Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-28 14:31:00    
Mwandishi wa vitabu Su Shuyang

cri

Mwaka huu ni mwaka wa 30 tokea tetemeko kubwa la ardhi lilipotokea mjini Tangshan, China. Siku hizi vitabu vingi kuhusu matetemeko ya ardhi vinachapishwa na kuuzwa madukani, kati ya vitabu hivyo, kitabu cha "Matetemeko ya Ardhi Niliyoshuhudia" kilichoandikwa na Su Shuyang kinanunuliwa zaidi.

Siku chache zilizopita, duka kubwa la vitabu la Wangfujing mjini Beijing lilimwalika mwandishi huyo kusaini kwenye vitabu vyake vinaponunuliwa. Baada ya kupata saini wasomaji walimzunguka na kusikiliza akiwasimulia hali ilivyokuwa baada ya matetemeko ya ardhi kutokea mjini Tangshan.

Sun Shuyang ana umri wa miaka 70, hapo zamani nyumbani kwake palikuwa karibu na mji wa Tangshan kwa kilomita mia moja hivi, tetemeko la ardhi mjini Tangshang limemkaa sana akilini mwake. Baada ya shughuli za kuweka saini kwa wasomaji wake alihojiwa na waandishi wa habari alisema, "Tarehe 28 Julai, mwaka 1976 matetemeko makubwa ya ardhi yalitokea mjini Tangshan, hili ni tukio kubwa katika historia ya China. Tukio hilo lilitokea kwa ghafla lilileta maangamizi makubwa kwa wakazi laki kadhaa wa mji huo, jinsi serikali ilivyoshirikisha haraka watu wa fani mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali kufanya uokoaji na jinsi kuwasaidia walionusurika kujenga makazi na kuwapatia maisha mapya ni mambo yasiyosahaulika. Nadhani kitabu changu kitawasaidia watu ambao hawakukumbwa na maafa hayo kufahamu jinsi hali ilivyokuwa ya kuhuzunisha baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, na kitabu hicho pia kitakuwa ni kumbukumbu isiyosahaulika kwa watu walionusurika katika janga hilo."

Bw. Su Shuyang alizaliwa mwaka 1938, alikuwa na tabia ya kuangalia mambo ya jamii kwa makini toka alipokuwa mtoto. Alipokuwa mwanafunzi wa sekondari alianza kuandika tamthilia akitumai kuwa baadaye atakuwa mwandishi wa tamthilia. Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu alikuwa mwalimu na aliwahi kufundisha katika vyuo vikuu mbalimbali. Alipofundisha katika Chuo Kikuu cha Matibabu ya Kichina aliandika kitabu chake kiitwacho "Vidonge vya Dawa". Hiki ni kitabu cha tamthilia inayoeleza jinsi wataalamu wa dawa za Kichina walivyojitahidi kufanya utafiti na kuendeleza dawa za jadi za Kichina. Maandishi yaliwavutia wasomaji na yalipata tuzo ya kwanza katika maonesho ya taifa ya tamthilia yaliyofanyika mwaka 1979. Bw. Su Shuyang hakutegemea kama kitabu chake kingeweza kupata ufanisi mkubwa namna hiyo. Alisema, "Nilikuwa siamini kabisa, hata magazeti yalipochapisha makala chungu nzima ya kusifu kitabu changu nilikuwa naona kama yanamsifu mtu mwingine. Na vile vile kamwe sikufikiria kuambua chochote kutoka kwenye kitabu changu hicho ingawa ningeweza kuwa mjumbe katika baraza la bunge, katika kamati ya vijana na katika baraza la mashauriano ya kisiasa. Yote hayo nilikataa kwani niliona sistahiki."

Lakini kitabu cha "Vidonge vya Dawa" kweli kilibadilisha maisha yake. Mwaka 1978, Su Shuyang alipokuwa na umri wa miaka 40 aliacha kufundisha na kuwa mhariri katika Studio ya Filamu ya Beijing, wakati huo ulikuwa mwanzo wa mageuzi nchini China, mawazo ya watu yalikuwa yanabadilika badilika. Kwa kutumia nafasi hiyo aliamua kuandika tamthilia ya "Mtaa wa Machweo" kuonesha mabadiliko ya maisha ya wakazi wa Beijing. Alisema, "Nilizingatia hali ilivyokuwa wakati mji wa Beijing ulipokuwa katika mabadiliko hayo. Katika siku za mabadiliko hayo watu walikuwa wanatamani mambo mapya na kuachana na yale ya zamani, lakini wakati huo pia walikuwa na masikitiko walipoagana na ya zamani. Hisia hizo zinaendelea kuwepo hadi sasa. Hisia kama hizo zenye mchanganyiko wa furaha na masikitiko ndio sanaa inayovutia."

Hadithi ya "Mtaa wa Machweo" ilitokea kwenye kichochoro kimoja mjini Beijing, nyumba za miaka mingi kwenye kichochoro hicho zilitakiwa kubomolewa na badala yake yatajengwa majumba ya ghorofa, ambapo wakazi wa hapo walikuwa na matumaini yao tofauti, kijana asiyekuwa na ajira alitumai kufungua duka, walimu mume na mke walitumai kupata nyumba mpya na msichana alitumai kwenda nchi za nje kuona mambo mapya, na mwishowe kwa kusaidiwa na majirani wote walimiza matumaini yao. Nyumba zao zilibomolewa, jumba la ghorofa lilijengwa, ingawa walisikitika kupoteza yale ya zamani waliyozoea, lakini walipata mapya na mazuri.

Tamthilia hiyo ilipooneshwa iliwavutia watazamaji wengi, hali hiyo ilimchochea juhudi zake katika utungaji. Baadaye aliandika maandishi mengi ya riwaya na mashairi ambayo yote yalihusiana na maisha ya wakazi na wasomi wa Beijing. Maandishi hayo mengi yametafsiriwa kwa lugha nyingi za kigeni.

Alipokuwa akielekea kwenye kilele cha mafanikio yake, ugonjwa ulimnyemelea. Mwaka 1994 kutokana na saratani, tumbo lake lilikatwa kwa sehemu, mwaka 2001 pafu lake la kushoto lilikatwa, na 2004 alikatwa wengu, mzee huyo amevumilia pigo kubwa lisiloweza kufikirika. Lakini waandishi wa habari walipozungumza naye hawagundui dalili kuwa alifanyiwa upasuaji mara tatu. Su Shuyang aliwaeleza waandishi wa habari fikra zake katika miaka zaidi ya kumi iliyopita alipougua. Alisema, "Baada ya kupata ugonjwa lazima ukubali ukweli ulipo na utibiwe, usipingane nao bali lazima utibiwe kama unavyotakiwa. Ugonjwa ni kama rafiki yako unayemchukia, anakusumbua kila siku, lakini kwa sababu ugonjwa ingia mwilini mwako inakupasa uutendee inavyostahili, usiwe na hofu bali uwe jasiri wa kuendelea na maisha yako, na nikijaliwa kuishi kwa mwezi mmoja zaidi basi nitapata ushindi wa mwezi mmoja zaidi, na kazi uliyomaliza katika mwezi huo ndio mafanikio mengine yanayokufariji."

Su Shuyang licha ya kuvumilia usumbufu wa ugonjwa bado anaandika, kutumia dawa na kuandika makala ni maisha yake ya kila siku. Mgonjwa huyo katika muda wa miaka 12 ameandika vitatu saba vyenye maneno milioni tatu na hadi sasa zimeuzwa nakala milioni 12.

Kutokana na ugonjwa, Su Shuyang hawezi kuandika tamthilia, lakini akiwa mwandishi wa michezo ya tamthilia anazingatia zaidi utungaji wa tamthilia. Alisema, "Waongoza filamu wa sasa wanakosea kufikiri kwamba filmu nzuri inategemea rangi na ufundi wa kupiga picha tu. Kama filamu za China zikitaka kuimarika, kitu cha kwanza ni maandishi bora ya tamthilia, na maandishi bora yanategemea waandishi waliokuwa na elimu ya pande nyingi na ya kina."

Bw. Su Shuyang alisema, mambo yote yakiwa mema au mabaya yachukuliwe kuwa ni marafiki zako na uyatendee kwa moyo mwepesi. Hivyo maisha yako yatakuwa ya maana na ya furaha.

Idhaa ya Kiswahili 2006-08-28