Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-29 16:48:43    
Benki kuu ya China yachukua hatua kudumisha maendeleo endelevu ya uchumi

cri

Benki kuu ya China Jumamosi iliyopita iliongeza riba ya fedha zinazowekwa benkini na mikopo inayotolewa na benki kwa 0.27%, hii ni mara ya pili kwa benki kuu ya China kuongeza riba. Lengo muhimu la kuongeza riba safari hii vilevile ni kuzuia ongezeko kubwa la uwekezaji vitega uchumi na utoaji wa mikopo; kwa upande mwingine utungaji wa sera hizo ulizingatia zaidi upunguzaji wa athari kwa maisha ya umma.

Uchumi wa China umekuwa ukiongezeka kwa zaidi ya 10% tokea mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo uwekezaji kwenye mali zisizohamishika uliongezeka karibu kwa 30% katika nusu ya kwanza ya mwaka huu kuliko kipindi kama hiki mwaka jana, na utoaji wa mikopo wa benki za biashara unakaribia kumaliza 90% ya mpango wa mwaka huu mzima. Uwekezaji mkubwa na wingi wa mikopo ya fedha iliyotolewa zinachagia upanuzi usio wa mwafaka wa baadhi ya sekta ambazo uwezo wake wa uzalishaji mali umezidi mahitaji. Hivyo benki kuu ya China katika mwezi Aprili mwaka huu iliongeza riba ya mikopo kwa 0.27%, licha ya hayo ilirekebisha mara mbili kiwango cha fedha za Renminbi, ambacho benki zinapaswa kuwa nazo mkononi kwa kufuatia kiasi cha fedha zilizowekwa benkini ili kupunguza wingi wa fedha kwenye mzunguko.

Kuhusu benki kuu ya China kuongeza riba tena, mtaalamu wa mambo ya fedha wa kituo cha utafiti wa maendeleo cha baraza la serikali Bw. Xia Bin alisema, kwa kuangalia kutoka kwenye udhibiti wa maendeleo ya uchumi, lengo la kuongeza riba kwa benki kuu ya China pia ni kuzuia ongezeko kubwa kupita kiasi la uwekezaji na utoaji wa mikopo. Bw. Xia alisema,

"Kuongeza riba ni kufuatia hali halisi ya uchumi wa taifa, hususan ni ongezeko kubwa kupita kiasi la uwekezaji katika hali ya kuongezeka kwa haraka kwa akiba ya fedha za kigeni na mitaji ya fedha. Lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa uchumi unakuzwa kwa kasi mwafaka na tulivu. Utoaji mikopo ya muda mrefu unatakiwa ulingane na uwekezaji wa muda mrefu wa mali zisizohamishika, ili kuzuia ongezeko kubwa kupita kiasi la uwekezaji, kwa hiyo riba ya mikopo ya muda mrefu inatakiwa kuongezwa zaidi."

Bw Xia Bin alisema kuongezwa riba ya mikopo ya benki, kutaongeza gharama ya mikopo ya viwanda na kampuni, hivyo kwa kiwango fulani, kutaweza kupunguza uhamasa wa uwekezaji wa viwanda na kampuni na kupunguza kasi ya ongezeko la uwekezaji na utoaji mikopo. Lakini Bw. Xia Bin pia alisema si vizuri kuwa na matumaini ya kuhitimisha lengo la kudhibiti ongezeko la uchumi kwa mbinu hiyo tu, pia hatua nyingine za kurekebisha muundo wa sekta ya uzalishaji mali na kudhibiti ardhi inayotolewa zinapaswa kuchukuliwa.

Ofisa husika alisema ikilinganishwa na mwezi Aprili, kuna tofauti kidogo katika kuongeza riba ya benki ya safari hiyo, ambazo zinaonesha kuwa sera ya uchumi ya serikali inazingatia hali ya watu.

Kwanza kuongeza riba iliyoongezwa katika mwezi Aprili ilikuwa riba ya mikopo inayotolewa na benki, lakini sasa hivi inayoongezwa ni faida kuhusu fedha zilizowekwa na watu benkini pamoja na mikopo inayotolewa na benki, hatua hiyo inamaanisha kuwa wakazi walioweka fedha katika benki kwa muda mrefu watanufaika zaidi kuliko zamani. Baada ya kuongezwa riba, wachina wengi wanaweka fedha zao taslimu katika benki. Mwandishi wetu wa habari katika tawi moja la Benki ya China aliona watu zaidi ya mia moja walioweka fedha zao katika benki siku ya pili baada ya kutangazwa habari kuhusu kuongezeka kwa riba. Mfanyakazi mmoja wa tawi hilo dada Liu Ying alisema,

"Kwa kuwa tarehe 19 ilikuwa siku ya kwanza baada ya kutangazwa kuongezeka kwa riba, watu wengi walikuwa bado hawafahamu vizuri, hivyo watu waliofika benkini hawakuwa wengi, lakini leo watu wameongezeka sana, karibu nusu ya wateja waliofika hapa wanaweka fedha zao benkini kwa muda mrefu."

Lakini mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, watu wengi waliofika huko kuweka fedha zao benkini kwa muda mrefu ni wazee, ambao hawataki kuona hatari ya uwekezaji, hivyo wanafuatilia sana mabadiliko ya kiasi cha riba na kupenda zaidi kuweka fedha zao benkini. Lakini vijana wengi wanasema faida ya fedha zilizowekwa benkini bado ni ndogo sana, kuongeza kwa asilimia 0.27 hakuwezi kuwashawishi kuweka fedha zao benkini badala ya kuwekeza kwa njia nyingine.

Aidha katika mazingira ambayo bei ya nyumba inapanda kwa mfululizo, kuongezeka kwa riba ya mikopo, licha ya kupunguza uwekezaji, kunaleta wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mzigo wa mikopo ya nyumba. Tarehe 26 mwezi Agosti, benki kuu ya China iliamua kupunguza kikomo cha chini cha riba ya mkopo wa benki. Mkazi anaponunua nyumba ya kwanza anaweza kupata nafuu ya 85% ya riba ya mkopo wa nyumba. Mtaalamu wa mambo ya fedha wa kituo cha utafiti wa maendeleo cha baraza la serikali Bw. Xia Bin alisema, hatua hiyo inaonesha kuwa wakazi wanaonunua nyumba kwa mikopo ya benki wanaweza kupata nafasi kubwa ya kupunguziwa kikomo cha chini cha riba ya mikopo kuliko zamani.

"Kwa ufupi ni kuwa, serikali inapofanya uamuzi inafikiria hali ya maisha ya watu, ilipunguza kikomo cha chini cha riba ya mikopo ili kupunguza athari kwa wakazi wanaonunua nyumba."

Benki za biashara zimechukua hatua kwa haraka kwa kufuata sera za benki kuu, wakati zilipoongeza riba ya mikopo ya nyumba ya vipindi mbalimbali, ziliamua kuwapa nafuu kubwa kabisa wakazi wanaonunua nyumba ya kwanza.

Ili kukabiliana na marekebisho ya riba ya mikopo, watu wa China wana maoni ya aina mbalimbali. Bw. Li Lei, ambaye anafanya kazi katika chombo cha habari alisema, ongezeko la gharama ya nyumba lililoletwa na kuongezeka kwa riba ya mikopo ya benki bado liko katika kiwango cha kuweza kulihimili. Alisema "Sioni kama kuna tofauti kubwa, kwani fedha za mkopo wa nyumba ninazotakiwa kulipwa kila mwezi si nyingi, hivyo shinikizo ninalokabiliwa nalo si kubwa. Kwa hiyo sioni athari kubwa kwangu kutokana na kuongezeka kwa riba."

Lakini Bw. Xu Yunting ambaye anafanya kazi katika kiwanda kimoja cha serikali alisema, atatafuta njia nyingine ya kurudisha mapema fedha za mkopo wa nyumba ili kupunguza ongezeko la shinikizo linalomkabili kutokana na kuongezeka kwa riba ya mikopo. Alisema "Bila shaka nimekuwa na wazo la kurudisha mapema fedha za mkopo, kwa vyovyote ninadaiwa fedha na benki, tena riba imeongezeka, hivyo ninataka kurudisha fedha zote za mkopo mapema kadiri inavyowezekana."

Hatua ya kuongeza riba ya benki kuu ya China pia inafuatiliwa na jumuiya ya kimataifa, maoni ya baadhi ya watu yanasema, China inaingia kipindi kipya ya kuongeza riba ya mikopo, katika siku za baadaye benki kuu ya China itatekeleza sera za kuongeza riba mara kwa mara na kwa kiwango kidogo, pamoja na kudhibiti uchumi kwa sera za sarafu. Kuhusu suala hilo Bw. Xia Bin alisema, kuongeza riba au la, na kuongeza riba kwa kiwango gani katika siku za mbele, kutaamuliwa na hali ya uchumi wa taifa.

Idhaa ya Kiswahili 2006-08-29