Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-23 21:19:58    
Msomi wa Kenya azungumza utungaji wa ushairi

cri

Mwandishi wetu wa habari aliyeko huko Kenya Bwana Ali Hassan hivi karibuni alifanya mahojiano na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Bw. Hamisi Babusa, ambaye pia ni mshairi maarufu wa Kenya kuhusu utungaji ushairi. Yafuatayo ni mahojiano kati yao, hebu sikilizeni.

Ali: Kwanza naomba utueleze ukiwa ni mtunzi wa mashairi na mhadhiri wa mambo hayo, je una jina la ushairi (lakabu)?

Babusa: Ndiyo nina jina langu la ushairi, naitwa gwiji wa mashairi ama gwiji wa matungo.

Ali: Ulianza lini kujihusisha na mambo ya ushairi?

Babusa: Ushairi nilianza tangu nikiwa darasa la saba. Nakumbuka mwalimu wangu alituambia kuwa kila mwanafunzi atunge beti mbili ama beti tatu za shairi. Sikujua kama naweza kutunga mashairi lakini kweli naimba mashairi ya watunzi kama vile "Kilimani". Nilipoambiwa na mwalimu nitunge shairi, nikakuta tu nimetunga shairi lenye beti saba hivi. Ndipo nikagundua kuwa nina kipawa cha kutunga shairi, kuanzia hapo sikuacha kutunga mashairi.

Ali: Mshairi gani amekuchochea zaidi katika utunzi?

Babusa: Washairi ninaowapenda sana ni Bw. Mathias Mnyambala wa Tanzania, mashairi yake mazito sana, halafu beti zake anazipanga vizuri, huyu alinifanya nikashika ushairi kabisa. Mshairi mwingine ni Bwana Ahmed Nasiri huyo naye amenitia moyo, na mwingine ni Ablatifa Abdallah. Hawa washairi watatu kwangu ndio ni mafundi wa tungo za Kiswahili.

Ali: Bwana Babusa, unapotunga mashairi yako unaegemea zaidi upande gani? Labda mahaba, matatizo ya kijamii, umasikini, na vitu kama hiyo?

Babusa: Mimi najaribu kuzunguka kote, kama ni mahaba nimeyatunga, matatizo ya kijamii, mambo ya siasa nimeyatunga, kwa hivyo natunga shairi lolote, siegemei upande wowote.

Ali: Unafikiri ushairi una nafasi gani katika jamii?

Babusa: Ushairi ni kama wimbo, ni vile tu watu wanasikiliza sana, hawajafuatilia sana ushairi wa Kiswahili, hata vyuoni utawakuta wanafunzi wanalemewa na mashairi wa Kiswahili, watunzi pia unakuta wengi wameingia katika upande wa ushairi huru, ambapo ni kuharibu zile kanuni za ushairi. Hasa ushairi inafaa uchukuliwe kama ni wimbo, wimbo ambao hauna ala za muziki, kwa hivyo zile nafasi za nyimbo zinazopigwa kwenye radio, kanda za video, ni ushairi uwe katika hali hiyo hiyo, lakini vile tu haujachukuliwa ala juu, lakini nafasi za ushairi inaweza kuchukuliwa kama nafasi ya wimbo ambao hauna ala.

Ali: Mtu anaweza akajiajiri kwa kuandika mashairi?

Babusa: Hivi sasa ni vigumu sana kwa sababu kwanza hapa Kenya kama ujuavyo watu hawafuati sana mambo ya Kiswahili, wanafuata mambo ya kizungu kizungu. Ukiwa ndiyo mshairi kama wa Kiingereza, unaweza kujiajiri. Lakini mshairi wa Kiswahili inakuwa vigumu kwa sababu hapa Kenya bado tunadunisha lugha ya Kiswahili.

Ali: Una ushauri gani kwa watu wanaopenda mambo ya ushairi?

Bbusa: Atunge mashairi, na baada ya kutunga pengine aangalie upande wa uchapishaji, na ajifunze pia kuyaimba, kwa sababu ukiwa na kipawa cha ushairi inamaanisha kwamba, una kipawa cha kutunga nyimbo au kuimba. Kwa hivyo akiona kama ushairi pengine umemlemea anaweza kuingia kwenye upande wa nyimbo zenye ala, kwa sababu nyimbo hizo zinajulikana. Nyimbo pia ni mashairi.

Ali: Mpangilio yupi uliopo kati ya taarabu na ushairi

Babusa: Taarabu zimepangika kwa beti na zina kibwagizo, ni moja kwa moja, sema nyimbo za zamani ndiyo ushairi wake kidogo, ni ushairi huru ama huu muziki wa kufokafoka. Nyimbo zao ukiangalia na kusikiliza vizuri utaona ni mashairi yenye vina na mizani wameyapanga vizuri. Kwa sababu nyimbo zao haziishi utamu, ni vizuri kuliko zile za kufoka ambazo hazijapangwa vizuri, zinaisha baada ya wiki moja wiki mbili.