Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei tarehe 21 alisema, Iran imetunga mpango wa kinyuklia na itaendelea kuutekeleza kwa uthabiti. Alisema nchi kadhaa ikiwemo Marekani zina hofu na Iran kuendeleza teknolojia ya nyuklia, kwa hiyo zinaiwekea Iran shinikizo kubwa ingawa zina ufahamu kwamba Iran haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia.
Iran iliahidi kutoa jibu rasmi tarehe 22 Agosti kuhusu pendekezo jipya la kutatua suala la nyuklia la Iran lililotolewa na nchi 6 za Russia, Marekani, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani mwanzoni mwa mwezi Juni. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 1696 mwishoni mwa mwezi Julai, likiitaka Iran isimamishe shughuli zote zinazohusu kusafisha uranium nzito, na kufanya ushirikiano na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki. Hapo baadaye Iran ilieleza kutolikubali azimio hilo. Na kauli hiyo kali ya Ayatollah Khamenei inawafanya watu wawe na wasiwasi kuwa, suala la nyuklia la Iran linaweza kuendelea na hali ya mvutano.
Katika siku kadhaa zilizopita, maofisa waandamizi wa Iran walitoa kauli kali kwa nyakati tofauti. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Bw. Hamid-Reza Asefi tarehe 20 alisema, Iran haina mpango wala ratiba ya kusimamisha shughuli za kusafisha uranium nzito. Alisema azimio namba 1696 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa halina msingi wa kisheria. Siku moja baadaye naibu mwenyekiti wa shirika la nishati ya atomiki la Iran Bw. Mohammad Sa'eedi alisema, Iran imepata maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, hivi sasa haiwezi kusimamisha shughuli za kusafisha uranium nzito. Alidokeza kuwa, kinu cha kutengeneza maji mazito cha Iran kitaanza kufanya kazi hivi karibuni, kitatoa maji mazito kwa kinu cha nyuklia cha maji mazito ambacho bado kinatengenezwa. Imefahamika kuwa kinu cha nyuklia cha maji mazito kinazalisha plutonium, ambayo ni rahisi zaidi kutumika katika kutengeneza silaha za nyuklia. Zaidi ya hayo tarehe 19 jeshi la Iran lilianza kufanya luteka kubwa. Hili ni onyo kwa nchi za magharibi kuwa, Iran haitakubali shinikizo lao, na ina uwezo wa kukabiliana na uvamizi wowote.
Hata hivyo vyombo vya habari vimeona kuwa, Iran haijafunga kabisa mlango wa kufanya mazungumzo. Ofisa mwandamizi wa Iran ambaye hakutaka kutaja jina lake alidokeza kuwa, tarehe 22 Iran itatoa waraka wa jibu kamili kwa Umoja wa Ulaya. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bw. Hamid-Reza Asefi hivi karibuni alisema, pendekezo la nchi 6 linahusiana na masuala ya pande mbalimbali, kwa hiyo jibu la Iran litakuwa la pande mbalimbali. Vyombo vya habari vya Ulaya vimekadiria kuwa, katika jibu la Iran litakalotolewa tarehe 22, Iran haitalipokea kabisa pendekezo la nchi 6 wala haitalikataa kabisa, bali inaweza kukubali sehemu ya pendekezo hilo, kuzikataa sehemu fulani, na kuendelea na mazungumzo juu ya sehemu nyingine. Yaani Iran haitasimamisha shughuli za kusafisha uranium nzito kama inavyotakiwa na pendekezo la nchi 6 na azimio namba 1696 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lakini Iran itaeleza nia ya kuendelea na mazungumzo na Umoja wa Ulaya kwa msingi wa pendekezo la nchi 6.
Lakini je, jibu la namna hii litakubaliwa na nchi za magharibi? Wachambuzi wanaona kuwa nchi za Ulaya labda zitalikubali, lakini Marekani itaonesha msimamo mkali. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Nicholas Burns tarehe 19 alionya kuwa, kama Iran haitatekeleza azimio la baraza la usalama, basi Marekani itajitahidi kuiwekea vikwazo. Lakini iwapo Iran itachukuliwa hatua zaidi vikiwemo vikwazo, nchi hiyo itaweza kuchukua hatua kali za kupingana, kama vile kujitoa kutoka kwenye Maktaba wa kutosambaza silaha za nyuklia, jambo ambalo hakika litafanya mzozo wa nyuklia kati ya Iran na Marekani upambe moto zaidi. Na nchi nyingi duniani hazifurahii matokeo ya namna hii, kwani yanaweza tu kuleta vurugu na kutakuwa hakuna mshindi kamili katika vurugu hizo.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-22
|