Hivi karibuni China na Marekani ziliafikiana kuhusu namna ya kuhimiza mazungumzo ya biashara ya pande nyingi duniani, zikieleza kuwa zitahimiza urejeshaji wa raundi ya Doha ya mazungumzo ya Shirika la Biashara Duniani, WTO, ingawa bado kuna tofauti kubwa kati ya pande hizo mbili.
Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai alipokuwa na mazungumzo na mwakilishi wa biashara wa Marekani Bibi Susan Schwab, ambaye yuko ziarani nchini China alisema, China inapenda kuhimiza urejeshaji wa raundi ya Doha ya mazungumzo ya WTO. Lakini alisema raundi ya Doha ni raundi ya maendeleo, suala kuhusu maendeleo linatakiwa kupewa kipaumbele katika mazungumzo ili kukwamua mazungumzo hayo na kuhimiza ujenzi wa utaratibu wa biashara ya pande nyingi wenye ulingano, utulivu na ufunguaji mlango.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 29 hapa Beijing, Bibi Susan Schwab aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Marekani inatumai nchi kubwa za biashara duniani zitaunda umoja mpya, hususan kutarajia kuhimiza mazungumzo ya raundi ya Doha.
"Natarajia China itafahamu vizuri manufaa yanayoletwa na mafanikio ya mazungumzo ya Doha, vilevile itafahamu kuwa kufanikisha mazungumzo ya Doha na kujitahidi katika mchakato huo kunaendana na maslahi ya muda mrefu ya China."
Lakini msemaji wa wizara ya biashara ya China Bw. Chong Quan alitoa maoni tofauti kuhusu kauli hiyo ya Bibi Schwab akisema, kurejesha raundi ya Doha ya mazungumzo ya WTO na kujenga utaratibu wa biashara ya pande nyingi wa haki na usawa, kunaendana na maslahi ya nchi nyingi wanachama wa WTO. China inapenda kushirikiana na pande mbalimbali kushiriki kwa juhudi kwenye mazungumzo na kuhimiza kurejesha mchakato wa mazungumzo ya Doha, lakini anaona nchi wanachama zilizoendelea zinatakiwa kufanya kazi kubwa zaidi.
"Raundi ya Doha ni kuhusu maendeleo, hivyo ingewekwa katika nafasi ya kwanza ya mazungumzo. Natarajia nchi wanachama zilizoendelea kutoa mchango halisi ili kurejesha mazungumzo haraka iwezekanavyo na kuhitimisha lengo la mazungumzo katika tarehe iliyowekwa."
Mwezi mmoja uliopita mazungumzo ya raundi ya Doha, ambayo yanachukuliwa kuwa ni kuhimiza maendeleo na yaliyofanyika kwa muda wa miaka karibu mitano, yalisitishwa kutokana na kutoweza kuafikiana kati ya nchi wanachama kuhusu suala la kilimo, ambapo nchi wanachama zilizoendelea ikiwemo Marekani hazitaki kusitisha utoaji ruzuku kubwa kwa mazao ya kilimo kwa nchi yake, pamoja na tofauti ya misimamo ya nchi wanachama kuhusu masuala mengine, mazungumzo ya raundi ya Doha yalisitishwa bila kikomo cha muda.
Kuhusu msimamo wa China kuhusu kurejesha mazungumzo ya raundi ya Doha Bibi Schwab alisema, Marekani inakubali kufanya juhudi kuzindua upya mazungumzo ya raundi ya Doha. Lakini alisisitiza wakati wa kufuatilia maendeleo, mazungumzo pia yatakiwa kujadili suala la kupunguza kikomo cha uidhinishaji wa maombi ya kuingia sokoni, yaani suala la kufungua masoko lijadiliwe pia, ikiwemo kufungua masoko kwa mazao ya kilimo ya nchi za nje. Kuhusu umuhimu wa China Bibi huyo alisema, China ni nchi iliyonufaika zaidi kutokana na utaratibu wa biashara ya pande nyingi, na anatumai kuwa China itafanya kazi kubwa zaidi katika mazungumzo ya raundi ya Doha.
Kuhusu kauli hiyo mtafiti wa wizara ya biashara ya China Bw. Mei Xinyu alisema, kuhimiza kurejesha mazungumzo ya duru la Doha, kweli kunanufaisha pande mbili za China na Marekani, lakini aliukumbusha upande wa Marekani kufahamu kuwa chanzo cha kusitishwa bila kikomo kwa mazungumzo ya Doha ni nchi wanachama zilizoendelea kutojali matakwa ya nchi wanachama zinazoendelea kuhusu maendeleo na kutaka kuondoa msingi wa lengo la maendeleo la nchi wanachama zinazoendelea. Alisema ili kunufaisha washiriki wa pande mbalimbali wa mazungumzo, nchi wanachama zilizoendelea zinapaswa kuzingatia nafasi ya manufaa katika biashara ya kimataifa, ule mpango wa ugawaji wa manufaa usio wa mwafaka unatakiwa kubadilishwa.
Mtaalamu huyo alisema ingawa kuna tofauti kati China na Marekani kuhusu mazungumzo ya biashara ya pande mbili na pande nyingi, lakini nchi hizo mbili zinatakiwa kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo.
|