Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-22 16:26:30    
Mji wa kale wa Xian waendeleza kilimo kipya cha mjini

cri

Vituo vya kilimo vyenye mazingira ya kupatana kwa viumbe na bustani za maua vilivyojengwa kwenye viunga vya mji wa Xian, mkoani Shanxi, kaskazini magharibi mwa China vinawavutia wakazi wa mjini kwenda kupumzika na kuvitembelea. Sekta hiyo ya kilimo inayounganisha mambo ya utalii na mazingira ya kupatana kwa viumbe inaonesha mwangaza wa kilimo cha mji huo. Katika kipindi hiki cha leo, nitawafahamisha jinsi mji wa Xian unavyoendeleza kilimo kipya cha mji.

Kwenye vituo vya majaribio ya kilimo, mwandishi wetu wa habari aliona mashamba makubwa na ya wastani ya wakulima yenye mazingira tupu ya sehemu ya vijiji pamoja na shughuli za "kuchuma matunda mitini" zinavutia idadi kubwa ya wakazi wa mjini. Kilimo cha mjini kinachounganisha rasilimali za kilimo na shughuli za utalii kinawavutia wakazi wa mji kupunga hewa safi ya milimani, kuonja matunda safi yasiyoathiriwa na vitu vya uchafuzi na kuburudika katika mazingira ya sehemu ya vijiji. Wakati wakulima wanapotoa huduma na aina mbalimbali za chakula kwa wakazi wa mijini, pato lao linaongezeka siku hadi siku.

Wazo kuhusu "kilimo cha mji" lilitolewa na baadhi ya wanauchumi nchini Marekani kati ya miaka ya 50 na 60 ya karne iliyopita, walisisitiza kama uzalishaji-mali, mzunguko wa fedha na ununuzi wa bidhaa ni shughuli muhimu za kwanza za kilimo cha mji zinazohudumia miji. Naibu mkurugenzi wa taasisi ya sayansi ya kilimo ya mji wa Xian ambaye ni mtaalamu wa kilimo Bw. Zhang Xuanhou alisema, kilimo cha mji ni mtindo mpya wa kilimo cha kisasa na ni maendeleo makubwa ya kilimo cha jadi.

"Kilimo cha mjini kimepiga hatua mpya za kuelekea kilimo cha kisasa kutoka kilimo cha jadi, umuhimu wake ni kuharakisha mchakato wa kuinua kiwango cha uzalishaji mali wa kilimo."

Habari zinasema umaalumu wa kilimo cha mjini kinachounganisha kilimo cha utalii na kilimo cha mazingira ya kupatana kwa viumbe siyo kutoa mazao kwa wakazi wa miji peke yake, na iliyo muhimu zaidi ni kuweka mazingira mapya ya mapumziko na starehe kwa wakazi wa mijini.

Kilimo cha mjini kimepata nafasi nzuri sana ya kuunganisha vijiji, wakulima na wakazi wa mijini, ambacho licha ya kuhamasisha nguvu ya uzalishaji mali wa kilimo, kinaongeza pato lake. Shamba la miti ya mipichi lenye hekta zaidi ya 1,000 katika wilaya ya Weiyang, ya mji wa Xian linasifiwa kuwa ni "bustani ya nyuma" ya wakazi wa mji wa Xian, inatembelewa na idadi kubwa ya watu katika majira ya mchipuko. Naibu kiongozi wa kituo cha utafiti wa matunda Bw. Huang Xiao alisema,

"Wilaya ya Weiyang ilianzisha shamba la mipichi toka mwaka 1986, hivi sasa eneo la shamba la mipichi limezidi hekta 1,000. Mauzo ya mapichi yalikuwa mazuri katika miaka ya karibuni, pato la kila hekta kutokana na mauzo ni kiasi cha Yuan 75,000. katika miaka ya hivi karibuni matembezi ya kuangalia maua ya mipichi na kuchuma mapichi mitini vinafanyika kila mwaka na kuvutia idadi kubwa ya wakazi wa mjini, licha ya kuangalia maua na kuchuma mapichi mitini, watu wanaburudika kwa kuishi katika nyumba za wakulima na kula chakula cha wakulima.

Kilimo cha jadi kikiungana na teknolojia ya kisasa, wazo jipya na kupata mtaji unaohitajiwa, kitaleta ufanisi mkubwa, ambao watu hawakuutazamia. Ardhi za wilaya nyingi zilizoko nje ya mji wa Xian ni za tambarare na zenye rutuba. Lakini uzalishaji mazao ya kilimo wa jadi uliodumu kwa miaka mingi na bila kubadilika haukuleta maisha mazuri kwa wakulima wanaoishi kwenye ardhi hiyo. Wakati wimbi la kilimo cha kisasa linapoikumba sehemu kubwa nchini China, mji wa Xian ulianzisha shamba la majaribio ya kilimo lenye shughuli za utalii. Hivi sasa kilimo cha kipya cha mji kinapiga hatua kubwa za maendeleo, kilimo cha mazingira ya kupatana kwa viumbe na kilimo cha kiwango cha juu vimepata mafanikio ya mwanzo. Wakulima wanaolemewa na kazi ngumu mashambani, wananufaika hatua kwa hatua kutokana na kilimo cha mazingira ya kupatana kwa viumbe na kilimo cha kiwango cha juu.

Kijiji cha Xibashi kilichoko kwenye kiunga cha mji wa Xian kinajulikana sana kwa matikiti maji matamu kinachozalisha kwa kutumia mbolea ya samadi. Mkuu wa kijiji cha Xibashi Bw. Gong Kanghai alisema,

"Usimamizi unafanyika katika hatua zote toka kuotesha miche hadi matikiti maji yanapokomaa, mbolea inayotumika yote ni ya samadi, na dawa za kuua vijidudu pia ni dawa zisizoleta madhara kwa afya ya binadamu."

Kutokana na kutumika kwa njia za kisayansi katika zao la matikiti maji, matikiti maji ya kijiji hicho ni matamu zaidi kuliko matikiti maji ya vijiji vingine. Hivyo pato la wakulima wa kijiji hicho ni kubwa kuliko wa vijiji vingine, na wastani wa pato la familia ya mkulima kutokana na matikiti maji unazidi Yuan elfu 10 kwa mwaka.

Kilimo cha mjini chenye teknolojia ya kisasa licha ya kuongeza pato la wakulima, kinachangia kujitokeza kwa kampuni za wakala wa kilimo. Ili kukidhi mahitaji ya soko la miji, inapaswa kuendeleza vyama vya uchumi wa ushirika wa vijiji, kukiuka uzalishaji wa kifamilia, na kushirikisha wakulima kuzalisha kwa wingi mazao bora ya kilimo. Katika hali ya namna hiyo, jumuiya maalumu za kilimo ziliibuka kwa wingi.

Jumuiya ya wazalishaji wa zao la cheri ya wilaya ya Baqiao ya mji wa Xiani inasaidia wakulima kuuza cheri zao kwa kuandaa shughuli za kuchuma matunda ya cheri na kwenda kutoa matangazo katika sehemu ya nje. Wakulima wanasifu jumuiya yao ya wakulima wa cheri wakisema, "Matunda ya mwanzoni ya cheri yanaweza kuuzwa kwa bei kubwa zaidi, ambayo si chini ya Yuan 60 kwa kilo 1, wakulima wanafurahi wakisema, kwanza ni kutokana na sera nzuri za chama, pili ni maelekezo bora ya jumuiya ya wakulima wa cheri, ambayo ilinunua vitabu na kueneza ufahamu kuhusu zao la cheri na kusisitiza usimamizi wa kisayansi, inatoa maelekezo ya kiufundi kuhusu kuzalisha cheri zisizo na vitu vya kuathiri afya ya binadamu, kwani matunda ya namna hiyo yananunuliwa sana na watu."

Habari zinasema ili kuunga mkono na kuzisaidia wilaya zake mbalimbali kuendeleza kilimo cha mji, hivi karibuni mji wa Xian ulianzisha mfumo wa uwekezaji wa aina mbalimbali. Idara ya fedha ya mji wa Xian mwaka huu imetenga Yuan milioni 50 kwa matumizi maalumu ya kuendeleza kilimo cha mjini, ambazo zitaongezeka hadi Yuan milioni 60 kwa mwaka tokea mwaka 2007 hadi mwaka 2010.

Kutokana na uungaji mkono wa kifedha, mji wa Xian hivi karibuni umeanzisha kituo cha majaribio ya kilimo chenye mashamba hekta laki kadhaa na kuanzisha viwanda 9 vya usindikaji wa mazao ya kilimo vyenye uwezo wa uzalishaji mali wa Yuan milioni zaidi ya 100. Viwanda hivyo ambavyo vinashirikisha familia laki 5 za wakulima, vimekuwa na bidhaa zake maarufu zenye nguvu ya ushindani katika masoko, hivi sasa kilimo cha mji kimekuwa njia muhimu ya maendeleo ya kisasa ya kilimo katika viunga vya miji.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-22