Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-22 15:13:13    
Barua 0822

cri
Msikilizaji wetu Ingkti Paramena wa S.L.P 7, Bunyore, Kenya ametuletea barua akiwapongeza wahusika wote wa Radio China Kimataifa. Anasema kwa kweli imembidi anunue radio ndogo ili aweze kusikiliza vipindi vya Radio China Kimataifa akiwa shuleni. Anasema Radio China Kimataifa inaendelea kuwavutia mashabiki wengi, yeye akiwa miongoni mwao. Ndio maana ameamua kuandika barua kutushukuru kwa vipindi vya Radio China Kimataifa. Mwishoni anaomba Mungu atujalie, kuwapa nguvu viongozi wote wa Radio China Kimataifa, wasikilizaji na wasomaji wa tovuti ya Radio China kimataifa.

Tunamshukuru Bwana Ingkti Paramena kwa ushabiki wake kwa matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutembea kwenye tovuti yetu ili kutoa maoni na mapendekezo kutusaidia kuboresha vipindi vyetu. Na hapa tunawakumbusha wasikilizaji wetu anuani ya tovuti ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa ni www. cri.cn. Tunawakaribisha wasikilizaji wetu watembelee tovuti yetu kwenye mtandao wa internet.

Msikilizaji wetu Sakah Nyagwoko wa S.L.P 351, Kisii Kenya ametuletea barua akitoa shukrani kwa wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa, kutokana na matangazo ya Kiswahili yanayorushwa kila siku. Anasema yeye ni shabiki mpya wa Radio China Kimataifa, anatuambia kuwa ataendelea kuwasiliana nasi, kusikiliza matangazo yetu na kututumia maoni mbalimbali.

Msikilizaji weu Bi. Edinah Nyakundi wa S.L.P 2995 Kisii, Kenya naye ni shabiki mpya wa Radio China kimataifa, anasema katika barua yake kuwa, anafurahia matangazo yetu kwa hiyo ametuandikia barua akitoa shukrani kwa vipindi na matangazo yetu na kusema kuwa ataendelea kuwasiliana nasi mara kwa mara.

Tunawashukuru na kuwakaribisha kwa furaha Bwana Sakah Nyagwoko na Bi. Edinah Nyakundi kuwa wasikilizaji wetu, ni matumaini yetu kuwa watasikiliza matangazo yetu kila mara na kutuletea maoni na mapendekezo yao.

Msikilizaji wetu Mogire Machuki wa P. O . Box 646, Kisii, Kenya ametuletea barua akiwasalimu kwanza wafanyakazi na wasikilizaji wote wa Radio China Kimataifa, anasema yeye anaendelea kufurahia matangazo na vipindi vya Radio China Kimataifa.

Anasema baada ya kukamilika kwa kombe la dunia FIFA 2006 lililokuwa linafanyika huko Ujerumani, bila shaka macho ya watu duniani sasa yanaelekea kwenye michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Beijing China mwaka 2008. Anafurahia kuwa serikali kuu ya China inazidi kuweka mikakati ya kufanikisha michezo ya Olimpiki. Aidha ni hatua ya kuvutia kwa China kwa kuzindua kampeni dhidi ya uvutaji wa sigara kwenye maeneo ya viwanja vya michezo ya Olimpiki. Imethibitishwa na wanasayansi kuwa sigara au moshi wake una athari kubwa sana kwa mtu ambaye havuti sigara.

Anasema ni matumaini yake kuwa ifikapo mwaka 2008 idadi ya watu wanaovuta sigara nchini China itakuwa chini ya idadi ya wavutaji wa sasa ambayo takwimu zinaonesha kuwa ni karibu milioni 350. Na alisema hili ni tatizo ambalo idara ya afya ya Kenya inajaribu kukabiliana nalo. Ingawa sekta ya sigara inachangia sana kwenye ukuaji wa uchumi wa Kenya, lakini pia imegundulika kuwa uvutaji wa sigara ni tishio kwa afya ya wananchi wa Kenya ambao sio wapenzi wa sigara.

Anasema, Sheria yenyewe bado haijapitishwa rasmi na swala la uvutaji wa sigara bado linaendelea, lakini muhimu zaidi ni kuwa afya za wanadamu ni lazima zilindwe kwa kila namna. Anamaliza barua yake kwa kusema kupitia Radio China Kimataifa ana uhakika kuwa wasikilizaji wataendelea kunufaika na mada ambazo hutangazwa kwenye vipindi mbalimbali.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Mogire Machuki ambaye kila mara anatuletea barua akituelezea maoni yake baada ya kusikiliza matangazo ya Radio China kimataifa, maoni yake yanatutia moyo tuweze kuchapa kazi zaidi ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu, na hivi karibuni tunaandaa vipindi kuhusu michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itakayofanyika hapa Beijing, ambapo tutawaelezea wasikilizaji wetu habari mbalimbali kuhusu michezo hiyo itakayofanyika hapa Beijing.

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa P. O. Box 504, Lindi, Tanzania ametuletea barua akieleza kuhusu ziara ya waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao barani Afrika mwezi Julai mwaka huu. Anasema anaipongeza serikali ya China kwa kuandaa safari ya kiongozi wa China barani Afrika. Safari hiyo ilianzia Misri na kupitia nchi mbalimbali, mpaka Tanzania. Anasema Watanzania wote wa bara na visiwani walifarijika sana kwa safari hiyo ya waziri mkuu wa China, na kufurahia na neema kubwa waliyopata.

Anasema wakati wa ziara ya waziri Mkuu Wen Jiabao nchini Tanzania, mikataba mbalimbali ilitiwa saini kati ya Tanzania na China, kwa mfano kuimarisha reli ya TAZARA. Na makubaliano kati China na Tanzania yanahusu mambo ya kiufundi na kiuchumi, yakiwemo msaada wa dawa za kupambana na malaria, ujenzi wa shule za msingi vijijini, kituo cha kilimo na kituo cha kinga na tiba ya malaria, na mkataba wa mkopo wa fedha kutoka kwa serikali ya China. Kwa upande wa Zanzibar, makubaliano ya kiuchumi na kiufundi yaliyotiwa saini ni ukarabati wa Uwanja wa Amaan na Kituo cha Televisheni na Radio Zanzibar, na makubaliano mengine mengi. Hiyo inaonesha kuwa China ni nchi inayozijali nchi marafiki za Afrika.

Bw. Karim anamaliza kwa kusema anatoa shukrani nyingi na anawatakia viongozi wote waliokuwepo kwenye msafara huo kila la heri waliofanikisha ziara hiyo ya kihistoria, kwani uhusiano kati ya China na Afrika haukuanza leo, na utaendelea kuwepo.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Gulam Karim kwa barua yake inayotuelezea ziara ya waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao nchini Tanzania, kutokana na maelezo yake tumehisi zaidi urafiki na ushirikiano wa kunufaishana kati ya wananchi wa China na Tanzania. Tuna imani kuwa baada ya juhudi za wananchi wa China na Afrika urafiki na ushirikiano kati ya pande mbili utaimarishwa siku hadi siku. Sisi tunajitahidi kushirikiana na wasikilizaji wetu kuchangia maendeleo ya uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika.

Idhaa ya kiswahili 08-22