Tarehe 31 Agosti Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio No. 1076 la kutuma jeshi a Umoja wa Mataifa kwenye sehemu ya Darfur mwishoni mwa mwezi Septemba, wakati ambapo jeshi la Umoja wa Afrika litakamilisha kipindi chake, ili kuhakikisha "makubaliano ya amani ya Darfur" yaliyosainiwa na serikali ya Sudan na kundi la upinzani mwezi Mei mwaka huu yanatekelezwa.
Kwa mujibu wa azimio hilo, kundi la wanajeshi la Umoja wa Mataifa lililoko sasa kwenye sehemu ya Darfur lenye wanajeshi elfu kumi litaongezewa hadi elfu 17 na mia tatu, na kwa msingi huo askari polisi elfu 3.3 pia watatumwa huko. Azimio hilo limeidhinisha haki ya jeshi la amani la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua yoyote ya kulinda usalama wake na raia dhidi ya tishio lolote la nguvu na kuhakikisha makubaliano yanatekelezwa.
Aidha azimio hilo pia linasema jeshi la amani la Umoja wa Mataifa halitatumwa mpaka likubaliwe na serikali ya Sudan.
China, Russia na Qatar hazikupigia kura azimio hilo. Baada ya kulipigia kura azimio hilo, balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Bw. Wang Guangya alieleza kuwa kwenye mchakato wote wa kutatua mgogoro wa Darfur China ilikuwa ikijitahidi kushauriana na pande husika na inaunga mkono sehemu nyingi zilizomo kwenye azimio hilo, lakini ina maoni yake kuhusu wakati wa kupitisha azimio hilo na maneno yaliyotumika katika azimio hilo, kwa hiyo China haikupiga kura.
Bw. Wang Guangya alisema, utatuzi wa mgogoro wa Darfur lazima uwe wa haraka na pia uzingatie utatanishi wake, lazima uwe na nia thabiti na pia uwe na subira na njia zinazofaa. Alisema katika wakati huu ambapo serikali ya Sudan inakataa katakata azimio hilo kupitishwa kwa pupa, na Umoja wa Mataifa unafaa kufanya majadiliano vya kutosha na serikali ya Sudan. Alisema, vitendo vya Umoja wa Mataifa vinaambatana na hali halisi na vitendo vya kutuma jeshi la Umoja wa Mataifa na lazima vikubaliwe na serikali ya Sudan. Hayo ni maoni ya pamoja ya Umoja wa Afrika na pia Baraza la Usalama.
Mwenyekiti wa Baraza la Usalama mwezi huu, balozi wa Ghana katika Umoja wa Mataifa Bw.Effah Apenteng baada ya kulipigiwa kura azimio hilo alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuwasiliana na serikali ya Sudan, alisema kupitishwa azimio hilo hakumaanishi kuwa mazungumzo na serikali ya Sudan yamefungwa, amezitaka nchi zote wanachana wa Umoja wa Afrika, nchi za Kiarabu pamoja jumuyia za Kiislamu zishiriki kwenye mazungumzo hayo. Inasemekana kwamba hivi karibuni Umoja wa Mataifa utafanya mkutano na kujadili mgogoro wa Darfur na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Darfur iko magharibi mwa Sudan, kuanzia mwezi Februali mwaka 2003, vikosi vya upinzani dhidi ya serikali ya Sudan yaani Jeshi la Ukombozi wa Sudan na jeshi la haki na usawa yalianza shughuli za kuipinga serikali na kusababisha vifo vya watu wengi na watu milioni kupoteza makazi yao. Mwezi Agosti mwaka huo, Umoja wa Afrika ulituma vikosi kwenye sehemu ya Darfur kusimamia utulivu huko. lakini katika miaka ya karibuni vikosi vya Umoja wa Afrika vimekumbwa na matatizo ya fedha na huduma za maisha, vikosi hivyo vyenye askari 7,000 vinashindwa kutekeleza majukumu kama vinavyopaswa, kwa hiyo Umoja wa Afrika unatumai Umoja wa Mataifa utatuma jeshi lake badala ya vikosi vya Umoja wa Afrika. Kutokana na ombi la Umoja wa Afrika, Baraza la Usalama lilipitisha azimio No. 1663 la kupokea majukumu ya vikosi vya Umoja wa Afrika huko Darfur, lakini serikali ya Sudan inakataa kabisa na inapendekeza askari elfu kumi wa serikali ya Sudan watumwe badala ya jeshi la Umoja wa Mataifa. Rais Bashir wa Sudan alionya kwamba kama jeshi la Umoja wa Mataifa likiingia kwenye sehemu ya Darfur hali itakuwa sawa na matokeo ya jeshi la Marekani kulishambulia Iraq.
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-01
|