Tarehe 22 Agosti Iran ilitoa rasmi waraka wa majibu kwa pendekezo la kutatua suala la nyuklia la Iran lililotolewa na nchi 6 za Marekani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Mambo yaliyomo kwenye waraka huo bado hayajajulikana lakini kwa mujibu wa vyombo vya habari, Iran imetoa pendekezo jipya la kutatua suala hilo, pia imetoa jibu kamili kwa pendekezo la nchi 6. Mwakilishi mkuu wa mazungumzo ya kinyuklia wa Iran Bw. Ali Larijani siku hiyo alisema, nchi yake inapenda kufanya haraka "mazungumzo kwa makini" na nchi 6. Mpaka sasa hakuna dalili kuwa, Iran itasimamisha shughuli za kusafisha uranium kama inavyodaiwa na pendekezo la nchi 6. Jibu la namna hii la Iran la kukwepa suala kuu hakika halitakubaliwa na nchi za magharibi, hususan Marekani. Mwelekeo wa suala la nyuklia la Iran kabla ya tarehe 31 Agosti unafuatiliwa na watu.
Tarehe 31 Agosti ni siku muhimu, kwani hii ni siku ya mwisho iliyowekwa kwenye azimio namba 1696 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Kama Iran haitasimamisha shughuli za kusafisha uranium hadi tarehe 31 Agosti, Marekani na Umoja wa Ulaya zitaanza kuchukua hatua za kuiwekea vikwazo Iran. Marekani ina msimamo imara juu ya jambo hilo. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Bw. John Bolton tarehe 22 alitoa onyo kwamba, iwapo Iran haitatoa jibu linaloridhisha, basi Marekani itawasilisha kwa haraka mswada wa azimio la kuiwekea vikwazo vya kiuchumi kwenye baraza la usalama.
Je, Iran ingeweza kuchukua hatua gani kabla ya tarehe 31 Agosti? Wachambuzi wameeleza hali za aina tatu zitakazoweza kutokea. Katika hali ya kwanza, Iran itaweza kurudi nyuma kabla ya siku hiyo na kusimamisha shughuli zake za kusafisha uranium nzito. Lakini hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali mpya ya Iran katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani, na kauli zilizotolewa na maofisa waandamizi wa Iran hivi karibuni zinaonesha kuwa, hakuna uwezekano wa namna hii. Katika hali ya pili, Iran itachukua hatua zenye msimamo mkali, zikiwemo kusimamisha ushirikiano na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki na kujitoa kutoka kwenye Mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia. Hata hivyo hali hiyo pia inaonekana haitatokea kabisa, kwani si lazima kwa Iran kufuata njia hiyo ambayo si ya busara kwa kujitenga kabisa na jumuiya ya kimataifa, na kujifanya kuacha kabisa nafasi za kurudi nyuma. Katika hali ya tatu, Iran itaendelea na mbinu ya hivi sasa, yaani kwa upande mmoja inashikilia haki yake ya kujiamulia kuhusu shughuli za kusafisha uranium nzito, kwa upande mwingine haitafunga kabisa mlango wa mazungumzo, ili kujipatia muda mwingi zaidi. Dalili za hivi sasa zinaonesha kuwa Iran itafanya hivyo.
Lakini Marekani na Umoja wa Ulaya hazitavumilia mbinu hiyo ya Iran ya kujipatia muda mwingi zaidi. Kwa hakika zitashirikiana kulishinikiza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Iran. Basi mpira utarudi kwenye baraza la usalama. Baraza hilo litachagua ni vikwazo vya namna gani viwekwe dhidi ya Iran. Itaweza kuwa vikwazo hivyo havitakuwa na madhara makubwa, ambavyo ni pamoja na kupiga marufuku kushiriki kwenye michezo ya kimataifa, kuzuia ndege za Iran zisitue kwenye sehemu fulani, kupiga marufuku ziara za viongozi wa Iran katika nchi za nje, na kutowapa maofisa waandamizi wa Iran viza vya kuingia kwenye nchi nyingine. Vikwazo vingine vinahusiana na mambo halisi, kama vile vikwazo vya kuiuzia Iran zana za kijeshi au za mafuta ya petroli na vikwazo vya fedha. Lakini suala hilo la vikwazo linahusiana na maslahi ya nchi mbalimbali, kwa hiyo katika mjadala utakaofanyika kwenye baraza la usalama nchi mbalimbali zitakuwa na maoni tofauti, na itakuwa si rahisi kupitisha azimio la kuiwekea Iran vikwazo kama inavyotarajiwa na Marekani. Wachambuzi wanasema hali ya mvutano katika suala la nyuklia haitakwisha hata kama vikwazo fulani vitawekwa, na mvutano huo kati ya Marekani na Iran utaendelea na kuwa mkali zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-23
|