Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-28 19:52:49    
Mgogoro kati ya Iran na Marekani wapamba moto siku hadi siku

cri

Azimio No. 1696 lililopitishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linaitaka Iran iache shughuli za kusafisha uranium kabla ya tarehe 31 mwezi Agosti. Kutokana na kukaribia kwa siku hiyo, mvutano kati ya Marekani na Iran unapamba moto siku hadi siku.

Baada ya kinu cha maji mazito cha Iran kukamilika na kuanza kufanya kazi tarehe 26 mwezi Agosti, jeshi la baharini la Iran linalofanya luteka kwa kiwango kikubwa tarehe 27 lilirusha tena kwa mafanikio makombora ya masafa marefu dhidi ya manowari za kijeshi. Marekani imedai kuwa kama Iran haitaacha shughuli za kusafisha uranium ifikapo tarehe 31 Agosti, Marekani itaiwekea vikwazo Iran kwa kupitia Baraza la usalama, na kama juhudi zake hizo zinashindwa, basi Marekani itaunda "muungano huria" kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi.

Habari zinasema kinu hicho kipya cha Iran kinaweza kuzalisha tani 16 za maji mazito kwa mwaka, kiasi ambacho ni maradufu ya kile cha zamani. Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran alipotoa hotuba kwenye uzinduzi wa kiwanda hicho alisema: "wananchi wa Iran watalinda haki yao ya kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa njia ya kijeshi."

Kwa kuwa plutonium hupatikana kutoka kwenye nishati zilizotumiwa kwenye kinu cha kuzalisha maji mazito, hivyo nchi za magharibi zina wasiwasi kuwa Iran huenda itatumia plutonium kutengeneza silaha za nyuklia. Lakini azimio No.1696 linaitaka Iran iache shughuli zote zinazohusu kusafisha uranium, wala siyo kuacha ujenzi wa kiwanda au kinu cha maji mazito. Zaidi ya hayo, Iran ilitangaza kujengwa kwa kinu cha kuzalisha maji mazito kabla ya tarehe 31 Agosti. Kitendo hicho cha Iran si kama tu kimeepusha suala nyeti la kusafisha uranium, bali pia kimeonesha nia yake isiyolegea ya kutafiti matumizi ya nyuklia.

Watu wanaona kuwa Iran inapofanya uenezi kuhusu kinu cha kuzalisha maji mazito inadai "kutumia teknolojia ya nyuklia kwa njia ya amani" na "kutatua suala la nyuklia kwa njia ya mazungumzo" ili kujipatia uungaji mkono kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, pia inatumia hali ya kutokuwa na msimamo wa pamoja ndani ya baraza la usalama.

Wakati huo huo Marekani inapanga hatua itakazochukua dhidi ya Iran, kama vile kukabidhi mswada wa azimio la kuchukua hatua za kuiadhibu Iran kwenye baraza la usalama baada ya kwisha kwa muda wa "onyo la mwisho". Au kuunda "muungano huria" ambao ni pamoja na Umoja wa Ulaya na Japan kuweka vikwazo dhidi ya Iran. Marekani inafikiria kuwa kama Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan zinaweka vikwazo dhidi ya Iran kwa pamoja, uchumi wa Iran hakika utaharibiwa vibaya, kwa sababu Iran inatumia fedha za magharibi kufanya biashara ya kimataifa. Marekani pia itadhibiti biashara ya silaha dhidi ya Iran.

Wachambuzi wamedhihirisha kuwa kutokana na kuwepo kwa vizuizi vya aina mbalimbali, hivi sasa Marekani bado haiwezi kuchukua hatua nyingi mwafaka dhidi ya Iran. Habari zinasema ripoti iliyotolewa tarehe 23 Agosti na baraza la chini la bunge la Marekani imesema, habari zilizotolewa na shirika la upelelezi la Marekani kuhusu Iran hazitoshi kabisa, tena habari nyingi kuhusu Iran si sahihi kama ilivyokuwa kabla ya kufanya vita dhidi ya Iraq, hivyo Marekani haiwezi kufanya tathmini sahihi kuhusu uwezo wa Iran wa silaha za nyuklia na kusudi lake la kutengeneza silaha kali.

Serikali ya Iran tarehe 27 ilitangaza kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan tarehe 2 Septemba atafanya ziara nchini Iran, kujadiliana na viongozi wa Iran kuhusu suala la nyuklia na hali ya mashariki ya kati. Kutokana na kuwa baraza la usalama halitaamua hatua ya kuchukua kabla ya kusikiliza ripoti mpya itakayokabidhiwa na mkurugenzi wa shirika la nishati ya atomiki duniani kuhusu suala la nyuklia la Iran, hivyo kabla ya Bw. Annan kufanya ziara nchini Iran, mvutano kati ya Marekani na Iran utaendelea kufuatiliwa na jumuiya ya kimataifa.