Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-29 20:18:05    
Israel yachunguza makosa ya maofisa wa ngazi ya juu wa serikali na jeshi kuhusu mapambano kati ya Israel na Lebanon

cri

Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert tarehe 28 usiku alitangaza kuwa, serikali imeamua kuunda tume mbili kufanya uchunguzi kuona kama hatua walizochukua maofisa wa ngazi ya juu wa serikali na jeshi kuhusu mapambano kati ya Lebanon na Israel ni sahihi au la. Hii ni hatua iliyochukuliwa na Bw. Ehud Olmert kutokana na lawama kutoka kwa watu kushuku usahihi wa sera na uongozi wa maofisa hao kuhusu mapambano kati ya Lebanon na Israel, lengo lake ni kupunguza shinikizo kubwa la nchini na kuimarisha utawala wake. Lakini kwa sasa ni vigumu kutabiri kama anaweza kutimiza lengo lake hilo au la.

Bw. Ehud Olmert alitangaza huko Haifa, mji ulioko kaskazini mwa Israel kuwa serikali imeamua kuunda tume mbili za uchunguzi, ambazo moja itaongozwa na Nahum Admoni, ambaye alikuwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi ya Israel, Mossad, na kufanya uchunguzi kuhusu mipango iliyotungwa na serikali ya Israel kuhusu mapambano kati ya Lebanon na Israel. Tume ya pili itafanya uchunguzi kuhusu vitendo vya jeshi la nchi hiyo.

Habari zinasema wajumbe wa tume hizo mbili waliteuliwa na serikali, na hawakukabidhiwa madaraka ya kuwahoji mashahidi, wala kuwa na nguvu ya kuwaachisha kazi maofisa husika waliofanya makosa, uchunguzi utakaofanyika ni wa ndani ya serikali ya nchi hiyo. Hatua hiyo iliyochukuliwa bado iko mbali na matakwa ya watu wanaomkosoa Bw Olmert. Tarehe 28 mwezi huu Bw. Olmert alikataa madai ya wakosoaji akisema, hivi sasa kwa ndani serikali ya Israel inataka kujenga upya sehemu ya kaskazini iliyoharibiwa kutokana na mashambulizi ya chama cha Hezbollah, na kwa nje inataka kukabiliana na maadui ikiwemo Iran, hivyo haiwezi kupoteza wakati mwingi kwa ajili ya mambo yaliyopita.

Mapambano kati ya Lebanon na Israel yaliyodumu kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja, yalisimamishwa tarehe 14 mwezi huu. Watu wa Israel wanaona kuwa katika mapambano hayo, viongozi wa serikali na jeshi la Israel walifanya makosa ya kisera na uongozi, na kufanya jeshi la Israel kushindwa kutimiza malengo kadhaa yaliyowekwa katika operesheni za kijeshi. Kura za maoni ya umma zilizopigwa hivi karibuni zinaonesha kuwa, 63% ya watu wanataka Olmert aondoke madarakani. Katika wiki mbili zilizopita waisrael pamoja na askari wa akiba mia kadhaa wa nchi hiyo walifanya maandamano kwenye bustani moja karibu na jengo la bunge wakitaka serikali kufanya uchunguzi kuhusu hali halisi ya mapambano na kutaka Olmert ajiuzulu.

Ingawa Olmert alilazimika kuamua ufanyike uchunguzi wenye kikomo baadhi ya wachambuzi wamesema, huenda kitendo hicho cha Olmert kitawakasirisha wapinzani wake, kwani wanasema Bw Olmert na maofisa wengine wa serikali wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi, na wala siyo kuwafanyia uchunguzi wasimamizi na watekelezaji. Gazeti la Haaretz nchini Israel lilichapisha maoni ya mhariri yakisema, tume zilizoundwa na Olmert hazitaweza kufanya kazi zenye maana, na haziaminiwi na watu, kinyume chake ni kwamba hatua hiyo itaharibu zaidi sura ya serikali ya Bw Olmert.

Shinikizo kubwa la nchini limefunika kivuli kwa mustakabali wa utawala wa serikali ya Bw Olmert. Kuna wachambuzi waliosema kuwa maandamano ya kutoa malalamiko yanayofanyika hivi sasa nchini Israel huenda yatakuwa makubwa zaidi na kuleta mgogoro wa kiutawala na kuuangusha utawala wa serikali ya Bw Olmert. Lakini pia kuna wachambuzi wanaosema kuwa, maandamano yanayofanyika hivi sasa ni madogo na maoni ya watu wanaompinga Olmert siyo ya namna moja, hivyo hawatakuwa na nguvu kubwa. Mbali na hayo tukitupia macho utawala wa Israel, tunaweza kuona kuwa vyama mbalimbali vya kisiasa havijaungana, na hivi sasa hakuna mtu mwingine anayeweza kuchukua nafasi ya Bw Olmert. Kwa hiyo kwa sasa watu bado hawawezi kupuuza uwezo wa kisiasa wa Bw Olmert.