Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-31 19:27:11    
Bw. Kofi Annan hakupata mafanikio makubwa katika ziara yake nchini Lebanon na Israel

cri

Hivi karibuni katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alifanya ziara nchini Lebanon na Israel akitaka kuhimiza Hezbollah na Israel kuafikiana kwenye usimamishaji mapigano wa kudumu. Lakini kutokana na matatizo yenye utata mwingi kati ya Lebanon na Israel, hivyo Bw. Annan alikutana na shida kubwa katika shughuli za usuluhishi na hakupata mafanikio makubwa katika ziara yake kwenye nchi hizo mbili.

Mgogoro uliozuka hivi karibuni kati ya Lebanon na Israel ulisababishwa na askari wa Hezbollah, ambao walivuka mpaka kushambulia kituo cha jeshi la Israel na kuwateka nyara askari wawili wa jeshi la Israel, kisha Israel ikatumia kisingizio cha kutaka kuwaokoa askari wawili waliotekwa nyara, ilifanya mashambulizi ya kijeshi kwa siku zaidi ya 30, lakini haikufanikiwa kuwaokoa askari wake wawili waliotekwa. Hivyo suala la mateka limekuwa tatizo linalokwamisha uhusiano kati ya Lebanon na Israel. Baada ya Bw. Annan kuwasili nchini Israel tarehe 29 mwezi huu, kwanza kabisa aliwaona jamaa wa askari wa Israel waliotekwa nyara, ambapo alisema chama cha Hezbollah ni sharti kiwaache huru askari wa Israel. Lakini mara tu baada ya Bw. Annan kuondoka Israel, waziri wa maji na umeme wa Lebanon Bw. Mohammed Fneish, aliye mwanachama wa Hezbollah, alisema Hezbollah haitawaachia huru askari wa Israel waliotekwa nyara, ila tu kwa kubadilishana na askari wa Lebanon waliotekwa nyara vitani. Alisema lengo la Hezbollah la kuwateka nyara askari wawili wa jeshi la Israel ni wazi kabisa, ni kuona mateka wa kivita wa Lebanon wanaachiwa huru kwa njia ya mazungumzo.

Kuihimiza Israel kuacha kuizingira Lebanon ni moja ya majukumu muhimu aliyokuwa nayo Bw. Annan katika ziara yake hiyo. Bw. Annan alipofanya ziara nchini Lebanon aliwaambia viongozi wa nchi hiyo, ni aibu kwa Israel kuendelea kuizingira kijeshi Lebanon baada ya mapigano kusimamishwa. Lakini viongozi wa Israel hawakuonesha juhudi kuitikia wito wa Bw. Annan. Baada ya mazungumzo na Bw. Annan, waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert alisema Israel haitaacha kuizingira Lebanon kwenye bahari na anga, hadi azimio No. 1701 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litakapotekelezwa. Israel inasema sababu ya Israel kuendelea kuizingira Lebanon ni kuizuia Hezbollah isipate silaha mpya kutoka nchi za nje. Hivyo Israel imesema jeshi la Umoja wa Mataifa linalowekwa nchini Lebanon, halitakiwi kupangwa sehemu ya kusini mwa Lebanon tu, bali pia linatakiwa kupangwa kwenye sehemu ya mpakani kati ya Lebanon na Syria ili kuzuia njia ya kusafirisha silaha kwa Hezbollah. Kitendo hicho cha Israel ni kama kutoa shinikizo kwa Bw. Annan. Kwani hakuna mgogoro kati ya Lebanon na Syria, hivyo haina sababu ya kupanga askari wa jeshi la Umoja wa Mataifa kwenye sehemu ya mpakani kati ya nchi hizo mbili, nchi hizo pia hazitakubali kufanya hivyo.

Licha ya hayo Bw. Annan anatumai kuwa Israel kuondoka kutoka sehemu ya kusini mwa Lebanon hivi karibuni, lakini waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Amir Peretz alisema, ni baada ya idadi ya mwafaka ya askari wa jeshi la Umoja wa Mataifa kupangwa kwenye sehemu hiyo tu, ndipo jeshi la Israel litakapoondoka, lakini Bw. Peretz hakueleza wazi kuhusu "idadi ya mwafaka" aliyosema ni askari wangapi.

Bw. Annan katika ziara yake hiyo alitoa wito kwa pande husika na kuzitaka ziwe na ushirikiano kwa juhudi ili kuleta amani ya kudumu kati ya Lebanon na Israel. Lakini katika mazingira ya kuweko kwa mapambano kati ya nchi za kiarabu na Israel ni vigumu kuleta amani kati ya Lebanon na Israel.

Azimio No. 1701 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Lebanon na Israel ingawa limehimiza usimamishaji wa mapigano kati ya Lebanon na Israel, lakini bado kuna matatizo mengi, na masuala mengi ya kimsingi bado hayajatatuliwa. Katika ziara hiyo Bw. Annan hakuonesha upole wake kama alivyokuwa siku za nyuma, hakusema maneno ya kidiplomasia bali alisema maneno makali. Alisema azimio la baraza la usalama ina yaliyomo yasiyobadilika, wala siyo mahala pa kujichukulia kitu, ambapo mtu anaweza kuchagua chakula anachopenda. Aliongeza kusema pande zote husika lazima zioneshe udhati wake, kutekeleza kikamilifu azimio hilo, la sivyo, hatari ya kurudi kwa mapigano ni kubwa sana. Lakini je "pande zote husika" alizozitaja zitasikiliza maneno yake? Kwani kila upande unaweka maslahi yake katika nafasi muhimu.