Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-25 15:18:25    
Mazungumzo ni njia pekee ya kutatua suala la nyuklia la Iran

cri

Baada ya Iran kujibu mapendekezo ya nchi sita za Marekani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani tarehe 22 Agosti, Russia na China kwa nyakati tofauti zimesema zinatumai suala la nyuklia la Iran litatatuliwe kwa njia ya mazungumzo kwa msingi wa mfumo wa kimataifa wa kutoeneza silaha za nyuklia, na hili pia ni tumaini la nchi nyingi na maoni yanayotawala katika jamii ya kimataifa.

Shughuli za nyuklia za Iran zilianza katika miaka ya 50 ya karne ya 20 na shughuli zake za nyuklia ziliungwa mkono na Marekani na nchi nyingine za magharibi. Mwaka 1980 baada ya kuvunjwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Marekani na Iran, Marekani mara nyingi iliishutumu Iran kuendeleza silaha za nyuklia kwa kisingizio cha "matumizi ya amani" na kuichukulia Iran sera ya kuidhibiti. Kwa hiyo kwa kweli suala la nyuklia la Iran ni mgongano wa uhusiano wa nchi hizo kushindwa kuvumiliana. Iran kwa muda mrefu inaipinga Marekani na kuichukulia kama ni tishio kubwa kwa usalama wake, na Marekani inaichukulia Iran kama ni hatari kubwa inayoficha kwa Marekani. Kwenye "ripoti kuhusu usalama wa taifa" Marekani imesema "Iran ni nchi pekee ambayo ni tishio kwa Marekani".

Suala la nyuklia la Iran ni suala lenye utatanishi mkubwa. Kutokana na uchunguzi wa kina wa miaka mitatu, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki halikugundua kuwa Iran ilitumia nyenzo za nyuklia kutengeneza silaha, na shirika hilo pia halina ushahidi wowote ukionesha Iran ina nyenzo zozote ambazo hazijaripotiwai au shughuli zozote za nyuklia zisizo za wazi.

Kutokana na hayo kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya Iran sio wakati mwafaka, na wala haitasaidia chochote kutatua suala la nyuklia la Iran. Na pia hatua ya kuiwekea vikwazo vya kiuchumi pia haiwezi kutatua suala hilo kikamilifu. Baada ya kuanzisha vita dhidi ya Iraq na Afghanistan, kama Marekani ikianzisha vita vingine, licha ya kuwa vita hivyo vitapingwa na jumuyia ya kimataifa, pia havitakuwa na hali nzuri kuliko vilivyokuwa nchini Iraq na Afghanistan. Iran ina athari kubwa kwa madhehebu ya Shiya na ina uhusiano mzuri na chama cha Hezbollah cha Lebanon, Kundi la Hamas la Palestina na Jihad ya Waislamu. Iwapo Marekani ikianzisha vita dhidi ya Iran hakika itasababisha hali mbaya isiyoweza kudhibitika katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Wachambuzi wanaona kwamba chama tawala cha Republicn cha Marekani kikitaka kupata ushindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu, serikali ya chama hicho lazima kipige hatua katika utatuzi wa suala la nyuklia la Iran. Hii ni moja ya sababu kwa Marekani kutaka kuharakisha hatua zake za kuiwekea vikwazo Iran. Hata hivyo, hatua za vikwazo ni kama upanga wenye makali kwenye pande mbili, kwamba unaweza kumuumiza mwingine na kujiumiza mwenyewe. Iran ni nchi ya nne inayozalisha mafuta kwa wingi duniani na ni nchi ya pili katika OPEC. Vikwazo kwa Iran hakika vitapandisha bei ya mafuta duniani. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la LAND la Marekani, kama Iran itapunguza uzalishaji wa mapipa laki tano kwa siku bei ya mafuta duniani itazidi dola za Kimarekani 100 kwa pipa na kuathiri uchumi wa dunia. Mwaka 2004 Umoja wa Ulaya uliingiza mafuta kutoka Iran yenye thamani ya dola za Euro bilioni 8.2 na asilimia 80% ya mafuta hayo ni kwa ajili ya nishati, na katika mwaka huo, 15% ya mafuta nchini Japan yaliingizwa kutoka Iran. Ni dhahiri kwamba vikwazo vikiwekwa dhidi ya Iran, uchumi wa nchi za Magharibi utaathirika.

Aidha, hali itakuwa mbaya zaidi kama Iran ikifunga mlango wa bahari wa Hormuz, njia ya kusafirisha 20% ya mafuta duniani itakatwa, uchumi wa dunia utaathirika vibaya. Wataalamu wamekadiria kwamba kama mlango huo wa bahari ukifungwa kwa miezi mitatu na Iran ikisimamisha kutoa mafuta, thamani ya bidhaa itapungua kwa 4% hadi 5% na kiasi cha ukosefu wa ajira kitaongezeka kwa 2% nchini Marekani.

Bila shaka uchumi wa Iran utapata hasara kama vikwazo vikitekelezwa. Katika miaka ya karibuni, kutokana na hali ya wasiwasi, Iran imepoteza wawekezaji wengi wa nchi za nje, ukata wa fedha unazorotesha uchumi wa Iran na hali ya mfumuko wa bei na kiasi kikubwa ya ukosefu wa ajira inaendelea kwa muda mrefu nchini Iran.

Kwa ujumla, hatua za kijeshi au vikwazo vya kiuchumi, vyote havitasaidia utatuzi wa suala la nyuklia la Iran ila tu vitaleta hasara kwa pande zote mbili. Lakini kama pande mbili zikishikilia kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo itasaidia kulinda amani ya Mashariki ya Kati, amani na uchumi duniani na itakuwa na faida kwa pande zote mbili.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-25