Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-24 16:23:06    
Daktari aliyepata heshima kutoka kwa wagonjwa kutokana na kushikilia maadili ya udaktari

cri

Daktari Hua Yiwei aliyekuwa na umri wa miaka 73 alifariki dunia jioni ya tarehe 12 Agosti baada ya kuugua ugonjwa wa saratani kwa siku zaidi ya 380. Hata alipokuwa amelazwa, daktari huyo alikuwa anaweka kumbukumbu kuhusu alivyokuwa anajisikia kutokana na dalili za ugonjwa, ili ziwasaidie wagonjwa wengine katika matibabu yao.

Hua Yiwei alizaliwa mwaka 1933katika familia ya madaktari huko Tianjin, mji wa bandari uliopo kaskazini mwa China. Wazazi wake walikuwa ni madaktari mashuhuri wa huko. Na mtoto wao Hua Yiwei alichagua udaktari kuwa kazi atakayofanya katika maisha yake yote.

Daktari Hua Yiwei alipohojiwa alisema, "Sina ndoto nyingine bali nataka kuwa daktari hodari anayeweza kuondoa maumivu ya wagonjwa na kupata imani yao. Hii ni furaha kubwa kwangu."

Bw. Hua Yiwei alikuwa anatekeleza ahadi hiyo katika kipindi cha miaka 56 alipokuwa daktari. Yeye alikuwa ni daktari mashuhuri, na aliwafanyia upasuaji maelfu ya wagonjwa kwa mafanikio, na alifanya kila upasuaji kwa makini na kuwashughulikia wagonjwa kwa moyo wa dhati.

Katika upasuaji wa tumbo, kuna uwezekano wa kuokoa muda na nguvu ya daktari kwa kutumia zana za kushonea vidonda, lakini kama zana hizo zikitumika wagonjwa wanapaswa kulipa hata Yuan elfu 20 zaidi ya gharama za kawaida. Ili kupunguza gharama kwa wagonjwa wenye matatizo ya kifedha, daktari Hua Yiwei alikuwa anashona vidonda kwa mikono, hatua ambayo ilimchukua saa 5 hivi kila mara.

Daktari mwenzake Bw. Zhang Dongsheng alisema "Ana msingi imara wa kufanya upasuaji na mikono yake ni hodari katika ustadi wa kushona vidonda, ustadi wake unalingana na uwezo wa zana maalumu za kushonea vidonda."

Katika miaka yote 56 ya udaktari wake, Bw. Hua Yiwei hakufanya kosa hata moja katika kazi yake. Kabla ya kufanyika kwa upasuaji, alikuwa anashikilia kufahamu kwanza kuhusu hali ya wagonjwa na kurudia mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika upasuaji. Kamwe hakufanya uzembe, hii ilikuwa ni sababu kubwa ya yeye kutofanya makosa.

Mbali na ustadi mzuri wa kitaaluma, madaktari hodari wana sifa inayofanana, yaani moyo wa upendo kwa wagonjwa. Daktari Hua Yiwei alikuwa anawafuatilia wagonjwa hata katika mambo madogomadogo. Alipowapimia afya, kwanza alishika chombo cha kupimia mapafu (stetockopu) mkononi mwake ili kiwe na ujoto unaolingana na hali ya mwili wa mgonjwa. Kabla ya wagonjwa kufanyiwa upasuaji, daktari Hua Yiwei alitangulia kufika kwenye chumba cha upasuaji, akiwasaidia wagonjwa kulazwa vizuri na kufanya maandalizi ya upasuaji. Baada ya upasuaji kukamilika, daktari huyo akishirikiana na wauguzi, walikuwa wanawapeleka wagonjwa kwenye wodi, na wagonjwa walipoamka walimwona daktari Hua Yiwei akisubiri wodini, akiwauliza wanavyojisikia baada ya upasuaji. Daktari Hua Yiwei alikuwa anashikilia kufanya mambo hayo madogomadogo ambayo yalikuwa hayazingatiwi na madaktari wengine katika miaka yote 56 ya udaktari wake.

Tarehe 25 Julai mwaka 2005, daktari huyo alifanya upasuaji wake wa mwisho, mgonjwa alikuwa mwanamke aitwaye Yang Hua, ambaye bado anakumbuka siku alipofanyiwa upasuaji. Alipohojiwa alisema "Daktari Hua alikuwa yupo mlangoni, akinisalimia kwa kichwa. Naona alikuwa anaonesha mwenendo mzuri wa kitaaluma, yeye pia ni mpole, ambaye anakupa matumaini."

Lakini Bibi Yang Hua hakujua kuwa, wakati huo huo daktari Hua Yiwei alikuwa anadhaniwa kuwa na saratani ya tumbo, na siku hiyo hiyo alishikilia kwanza kumfanyia upasuaji mgonjwa wake, baadaye yeye mwenyewe alipimwa afya. Siku ya pili daktari Hua Yiwei alilazwa katika wodi, na siku nane baadaye tumbo lake lililokuwa na chembechembe za saratani lilifanyiwa upasuaji, ili kuondoa chembechembe hizo.

Daktari Hua Yiwei aliwapa wenzake picha ya tabasamu siku zote. Lakini alipolazwa na wagonjwa wake walipomtembelea, alionekana kuwa na masikitiko kwa kushindwa kuendelea kuwahudumia wagonjwa. Bw. Hua Yiwei aliwaomba wenzake wawaambie wagonjwa waliokuwa wamewekwa katika mpango wa kufanyiwa upasuaji naye wamwie radhi, kwani alikuwa hawezi kutekeleza ahadi zake.

Baada ya kupata habari ya kuumwa kwake, watu wengi aliowahi kuwatibu walikwenda kumtembelea hospitalini.

Bibi Liu Jurong alisema "Mwuguzi aliniambia kuwa daktari Hua amelala usingizi, nisiingie kumwona. Nilisema fungua mlango kidogo namwangalia kwa dakika mmoja tu. Nilikuwa na nia ya kumwangalia na kumwinamishia mwili wangu mara tatu."

Mgonjwa mwingine Bibi Wang Hongmin alisema "Sifahamu kwa nini Mungu hatendi haki. Kama watu wangeweza kubadilishana magonjwa, basi ningeumwa badala ya daktari Hua."

Mgonjwa Bibi Yang Hua alisema "Nilikwenda kwenye hekalu kumwomba Mungu ampatie baraka daktari Hua. Nilitarajia mwuujiza utokee apate ahueni, asije akasumbuliwa vibaya na ugonjwa."

Alipolazwa Bw. Hua Yiwei alikuwa anafuatilia matibabu. Wakati anasumbuliwa na saratani, aliweka kumbukumbu za hali mbalimbali zilizotokea katika kipindi alipopata matibabu, alitumai kuwa kumbukumbu hizo zitawasaidia wagonjwa wengine wenye ugonjwa kama wake. Pia aliamua mwili wake utumike kwa ajili ya uchunguzi, na alimwomba profesa mwenzake Ding Huaye afanye jambo hilo.

Profesa Ding Huaye alipohojiwa alisema "Aliniambia jambo hilo wakati nipo kando ya kitanda chake. Alisema amefanyiwa upasuaji wa kuondoa tumbo lakini baadaye zilijitokeza hali mbalimbali mbaya, hali ambayo haikutokea katika miaka yote ya udaktari wake aliposhughulikia saratani ya tumbo. Kwa hiyo alitaka mwili wake ufanyiwe uchunguzi ili kupata chanzo kilichosababisha kutokea kwa hali hiyo, hii itaweza kusaidia matibabu ya siku za baadaye."

Daktari Hua Yiwei alitumia miaka yote 56 ya udaktari wake kutekeleza ahadi aliyotoa ya kuwa daktari hodari. Maadili yake ya kitaaluma yalisifiwa na watu wengi, akiwemo rais Hu Jintao wa China, ambaye alikwenda kumtembelea daktari huyo katika wodi yake na kumpa salamu na pole.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-24