Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-22 16:29:18    
Sekta ya michoro ya katuni itaingia kipindi chenye maendeleo makubwa

cri

Hivi karibuni serikali ya China ilisema itahimiza maendeleo ya sekta ya michoro ya katuni, na kuweka lengo la kufanya sekta hiyo iwe na pato la Yuan za Renminbi bilioni 200 hadi 300 likiwa ni zaidi ya 1% ya pato la taifa katika miaka 5 hadi 10 ijayo. Maofisa wa sekta hiyo wanasema, kutokana na kuhimizwa na lengo hilo sekta ya michoro ya katuni itaingia kwenye kipindi chenye maendeleo makubwa.

Sekta ya michoro ya katuni inahusu vitabu vya michoro ya katuni, magazeti yenye michoro ya katuni, filamu za sinema za michoro ya katuni, michezo ya katuni ya televisheni, video pamoja na uzalishaji bidhaa za mavazi husika, vitu vya kuchezea watoto na michezo ya elektroniki. Katika miaka ya karibuni serikali ya China imebuni sera na mbinu nyingi za kuhimiza maendeleo ya sekta ya michoro ya katuni. Takwimu zinaonesha kuwa filamu za sinema za michoro ya katuni zilizotengenezwa katika mwaka jana karibu ni jumla ya filamu zilizotengenezwa katika miaka 10 iliyopita, wakati filamu za katuni zilizotengenezwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu ni ongezeko la kiasi cha 70% kuliko mwaka uliopita katika kipindi kama hiki. Uzalishaji bidhaa zinazokutokana na michoro ya katuni pia unainuka kwa mfululizo, na pato la sekta ya michoro ya katuni linaongezeka kwa udhahiri.

Filamu inayojulikana kwa jina la "Maswali 3,000 ya paka mtundu wa rangi ya bluu" ni filamu ambayo karibu watoto wote wenye umri wa kutoka miaka 2 hadi 8 nchini China wanaifahamu. Filamu hiyo ya katuni inapendwa sana na watoto nchini China tangu ilipooneshwa kwa mara ya kwanza katika televisheni miaka 7 iliyopita. Msimamizi mkuu wa idara ya mawasiliano wa kampuni ya katuni ya Sanchen, ambayo ilisanifu na kutengeneza filamu ya katuni ya "Maswali 3,000 ya paka mtundu wa rangi ya buluu", Bw. Nie Jinxing alipoelezea filamu hiyo alisema,

"Hadi hivi sasa tumemaliza kutengeneza mifululizo 6 ya 'Paka wa Rangi ya Buluu' yenye sehemu zaidi ya 2,000, ambazo zimeweza kuoneshwa kwenye mtandao wa kitaifa kutokea mwaka 2001. Hivi sasa filamu hiyo inaoneshwa kwa pamoja katika vituo vya televisheni zaidi ya 700 nchini China, watu zaidi ya milioni 80 wanaiangalia kila siku. Mbali na kuoneshwa katika televisheni, filamu ya Paka wa Buluu inaoneshwa katika tovuti ya katuni, ambayo inatembelewa na watu kiasi cha laki 4.5 kwa siku. Mji wa Beijing umeweka mpango na kujenga vituo kadhaa vya michoro ya katuni kwenye wilaya ya Shijingshan iliyoko magharibi mwa Beijing, hatua hiyo ni moja ya vitu vilivyotiliwa mkazo katika maendeleo ya sekta ya michoro ya katuni mjini Beijing. Naibu mkurugenzi wa kamati ya maendeleo ya mageuzi ya wilaya ya Shijingshan Bw. Peng Chunhui alisema,

"Kuna studio kiasi cha 30 za michoro ya katuni wilayani Shijingshan, ambazo zinahusu utengenezaji wa filamu za michoro ya katuni, na vitabu vya michoro ya katuni. Tumeanzisha sehemu ya michoro ya katuni kwenye kituo cha burudani cha teknolojia ya tarakimu, hivi sasa kampuni nyingi za michoro ya katuni zimetoa ombi la kuingia katika sehemu hiyo."

Bw. Peng Chunhui alisema serikali ya Shijingshan inatekeleza sera za kutoa ruzuku ya kodi ya nyumba kwa studio za michoro ya katuni, na kutoa misaada ya mitaji kwa studio hizo.

Japo kuwa sekta ya michoro ya katuni imepiga hatua kubwa, lakini bado iko katika kipindi cha mwanzo cha maendeleo, na iko mbali na nchi zilizoendelea katika sekta ya michoro ya katuni. Hivyo serikali ya China imesema katika miaka michache ijayo, wizara ya fedha ya China itatenga fedha maalumu kwa ajili ya kuisaidia kuendeleza sekta ya michoro ya katuni ili kuongeza nguvu ya ushindani za sekta hiyo.

Mkuu wa kitivo cha michoro ya katuni cha chuo cha filamu za sinema cha Beijing, Bw. Sun Lijun alisema, ili kutimiza lengo lililowekwa, inatakiwa kuwaandaa mabingwa wengi wa michoro ya katuni, kuongeza mitaji na kuboresha mazingira ya uzalishaji mali ya sekta hiyo. Alisisitiza kuwa studio za michoro ya katuni zinatakiwa kutoa michoro mingi zaidi yenye umaalumu wa kichina.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-22