Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-01 16:24:18    
"Mimi ni "Msichana wa Afrika mwenye asili ya China" 

cri

Mimi ni msichana niliyezaliwa katika kijiji cha Siyu, kwenye visiwa vya Lamu vya bahari ya Hindi nchini Kenya. Hadi leo bado nakumbuka vizuri kuwa, nilipokuwa mtoto mdogo, bibi yangu alikuwa akinisimulia hadithi kuhusu meli za China zilizozama karibu na kisiwa cha Pete, kwenye bahari ya Hindi kutokana na kukumbwa na dhoruba miaka 600 iliyopita. Mabaharia wa China walionusurika waliwasili kwenye kijiji cha Shanga, ambao walikaribishwa na kuanza kuishi huko, siku nenda siku rudi, baadhi ya mabaharia hao wa China walihamia kijiji cha Siyu kutafuta maisha. Bibi yangu aliniambia kwa kithabiti kuwa, sisi ni wajukuu wa mabaharia hao wa China. Hivi sasa familia nyingi za kijji chetu cha Siyu zina vitu vya kale vilivyobakizwa na mabaharia wa China. Nyumbani kwangu pia kuna chombo cha kale cha kauri ya China, chombo hicho kilimerithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine mpaka kufika mkononi mwa mama yangu.

Miaka tisa iliyopita kikundi cha kwanza cha waandishi wa habari wa China walifika kijijini kwetu kukusanya habari kuhusu hadithi ya mabaharia hao wa China, kuanzia hapo wachina walikuja kwetu mara kwa mara na wakatuambia kuwa, sisi huenda ni watoto wa kizazi cha ukoo wa mabaharia wa China. Mwaka jana kituo cha televisheni cha Nanjing kilipiga filamu ya kumbukumbu, nilihojiwa na baada ya kuoneshwa kwa filamu hiyo mimi nilianza kujulikana nchini China, nikaitwa "msichana wa China" aishiye barani Afrika.

Mwaka 2002 niliandika barua kwa ubalozi wa China nchini Kenya nikiomba kupewa nafasi ya kusoma nchini China ili kufahamu mambo mengi zaidi kuhusu historia ya China, na kujichangia urafiki kati ya Kenya na China. Nilirudishwa barua kwa haraka nikaambiwa kuwa, kama nikisoma kwa bidii, baada ya kumaliza masomo ya sekondari ya juu nitalipiwa gharama za kusoma nchini China. Mwezi Julai mwaka jana, China ilifanya shughuli za kuadhimisha miaka ya 600 ya safari ya Zheng He baharini, kwa mara ya kwanza nilialikwa kutembelea China na kushiriki kwenye shughuli hizo. Kwenye ukumbi wa mikutano wa Beijing niliwakuta viongozi wengi wa ngazi ya juu wa China. Nilipoulizwa matakwa yangu ya kwanza nikaomba kupewa fursa ya kusomea matibabu ya kichina nchini China.

Safari hii nilitembelea sehemu nyingi zinazohusiana na safari ya Zheng He baharini. Mbali na Beijing, mji mkuu wa China, pia nilitembelea mji wa Nanjing na Taicang. Nilipofika mjini Taicang, mkoani Jiangsu, niliambiwa kuwa msafara wa merikebu za Zheng He ulioelekea sehemu ya pwani ya mashariki ya bahari ya Hindi ndio ulianzia huko. Wakazi wa Taicang walinitambua kama mtoto wa kikazi cha ukoo wa baharia wa Zheng He, na kunikaribisha kwa ukarimu mkubwa, hivyo nilisikia kama nimefika nyumbani kwetu.

Jambo linalonifurahisha zaidi ni kwamba, kutokana na juhudi za ubalozi wa China nchini Kenya na Chuo Kikuu cha Matibabu ya Kichina cha Nanjing, kamati ya China inayoshughulikia mfuko wa wanafunzi wa nchi za nje ilinipa nafasi maalum ili kuniwezesha kusoma nchini China. Kwenye ufunguzi wa Chuo Kikuu, nilizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzangu. Siku ya kwanza nilipokuwa kwenye darasa la kujifunza Kichina nilifurahi sana. Na nikiwa na matatizo ya kimaisha na kimasomo, walimu na wanafunzi wa China wananisaidia kwa wakati na kwa ukarimu, hivyo naona furaha sana kusoma nchini China.

Viongozi wa Chuo Kikuu cha Matibabu cha Nanjing wameniwekea mazingira mazuri ya kuishi. Naishi katika chumba chenye choo, seti ya televisheni, kiyoyozi, simu na jiko. Bwalo la wanafunzi linatutayarishia kwa umaalum chakula cha kiislamu kwa hofu kwamba sisi waislamu hatutazoea vyakula vya kichina. Sasa naweza kuwasiliana na wachina kwa lugha ya Kichina taratibu. Matakwa yangu makubwa ni kurudi nchini Kenya baada ya kumaliza masomo yangu ili kuwahudumia wananchi wa Kenya kwa ustadi wangu wa tiba niliyojifunza nchini China, na kuwa mjumbe wa urafiki kati ya Kenya na China. Naona hii itakuwa maadhimisho mazuri zaidi kwa safari ya amani ya Bw. Zheng He barani Afrika.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-01