Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-31 20:16:52    
Mwanamke anayeongoza kijiji chake kupata maendeleo

cri

Kijiji cha Jinghua kipo wilayani Xinxiang, mkoani Henan, katikati ya China. Hivi sasa kijiji hicho kinajulikana kutokana na maendeleo yake. Wanakijiji wenyewe walisema hapo awali kijiji hicho kilikuwa maskini, baada ya Bibi Liu Zhihua kuchaguliwa kuwa mkuu wa kijiji hicho, juhudi za kuondokana na umaskini zikaanza kuzaa matunda.

Liu Zhihua anaonekana ni mkulima mwanamke wa kawaida wa China. Miaka 34 iliyopita alichaguliwa kuwa mkuu wa kijiji cha Jinghua bila kutarajia. Kabla ya hapo wanaume wa kijiji hicho walikuwa wameshika zamu ya ukuu wa kijiji, lakini wote hawakuweza kutimiza lengo la kuhakikisha wanakijiji wanajitosheleza kwa chakula. Kutokana na hali hiyo, wanakijiji waliamua kumchagua mwanamke aongoze kijiji hicho.

Bibi Liu Zhihua akawa mkuu wa kijiji cha Jinhua. Mwanzoni aliposhika wadhifa huo, jamaa zake walikuwa na wasiwasi naye. Lakini haikuchukua muda mrefu mkuu huyo mwanamke alipata imani kutoka kwa wanakijiji wenzake. Alipoingia madarakani hatua ya kwanza aliyochukua ililenga kuondoa tatizo la upungufu wa chakula. Aliwaongoza wanakijiji wenzake kulima mashamba yote yaliyoachwa na kupanda miche ya ngano. Kila siku asubuhi na mapema, Bibi Liu Zhihua alikuwa anatangulia kufika mashambani. Wanakijiji wenzake walipomwona mwanamke huyo anachapa kazi kwa bidii kwa manufaa ya wanakijiji wote, walikuwa wanahiari kuambatana naye kwenda kufanya kazi mashambani. Mwaka mmoja baadaye watu wa kijiji hicho walipata mavuno mazuri na kujitosheleza kwa chukula kwa mara ya kwanza.

Bibi Liu Zhihua alisema "Tatizo la upungufu wa chakula lilitatuliwa mwaka 1973, lakini bado tulikuwa tunakabiliwa na umaskini. Kwa hiyo tulianzisha shughuli ndogo za utengenezaji. Hadi ilipofika mwaka 1979 serikali ilizidi kupunguza udhibiti, tulianza kujishughulisha na sekta ya viwanda."

Toka mwaka 1974 wanakijiji walipoanzisha shughuli ndogo ndogo za utengenezaji, walianza kulimbikiza akiba ya fedha. Hapo baadaye kutokana na pendekezo la Bibi Liu Zhihua, kijiji hicho kilijenga kiwanda cha kuzalisha aina ya chakula kinachotengenezwa kwa maharagwe kiitwacho Fuzhu, kwani maharagwe hupatikana huko kwa urahisi. Bibi Liu Zhihua mwenyewe alileta bidhaa hizo mjini Beijing, ambapo alikwenda duka moja baada ya jingine na kukiuza. Hadi kufikia miaka ya 90 nusu ya chakula cha Fuzhu kilichouzwa kwenye soko la Beijing ilikuwa inatoka kwenye kijiji cha Jinghua.

Katika miaka iliyofuata Bibi Liu Zhihua alikuwa anawaongoza wanakijiji wenzake kuanzisha viwanda mbalimbali. Kutokana na jitihada zake hivi sasa kijiji cha Jinghua kimebadilika kuwa kundi la viwanda lenye mali zisizohamishika zenye thamani ya Yuan milioni 580, sawa na dola za kimarekani milioni 72.5.

Hivi sasa mkuu huyo wa kijiji Bibi Liu Zhihua anafikiria kuviendeleza viwanda vya kijiji hicho viwe viwanda visivyotoa uchafuzi kwa mazingira. Alisema 

 "Tunavitaka viwanda vyetu visichafue mazingira na vipunguze matumizi ya nishati na gharama za uzalishaji. Tunafuata kanuni moja, yaani hatufanyi biashara inayoleta uchafuzi wa mazingira."

Sura ya kijiji cha Jinghua imebadilika siku hadi siku. Wanakijiji wanasema hapo awali walikuwa wanaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa udongo na nyasi. Hivi sasa ukitembelea kijiji hicho, utakuta nyumba safi zinazopangwa vizuri kando ya barabara. Bibi Li Yu ni mmoja wa makada wa kijiji hicho, alisema:

"Mwaka 1993 ujenzi wa hoteli na bustani kwenye kijiji chetu ulikamilika. Nyumba ya mapumziko ilijengwa baadaye kwa ajili ya kuendeleza kazi ya utoaji wa maji ya chupa, pia kijijini hapo kuna shule na soko. Katika kipindi cha miaka mitatu, tulijenga shule tatu."

Mwanakijiji Bibi Du Xuefen alisema wanakijiji wanapewa bure mahitaji mengi ya nyumbani, kwa mfano nyumba zilijengwa na kijiji, samani zilinunuliwa na kijiji na huduma nyingine za maji, umeme na gesi pia zinapatikana bila ya malipo. Mwanakijiji huyo alimshukuru mkuu wa kijiji Bibi Liu Zhihua, alisema:

"Yeye amefanya kila awezalo kuwasaidia wanakijiji kuondokana na umaskini. Mbali na kuhakikisha tunapata chakula cha kutosha na nguo, pia amejitahidi kutuletea maendeleo. Awali tulikuwa tunakabiliwa na tatizo la chakula, hivi sasa maisha yetu yanaboreshwa mwaka hadi mwaka."

Bibi Du Xuefen aliongeza kuwa, kutokana na pendekezo la mkuu wa kijiji Bibi Liu Zhihua, tokea mwaka 1999 kijiji hicho kilijenga shule ya chekechea, shule ya msingi, na shule ya sekondari. Shule hizo zenye zana za hali ya juu na zinazotoa malipo mazuri na kuwavutia walimu hodari, hali ambayo imeinua sana sifa ya ufundishaji kwenye shule hizo.

Mtoto wa Bibi Lu Ruijuan anasoma kwenye shule ya msingi ya kijiji hicho. Alisema :

"Mkuu wetu ana upeo wa mbali. Alianzisha kazi ya ujenzi wa shule ya kijiji hata ilipokuwa shule haijaanzishwa wilayani kwetu, akiwa na lengo la kuwaandalia mazingira mazuri watoto wa vijijini na kuwafanya wapate elimu sawa na watoto wa mijini."

Hivi sasa watoto wa kijiji cha Jinghua wanasoma bure kutoka shule ya chekechea mpaka shule ya sekondari. Na watoto wanaoweza kufaulu mtihani na kuendelea na masomo ya vyuo vikuu wanapewa msaada wa masomo.

Katika miaka zaidi ya 30 iliyopita, kijiji kilichokuwa maskini kilibadilika kuwa kijiji chenye maendeleo. Hivi sasa mkuu wa kijiji hicho Bibi Liu Zhihua ana umri wa zaidi ya miaka 60. Lakini bado hajaridhika na mafanikio yaliyoptaikana, bali anachemsha bongo ili kuinua zaidi kiwango cha maisha ya wanakijiji. Alisema:

 "Wastani wa pato la wanakijiji bado si mkubwa, hivi sasa ni kati ya Yuan elfu 13 na 14 kwa mwaka. Sasa tuna mpango wa kuongeza pato la kila mtu kwa Yuan elfu 2 kwa mwaka."