Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-30 20:15:11    
Madakari na wauguzi wa Kenya wakabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi

cri

Leo basi kwenye makala yetu maalum kuhusu elimu, tumepata bahati ya kumtembelea Daktari Abdalah ambaye anafanya kazi katika hospitali ya Agha Khan iliyopo jijini Nairobi nchini Kenya, ambaye atatueleza jinsi yeye na madaktari wenzake wanavyokabiliana na virusi vya Ukimwi.

Karibu Dr.Abdalah

Dk: Khasante sana

U: Kumekuwa na makongamo mengi kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, na hili lililofanyika juzi nchini Canada lilikuwa ni kongamano la 16 la kimataifa kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, unadhani makongamano kama hayo yana umuhimu gani?? Na yanasaidia vipi katika vita dhidi ya Ukimwi kote ulimwenguni hasa barani Afrika??

Dr: Ni kweli kama ulivyosema kuna makongamano mbalimbali, kuna makongamano ya kitaifa na kuna ya kimataifa kama lile lililofanyika juzi nchini Canada ambalo ni lilikuwa ni la 16. Katika makongamano hayo watu kutoka vikundi mbalimbali hukutana na kujadili kwa kina mada zinazohusu ugonjwa wa Ukimwi. Wanasayansi wao hulinganisha utaratibu na tafiti mbalimbali ambazo zilikuwa zikiendelea kufanyika kwa muda wa miaka mitatu, ili kujua hatua na mafanikio yaliyofikiwa, kwa mfano mabadiliko ya virusi vya Ukimwi, dawa mpya na chanjo zilizopatikana.

Pia mawaziri kutoka nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa na Ukimwi kama nchi za Afrika na mawaziri kutoka nchi zilizoendelea ambapo wanataka kusaidiana, hivyo hukutana na kujadiliana na kupanga mikakati ya namna ya kusaidiana.

Waathirika nao pia huja na kujadiliana mambo mbalimbali, kwa mfano namna wanavyopata dawa na wengine hueleza unyenyepa wanaokutana nao katika maisha ya kila siku. Kwa hiyo katika makongamano kuna mada mbalimbali zinazojadiliwa ambazo zina faida kubwa ndani yake.

U: Hivi karibuni wakati kongamano lile la kimataifa likiendelea vyombo mbalimbali vya habari viliripoti kuwa waganga wa jadi ambao na wao pia hufanya utafiti dhidi ya tiba ya ugonjwa wa Ukimwi, wamesema kuwa utoaji bure wa dawa za kurefusha maisha ya wagonjwa wa Ukimwi kwa kiasi fulani kunaua biashara yao, wewe unalionaje suala hili?

Dr: Kwa hakika madai hayo siyo ya kweli, kwa sababu mzigo wa Ukimwi ni mzito sana, na hakuna kikundi chochote kinachoweza kuyamaliza matatizo ya ugonjwa huu peke yake. Kwa hiyo hata waganga wa kienyeji wakipewa jukumu hili hawataliweza, kwa hiyo kila mtu ana nafasi ya kufanya juhudi zake, hili ni jambo la kwanza.

Jambo la pili hizi dawa zinatibu magonjwa mbalimbali, lakini zile dawa za kienyeji hazitibu magonjwa yanayotibiwa kwa dawa za Arvs, utakuta kwa mfano dawa za kienyeji zinapunguza kasi ya mgonjwa kama ya kuharisha, homa, kukohoa au magonjwa ya ngozi. Na hizi ARV kazi yake ni kuua vile virusi vyenyewe, hakuna dawa ya kienyeji hata moja inayoweza kuua virus vyenyewe, na hatujapata ushahidi wa kuthibitisha, kwa hiyo jambo la msingi ni ushirikiano kati ya makundi haya mawili na kufanya kazi pamoja. Dawa za kienyeji zimekuwepo kwa zaidi ya miaka 20 sasa kabla hata ya dawa za ARV kugunduliwa, kwa nini kasi ya Ukimwi imezidi kuongezeka?? Kama waganga wa kienyeji walikuwa wanaweza kuumaliza ugonjwa kwa nini sasa hawajaumaliza?? Kwa hiyo waganga wa kienyeji wasiwalalamikie wenzao waliogundua mambo mbalimbali bali washirikiane nao na kufanya kazi pamoja.

U: Katika kongamano lililofanyika nchini Canada ilibainika kwamba matatizo mengi yanayoikumba vita dhidi ya Ukimwi barani Afrika ni kutokuwa na miundo mbinu ya kuukabili Ukimwi pamoja na uhaba wa wauguzi, ambapo katika baadhi ya sehemu unakuta mwuguzi mmoja anahudumia wagonjwa elfu kumi au daktari mmoja anahudumia wagonjwa elfu hamsini, unafikiri ni kwa vipi tatizo hili linaweza kutatuliwa?

Dr: Kuna mambo mawili, kwanza ni kweli hatujawa na uwezo wa kuwapatia watu wetu huduma nzuri zinazotakiwa, kwa mfano tukiongelea upande wa miundo mbinu hakuna hospitali za kutosha, hakuna vipimo za kutosha, hakuna dawa za kutosha, hakuna wauguzi na madaktari wa kutosha, lakini jambo moja nataka tutofautishe ni kuwa, tunaposema mwuguzi mmoja anahudumia wagonjwa elfu kumi sio kwa ugonjwa wa aina moja peke yake, ni katika mji au kijiji Fulani utakuta wako watu elfu kumi na katika kituo cha afya kuna wauguzi wawili, hii haina maana kwamba watu elfu kumi wanaugua ugonjwa wa Ukimwi, ni magonjwa yote kwa ujumla.

Tunachukua idadi ya watu kwa mfano hapa Kenya tunasema tuna wauguzi elfu thelathini ambao wamepata mafunzo katika vyuo mbalimbali, halafu tunachukua idadi ya watu wa Kenya, kwa mfano wakenya wapo milioni thelathini, sasa unagawanya jumla ya idadi ya watu wa Kenya na jumla ya wauguzi, kwa hiyo unaweza kusema mwuuguzi mmoja anahudumia watu 10.

Lakini cha muhimu ni kujua watu wangapi wanaugua Ukimwi, kwa mfano hapa Kenya wagonjwa wa Ukimwi wapo laki mbili tu, kwa hiyo hatutarajii kwamba watahitaji wauguzi wengi zaidi. Jambo la pili ni wale ambao hawajapata ugonjwa wa Ukimwi, unajua kuna tofauti katika ya kupata ugonjwa wa Ukimwi na kuwa na virusi vya Ukimwi, wenye virusi ni wengi zaidi lakini wana afya zao na hawahitaji kuhudumiwa, lakini kuna wale ambao wako mahututi sasa, ambao tunasema wako laki mbili. Na wengi kati yao wanahudumiwa na familia zao. Lakini kwa Kenya tuna bahati kwani tuna hospitali za kutosha na wauguzi wa kutosha, lakini nchi kama Namibia bado kuna shida, kwa sababu bado wana upungufu mkubwa wa wauguzi, na serikali yao imeomba wauguzi mia nne kutoka Kenya.

U: kwa kumalizia una ushauri gani kwa wagonjwa wa Ukimwi wanaokusikiliza hivi sasa, au ndugu wa wagonjwa na watu wengine ambao hawajaathirika ??

Dr: ushauri wangu mkubwa ni kuwa , tunapaswa kufikiria kwa makini na kuchukua hatua za kujikinga kabla hatujaathirika, hili ndio jambo la msingi kabisa. Ugonjwa unazidi kuenea kwa sababu watu wengi hawazingatii mafunzo wanayopata, hasa vijana ambao ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa huu. Hivyo ni muhimu kwa watu wote hasa vijana kutojitumbukiza katika masuala ya kujamiiana kabla ya ndoa, ili kuepuka hatari ya kupoteza maisha mapema