Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-28 14:16:41    
Mapango ya mawe wilayani Longyou

cri

Leo tunawaongoza kwenda Wilaya ya Longyou kutembelea mapango ya mawe.

Wilaya ya Longyou iko mkoani Zhejiang, mashariki ya China. Zaidi ya miaka 10 iliyopita mapango mengi ya mawe yaliyoko chini ya ardhi yaligunduliwa katika wilaya hiyo, mapango hayo si kama tu yamechochea hamu kubwa ya wataalamu wa taaluma hiyo, pia yamewavutia watalii wengi.

Mapango ya mawe ya Longyou yako katika kijiji cha Shiyanbei, kaskazini ya Wilaya ya Longyou, watalii wakipanda basi kutoka mji wa wilaya watafika Longyou baada ya dakika 5 tu. Katika sehemu ya Mapango ya mawe ya Longyou, kuna milima na mito pamoja na miti mingi. Katika zama za kale, wanakijiji waligundua madimbwi mengi ya maji milimani, maji ya madimbwi hayo ni safi sana, na kina cha madimbwi hayo ni kirefu sana.

Siku za joto mwaka 1992, wakulima kadhaa walitaka kutumia maji ya madimbwi hayo kumwagilia mashamba yao, wakatumia pampu kuvuta maji ya dimbwi moja kutwa kuchwa, hadi siku ya 4, waliona ngazi za mawe zilionekana ndani ya dimbwi, na walipovuta maji hadi siku ya 9 waliona nguzo mbili kubwa za mawe zilizo kama mifupa ya migongo ya samaki zilijitokeza kwenye uso wa maji, na walipovuta maji ya dimbwi hadi siku ya 17, waliona ukumbi mkubwa wa mawe chini ya ardhi ulionekana wazi.

Baada ya kugunduliwa kwa pango hilo la mawe, wanakijiji wa Kijiji cha Shiyanbei wakaongeza hamu zaidi za udadisi, wakatumia pampu kuvuta kabisa maji ya madimbwi 7, wakagundua mapango 7 ya mawe chini ya ardhi. Mapango hayo 7 ya mawe yanaegemeana moja baada ya lingine kwenye safu moja, na miundo ya mapango yote karibu ni sawasawa, ila tu ukubwa wa kila pango ni tofauti. Lakini jambo la ajabu ni kuwa, katika mapango hayo 7 ya mawe, mbali na sanamu moja ya mawe isiyo na kichwa, hakuna mabaki mengine yoyote ya kale.

Mtaalamu wa Taasisi kuu ya uhandisi ya China Bwana Wang Sijing alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema, mwanzoni mwa kugunduliwa kwa mapango hayo ya mawe, wanakijiji wa Kijiji cha Shiyanbei walikuwa na mashaka mengi juu ya mapango hayo ya mawe yaliyo makubwa na ya giza, hata hawakutambua kuwa wamegundua kundi kubwa zaidi duniani la mapango ya mawe chini ya ardhi. Bwana Wang alisema:

Nilipotembelea mapango hayo ya mawe kwa mara ya kwanza nilistaajabishwa na mapango hayo yaliyochimbuliwa na mababu zetu wa zama za kale, kweli si rahisi kufikiria uzoefu na akili zao jinsi zilivyoweza kufikia kiwango cha juu ya namna hii, mapango hayo ya mawe yalichimbuliwa vizuri kwa kushangaza watu.

Bwana Wang alisema, mapango hayo ya mawe yaliyogunduliwa, kila moja ni ukumbi mmoja mkubwa chini ya ardhi, na eneo la kila ukumbi ni zaidi ya mita 1000. Na kwenye sakafu ya kila pango kuna mashimo mawili ya mawe na mteremko mmoja, ambapo nguzo kubwa za mawe zinahimili dari la pango, ndani ya pango kubwa kuna nguzo 4 za mawe, na ndani ya pango dogo kuna nguzo moja ya mawe, pango lenyewe ni lenye umbo la kizoleo kinachopinduka. Ndani ya pango la mawe pia kuna ngazi za mawe, ngazi hizo zinaelekea mpaka kwenye ardhi. Jambo linalowashangaza watu ni kuwa, mpangilio wa mapango 7 ya mawe ni sawasawa na mpangilio wa sayari Big dipper yaani nyota kubwa kwenye mbingu ya kaskazini.

Kwenye kuta za mapango ya mawe, pia kuna picha kadhaa zisizoeleweka ambazo zinaonekana kama zina maana fulani ya siri. Katika kuta fulani ilichongwa michongo ya farasi, ndege, na samaki, na sanamu za wanyama zilizochongwa katika ukuta mwingine ni zenye maumbo ya ajabu, hata sanamu za ndege zilizochongwa ni zenye shingo ndefu mara kadhaa kuliko urefu wa mwili wa ndege. Katika sehemu iliyoko kwenye umbali wa kilomita moja kutoka pembezoni mwa mapango hayo 7 ya mawe yaligunduliwa pia mapango 24 ya mawe yanayofanana na mapango hayo 7.

Naibu mkurugenzi wa taasisi ya elimu ya nguvu ya miamba na elimu ya uhandisi ya China Bwana Yang Linde aliingia mara kadhaa ndani ya mapango ya mawe ya Longyou. Alisema kutokana na utafiti wake, kila pango la mawe lilijengwa kwa mujibu wa mpango kamili wa usanifu, mapango hayo yanaegemeana kutoka juu hadi chini, na kutoka kushoto hadi kulia, lakini kila pango linajitegemea na halipitani na lingine, ustadi murua wa hesabu na upimaji wa ujenzi wa mapango chini ya ardhi unawashangaza sana watu wenye teknolojia ya kisasa katika zama tulizo nazo. Alisema:

Kila nilipoingia kwenye mapango hayo ya mawe nilivutiwa kweli, naona mapango hayo ya mawe ni mavumbuzi ya wafanyakazi hodari wenye ustadi murua wa China ya kale, ambayo yana thamani kubwa kwa kuonesha historia ya ustaarabu wa China ya kale.

Bwana Yang Linde alisema mapango ya mawe ya Longyou yanastahili kusifiwa kuwa ni miujiza katika elimu ya sayansi na elimu ya ubora. Kwa mfano mpangilio wa mapango ulifuata utaratibu, kwa mtizamo wa zama tulizo nazo, mapango hayo bado yanaonesha thamani yake ya kufanyiwa utafiti; na uwekaji wa nguzo zinazohimili madari ya mapango unalingana kabisa na sehemu za nguvu za mihimili ya mapango. Ufundi waliokuwa nao wachimbaji wa mapango hayo ya mawe wa zama za kale kweli unawastaajabisha sana watu wa zama za hivi sasa.

Madhumuni ya kuchimbuliwa kwa kundi kubwa namna hii la mapango hayo ya mawe chini ya ardhi hayajulikani mpaka sasa. Watu fulani walisema mapango hayo yalikuwa makaburi ya wafalme wa zama za kale, wengine walisema hayo ni mapango ya mawe yaliachwa na watu wa zama za kale baada ya kuchimba mawe na kuyachukua, wengine wanasema mapango hayo yalikuwa ghala za kulimbikiza chakula katika zama za kale na kadhalika. Ingawa maoni hayo yaliyodhaniwa na watu yalitokana na sababu fulanifulani, lakini mpaka sasa hazijagunduliwa kumbukumbu za maandishi na haujapatikana ushahidi wa utafiti wa kisayansi unaoweza kuthibitisha madhumuni yaliyodhaniwa na watu wa hivi sasa.

Ukubwa na mpangilio wa mapango ya mawe ya Longyou, ama usanifu na ustadi murua wa ujenzi, ama thamani za aina mbalimbali za mapango hayo, yote ni nadra kupatikana duniani. Ingawa wanasayansi wa China walifanya utafiti kwa kina juu ya mapango hayo, lakini hivi sasa bado hawajaweza kuelewa zaidi mambo husika ya mapango hayo, na bado hakuna mtu anayeweza kutafsiri vizuri maswali mbalimbali. Kwa mfano watafiti wa mabaki ya kale wa China walithibitisha kuwa mapango hayo yalichimbuliwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita, lakini yalichimbuliwa katika miaka gani na enzi gani, na kuchimbuliwa na watu gani kwa vyombo gani, watafiti bado hawajapata hoja sahihi juu ya maswali hayo.

Maswali yenye maajabu na yasiyoeleweka kuhusu mapango ya mawe ya Longyou yamewavuta watalii wengi wa nchini na nje wafike kwenye mapango hayo kutafuta majibu. Mtalii kutoka Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ya kaskazini ya china Bibi Zhang Gu alisema:

Mapango hayo yanayostaajabisha watu yananivutia sana, nakuja kuyatembelea nikiwa na heshima kubwa kwake.

Na watalii wengi kutoka nchi za nje pia walifika kwenye mapango hayo kuyatembelea. Bibi Soili Vatanen kutoka Finland alimwambia mwandishi wa habari alisema:

Tuliwahi kutembelea mapango hayo ya mawe, tuliona maajabu mengi, zamani sikuwahi kutembelea mapango kama hayo, hata nilikuwa sijui kabisa kama kuna uwezekano wa kuwepo kwa mapango kama hayo duniani, kama nikipata fursa nitakuja China na mkoani Zhejiang kutembelea tena mapango ya mawe ya Longyou.

Idhaa ya Kiswahili 2006-08-28