Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-29 15:25:48    
Barua 0827

cri

Msikilizaji wetu Bwana Ali Hassan ambaye pia ni mwanahabari wetu aliyeko Nairobi Kenya ametuletea barua yenye kichwa cha "Pongezi kwa CRI kwa kuadhimisha miaka 65 tangu ianzishwe!" Barua hiyo inasema, kwanza kabisa anashukuru mkurugenzi, wasimamizi na wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, kwa kuamua kuwa na matangazo ya kimataifa, lakini zaidi kwa kuwa na wazo la kuanzisha kituo cha FM kwenye masafa ya 91.9, jijini Nairobi Kenya. Hatua hiyo imeibua hisia nzuri kutoka kwa wasikilizaji wa idhaa hii, hasa ikizingatiwa kuwa Radio China Kimataifa sasa inapendwa na wasikilizaji si nchini Kenya tu, bali pia katika nchi nyingine za Afrika.

Pili anapenda kutumia fursa hii kuwapongeza mkurugenzi na wasimamizi wa Radio China Kimataifa kwa kuzindua matangazo yao barani Afrika, na hasa jijini Nairobi, na kuweza kutoa nafasi za ajira! Radio China Kimataifa ikiwa inaadhimisha miaka 65 tangu ianzishwe, ana machache ya kuchangia akiwa mwanahabari wa kwanza Mwafrika nchini Kenya, kufanya kazi katika kituo cha matangazo ya FM cha Radio China Kimataifa.

Anasema anaipongeza Radio China Kimataifa kwa mpangilio wake wa vipindi, mbali na vipindi vya muziki wa Afrika na wa China. Wasikilizaji wengi na mashabiki wa idhaa hii ambao amekutana nao, wamekuwa wakisifu sana mpangilio wa vipindi vya Radio China Kimataifa, vipindi kama vile Salamu zenu, taarifa za habari, na vipindi murua vyenye kufundisha lugha ya Kichina, utamaduni na hali halisi ya maisha nchini China.

Vipindi kama hivi vimewapa wasikilizaji picha halisi ya Mchina na utamaduni wa China kwa ujumla. Akiwa mfanyakazi wa Radio China Kimataifa, amegundua kuwa Mchina ni mtu mwenye heshima na staha kwa mgeni wake. Hilo amelifahamu bayana kutokana na kuambatana mara kadhaa na wafanyakazi wenzake kutoka China katika shughuli mbalimbali za kikazi.

Anasema mchina anapomtembelea mtu, awe waziri au raia wa kawaida, yeye atafanya juu chini walau ashike kijizawadi japo kidogo, cha kumpa mwenyeji wake, au huyo anayekwenda kufanya naye mahojiano, huu ni utamaduni mzuri ulioje! Kadhalika yeye binafsi amevutiwa na mazingira ya kikazi ya Radio China Kimataifa, pamoja na sera yake nzima ya ushirikiano kati ya China na bara la Afrika.

Baadhi ya wafanyakazi wachina ambao amefanya nao kazi katika muda wa kama miezi sita hivi kama vile mabwana Xie na Chen, wamemwonesha kuwa Mchina ni mtu asiye na dharau, kiburi wala majivuno kamwe. Vilevile wamemdhihirishia kuwa Mchina ni mtu ambaye yuko tayari kumfunza mgeni wake utamaduni wa Mchina, na hapo hapo kuujua kiundani utamaduni wa Mwafrika na kuzifanyia utafiti hali za kimaisha za Mwafrika.

Mathalan wenzake hao wamekuwa wakiandamana naye kwenda kwenye chakula cha kichina kwenye mikahawa ya Kichina mjini Nairobi, pamoja na sherehe za mara kwa mara ambapo wasikilizaji wa Radio China Kimataifa hupata nafasi murua ya kukutana na viongozi na watangazaji na kubadilishana nao maoni, na kisha kufurahia vyakula vya kichina katika mazingira mwafaka ya kichina.

Lakini hata hivyo wanasema Waswahili husema kuwa hapana zuri lisilokuwa na dosari. Baadhi ya wasikilizaji wa Radio China Kimataifa, wamekuwa wakimwulizia kama idhaa hii inaweza kuongezea vipindi vya michezo, na hasa kuwapa habari motomoto za michezo ya kitaifa na kimataifa, hasa ligi kadhaa za bara la Ulaya kama vile Ujerumani, Hispania, Uingereza, Italia na Ufaransa, ambazo zinapendwa sana na wakenya, kwa kuwa wachezaji maarufu katika ligi hizo kama vile Didier Drogba wa Cote D'ivoire, Michael Essien wa Ghana, Kolo Toure wa Ivory Coast na wengine wengi wanatoka Afrika.

Tunamshukuru sana mwanahabari wetu Ali Hasaan kwa barua yake, kweli sisi watangazaji na watayarishaji wa Radio China kimataifa tunamshukuru sana kwa kazi anazofanya za kutusaidia kutayarisha vipindi, hasa kila mara ametuletea mahojiano kati yake na wakenya wa sekta mbalimbali, kuwaelezea wasikilizaji wetu habari mbalimbali nchini Kenya, ametusaidia kuboresha vipindi vyetu na kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu. Ni matumaini yetu kuwa siku zijazo tutashirikiana barabara zaidi ili kuandaa vizuri vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Bi. Celestine Mayogi wa sanduku la posta 2995 Kisii, Kenya ametuletea barua akianza kwa kutusalimu, na anasema kuwa yeye ni mzima. Kwenye barua yake anatoa pongezi kwa wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa wanaofanya kazi kuhakikisha kuwa wasikilizaji wanapata matangazo vizuri.

Anasema Radio China kimataifa ndiyo mambo yote, na anasema kuwa anaiombea idumu daima dawamu. Lakini pia anatuambia kuwa kama inawezekana anaomba tumtumie Radio ndogo, kwani yeye wakati matangazo ya Radio China kimataifa yanapokuwa hewani yeye anakuwa shuleni, na matangazo huwa yanampita, na huwa anajisikia vibaya kuona kuwa matangazo yanampita. Kwa hivyo anaomba Radio China Kimataifa imfanyie mpango huo, na pia anaomba tusisahau kumtumia kadi za salamu, kalenda, kitabu cha historia ya Radio CRI toleo la pili la jarida la daraja la urafiki.

Kuhusu ombi lake hilo tutawasilisha kwa ofisi husika ya Radio China kimataifa, kama ikiwezekana tutamsaidia.

Msikilizaji ambaye barua yake huhifadhiwa na Ayub Mutanda wa P.O. Box 172, Bungoma Kenya ametuletea barua akisema, Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa pokeeni Salamu nyingi kutoka Bungoma, Kenya. Pia anasema anashukuru sana kwa kazi zote tunazofanya kwa ajili ya wasikilizaji.

Anasema yeye ni msikilizaji wa vipindi vyetu ambavyo vimemwelimisha saa, sasa hivi yuko katika chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda akiwa anasomea shahada ya mambo ya kijamii, akiwa anasoma somo la sayansi ya kujumuika na sayansi ya siasa. Mwanzoni mwa mwaka huu alikuwa anasoma somo la Kiswahili. Huu ni mwaka wake wa pili chuoni.

Anasema siku moja angependa sana kuwa miongoni mwa wale watakaochaguliwa kuja kufanya kazini nchini China, kwani angependa kufahamu jinsi watu wanavyojumuika katika jamii mbalimbali na kufurahia. Hii ni moja ya sababu ya yeye kushiriki kwenye shindano la chemsha bongo la "Mimi na Radio China Kimataifa".

Anasema akiwa chuoni mjini Kampala Uganda yeye hupata matangazo yetu kupitia tovuti ya Internet: www.cri.cn au www. chinabroadcast.cn. Hata hivyo wakati wa likizo kama hii, yeye hupata matangazo yetu kupitia kituo cha KBC Nairobi. Nchini Uganda amewaeleza marafiki zake kuhusu matangazo haya. Hasa wale wanaopenda matangazo ya kimataifa haswa yanayohusu mambo ya kisiasa. Pia anasema ana furaha kutuambia wao pia hutembelea tovuti yetu na kusoma habari za kimataifa, na hivi karibuni wataanza kuwasiliana nasi.

Anasema pongezi zake ziwaende wote wanaofanya juhudi kuwafikishia habari na matangazo mbalimbali. Kwa hayo anampongeza Bw. Wang Gengnian na kundi lake kwa kazi nzuri. Angependa kusema kuwa hajawahi kuona kituo cha radio kinachowajali na kuwazawadia wasikilizaji kama Radio China Kimataifa. Kwani barua na bahasha tunazowatumia bila malipo zinawawezesha kuwasiliana nasi kwa urahisi, anatuomba tuendelee na roho hiyo.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu David.Sitabuka Fwamba kwa barua yake ambayo imetuelezea mengi kuhusu masomo yake nchini Uganda na usikilizaji wake wa matangazo yetu nchini Kenya na nchini Uganda, na hasa ametusaidia kuwaambia wenzake wa Uganda habari kuhusu matangazo ya idhaa yetu na tovuti yetu, tunamshukuru kwa dhati. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali.

Idhaa ya Kiswahili 2006-08-29