana na hali mbalimbali, bila kujali Marekani kuiwekea vikwazo vya kiuchumi au kuishambulia, Iran ina mbinu za kukabiliana na hali hiyo. Hii vile vile ni mbinu ya "vita vya kisaikolojia" dhidi ya Marekani.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan tarehe 20 aliitaka serikali ya Iran itoe jibu lenye juhudi kwa pendekezo la nchi 6 ambalo litaweka msingi wa kufanikisha utatuzi wa suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo.

Kutokana na Iran kufanya luteka hiyo, rais Hosni Mubarak wa Misri aliionya Marekani isichukue kitendo cha kijeshi dhidi ya Iran. Alisema Iran ni nchi muhimu katika sehemu ya Mashariki ya Kati, kuishambulia Iran kutakomesha amani na utulivu kwenye sehemu hiyo na hata kwenye dunia nzima. Mikwaruzano kati ya Marekani na Iran juu ya suala la nyuklia la Iran inapaswa kutatuliwa kwa njia za kidiplomasia na mazungumzo ya moja kwa moja. Maneno hayo yanaonesha maoni na ufuatiliaji wa nchi nyingine duniani.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-21