Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-31 20:07:31    
Wasichana wa milimani wanaopenda kuimba nyimbo

cri

Mwezi Juni mwaka huu, kutokana na mwaliko wa Radio China Kimataifa watoto 10 kutoka sehemu ya milimani wanakoishi watu maskini mkoani Guizhou, kusini magharibi mwa China walitembelea ofisi za Radio China Kimataifa. Hivi karibuni waandishi wetu wa habari walikwenda kutembelea maskani ya watoto hao.

Mliosikia ni wimbo wa kabila la Wamiao ulioimbwa na kina dada wawili. Dada mkubwa anaitwa Luo Huaxiang, ana umri wa miaka 15, na mwingine anaitwa Luo Xiaoxiao, ambaye ni mdogo kwa mwaka mmoja kuliko dada yake mkubwa. Watoto hao wa Kabila la Wamiao wanaishi wilayani Panxian, sehemu ya milimani mkoani Guizhou ambayo iko mbali na miji. Inawachukua saa moja au mbili kwenda shuleni, na chakula chao kwa kawaida ni viazi na mahindi. Familia yao yenye watu 6 inategemea mazao ya kilimo yanayolimwa kwenye shamba lenye ukubwa unaolingana na kiwanja cha kuchezea mpira wa kikapu. Baadhi ya wakati wazazi wao wanatafuta dawa za mitishamba milimani, ambazo wanauza na kupata hela.

Nyumba yao ya mbao iko kando ya mlima. Mbele ya mlango, imepandwa migomba na mahindi. Nyumbani sakafu si nzuri na mwangaza unaingia ndani kwa kupitia nyufa mbalimbali zilizopo kwenye paa la nyumba. Kuna mtambo wa kufuma vitambaa na samani kadhaa za hali duni, ambapo nyaraka zaidi ya 10 za tuzo zilizotundikwa ukutani zinaonesha furaha ya maisha kwenye familia hiyo maskini. Dada wawili walipata tuzo hizo kwenye mashindano mbalimbali ya kuimba. Uwezo wao wameurithi kutoka kwa mama Tao Chunyan, ambaye aliwahi kupata ubingwa kwenye shindano la kuimba la wilaya hiyo.

Mama huyo alikuwa akifuma vitambaa huku akiimba wimbo wa kale wa kabila la Wamiao.

Familia hiyo ni ya watu wa kabila la Wamiao wanaoishi katika sehemu ya kusini magharibi mwa China. Bibi Tao Chunyan alianza kujifunza kufuma vitambaa na kutarizi alipokuwa na umri wa miaka 10, lakini hakuwafundisha mabinti zake ufundi huo. Mama huyo mkulima mwenye elimu ya msingi tu anashikilia kuwa kupata elimu ni njia nzuri kuliko nyingine kwa watoto wake. Lakini si rahisi kwa familia hiyo maskini kuwasomesha watoto wanne. Mama Tao Chunyan alisema:

 "Hatuna fedha za kutosha, hatuna uwezo wa kuwalisha na kuwasomesha watoto wetu kwa wakati mmoja."

Mabinti wawili wa mama huyo walikuwa hodari katika masomo. Lakini iliwabidi waache masomo kutokana na kushindwa kulipa ada za shule. Katika muda huo walikuwa wanafanya shughuli za kilimo na kuanika mitishamba. Dada mkubwa Huaxiang akikumbusha siku hizo alishindwa kujizuia na kulia,

"Nilikuwa nina hamu ya kusoma. Kila siku niliwaangalia watoto wengine wakienda shuleni kwa furaha, niliona wivu. Lakini nilikuwa nafahamu kuwa wazazi wangu hawana uwezo, kwa hiyo sikutaja jambo hilo kwa wazazi wangu."

Mwaka 2000 maisha ya dada hao wawili yalibadilika. Walisamehewa nusu ya ada za shule na serikali, wakarudi shuleni. Hata hivyo kila mtoto alipaswa kulipa karo ya Yuan 40, sawa na dola za kimarekani 5 kwa mwaka, huu ulikuwa ni mzingo mkubwa kwa familia hiyo. Kwa hiyo mwaka mmoja baadaye watoto hao wawili walikuwa wanakabiliwa na uwezekano wa kuacha masomo kwa mara nyingine tena. Wakati huo huo mwalimu wao Bw. Zhang Youfu alijitokea kuwasaidia. Dada mkubwa Huaxiang alisema 

 "Wazazi wangu walishindwa kulipa karo, mwalimu alitoa Yuan 40 kunisaidia kulipa karo. Sijui namna ya kumshukuru kwa maneno. Naweza tu kumwambia asante, na nitafanya kila niwezalo kusoma kwa bidii."

Baada ya hapo dada mkubwa Huaxiang alipata maendeleo zaidi katika masomo. Alisema anavutiwa na somo la hisabati kwa vile mwalimu Zhang Youfu aliyemsaidia anamfundisha somo hilo.

Tokea mwaka 2005 serikali iliongeza kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za elimu, kwa hiyo watoto wa huko wanaweza kupata elimu bure kutoka shule za kimsingi hadi shule za sekondari ya chini, zaidi ya hayo wanafunzi kutoka familia maskini wanapewa misaada.

Jambo lingine linalofurahisha familia hiyo ni kuwa, mwaka huu dada mdogo Xiaoxiao na wanafunzi wenzake zaidi ya 80 kutoka familia maskini walipata msaada kutoka kwa wafanyakazi wa Radio China Kimataifa. Msaada huo ni Yuan 360, sawa na dola za kimarekani 45 kwa kila mtoto kwa mwaka. Fedha hizo ni nyingi kwa familia hiyo ambayo pato lake kwa mwaka halizidi Yuan elfu moja. Mama Tao Chunyan alitengeneza kwa mikono mkoba wenye mtindo wa kabila la Wamiao kama zawadi kwa mfadhili wa Radio China Kimataifa.

Mwezi Juni mwaka huu Xiaoxiao ambaye hakuwahi kwenda mjini akiambatana na wanafunzi wenzake 9, walikuja Beijing kutokana na mwaliko wa Radio China Kimataifa. Ziara hiyo ya siku 5 si ndefu, lakini imeweka kumbukumbu nzuri kwa mtoto huyo. Baada ya kurudi nyumbani, anawasimulia mara kwa mara wenzake mambo alivyoshuhudia katika mji mkuu Beijing.

"Katika jumba la makumbusho la sayansi na teknolojia, kuna roboti ambaye anaweza kujibu maswali. Nilimwuliza je, unajua kuogelea? Alijibu sijui, mwilini mwangu zimejaa nyaya za umeme, siwezi kuingia majini, la sivyo nitakufa. Ukuta mkuu unapendeza, watu wazima wa Beijing waliona ni vigumu kupanda, lakini naona ni rahisi sana kwani nimezoea kupanda milima hapa nyumbani."

Wasichana wa kabila la Wamiao walizaliwa wakijua kuimba nyimbo. Dada hao wawili wanapenda kuimba nyimbo. Uimbaji nyimbo ni sehemu ya maisha yao, na maisha yenye nyimbo ni maisha yenye matumaini.