Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-05 16:34:39    
Barua 0903

cri

Bwana Kilulu Kulwa wa Sanduku la 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akianza kwa salamu kwa wahariri na watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Ni matumaini yake kuwa sote hatujambo na tu bukheri wa afya tukiendelea na kazi na juhudi kubwa za kuwahudumia wasikilizaji wetu popote pale ambapo Kiswahili kinafahamika na kueleweka.

Anasema anatusikiliza takribani kila siku katika matangazo ya Kiswahili na pia hutembelea tovuti yetu kila anapopata nafasi hiyo na kusoma na kuburudika na vipindi murua na vya kuchangamsha katika tovuti hiyo ya CRI Online. Pia anasema anapenda atumie fursa hii kutupongeza sana kwa ajili ya kuanzisha kituo cha FM huko Afrika mashariki ili kuwapa uhondo zaidi wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili. Jambo hilo lina maana kubwa na ni hatua kubwa iliyochukuliwa na Radio China kimataifa ili kujipanua zaidi na hivyo kuwaletea wasikilizaji vipindi vya kuvutia, taarifa za kweli na za uhakika kuhusu Jamhuri ya watu wa China na duniani kote, popote pale walipo humu duniani, anasema wao wanatushukuru sana.

Anasema anapenda pia kutujulisha kuwa ametuma majibu ya shindano la chemsha bongo la Mimi na Radio China kimataifa, atashukuru sana ikiwa tutamfahamisha mara baada ya kupokea barua hiyo yenye maswali na majibu ya shindano hilo, ambalo yeye amelifurahia sana kwa kuwa linawajengea uwezo mkubwa wa ufahamu kuhusu Radio China kimataifa na historia yake yenye changamoto na pia mafanikio makubwa kabisa hadi wakati huu inapoelekea katika kutimiza miaka 65 tangu Radio China Kimataifa ianzishwe.

Anasema hao wasikilizaji wetu wanafurahi kusikia mengi zaidi kuhusu maadhimisho hayo ya Radio China kimataifa, anaamini yatafana sana kutokana na Radio China kimataifa kuwashirikisha wasikilizaji wake. Anatutakia maandalizi mazuri na mafanikio makubwa wakati wa maadhimisho hayo ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa Radio China kimataifa.

Tunamshukuru sana Bwana Kilulu Kulwa ambaye ni rafiki yetu wa miaka mingi aliyewahi kuchaguliwa kuwa msikilizaji bora na kupata nafasi ya kuja China kutembelea mwaka 1997. Naye kweli ni mshabiki wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, kila mara anatuletea barua akieleza maoni na mapendekezo yake mazuri ya kutusaidia kuboresha vipindi vyetu. Ni matumaini yetu kuwa tutadumisha uhusiano na urafiki kati yetu daima.

Msikilizaji wetu Andrew Kichele wa sanduku la posta 11508 Mwanza Tanzania anasema katika barua yake kuwa, dhumuni la barua yake hii ni kutaka kutueleza kuwa vipindi vyetu ni vizuri kwani vijana wengi wanavifurahia, pia wazee huvifuatilia. Vipindi vya Radio China kimataifa husikika karibu nchi nzima ya Tanzania. Yeye huwa anawahimiza vijana wenzake kusikiliza vipindi vyetu, nia yake nyingine ni kutoa pongezi motomoto, alikuwa anaomba tumtumie maelezo ya historia ya Radio China kimataifa, pia anaomba picha za watangazaji na picha za hifadhi za taifa nchini China, ushauri wake ni kuwa matangazo ya FM yasikike kwenye eneo kubwa zaidi ili wasikilizaji wengi zaidi wapate usikivu mzuri zaidi wa matangazo ya Radio China kimataifa.

Msikilizaji wetu David J. Sitabuka Fwamba ambaye barua yake huhifadhiwa na Mutanda Ayoub wa P.O Box 172 Bungoma ametuletea shairi moja lisemalo: Hongera Radio China Kimataifa , shairi hilo linasema:

Kenya nzima imeenea, Radio China Kimataifa

Uzuri wenu unaridhisha, katika nyanja mbalimbali

Mizizi yenu imesambaa, kote nchini nzima

Hongera Radio China kwa huduma zenu nzuri.

Nang'oa nanga, uzuri wenu kuorodhesha

Sifa zenu nzuri, kuziandika peupe

Kuanzia maelezo ya habari, utamaduni hamkosi

Hongera Radio China kwa huduma zenu nzuri.

Matukio yote duniani, mwatujuza nchini mwetu

Katika umoja na ushirikiano, mwatuleta pamoja

Kiburidisho hakika, nacho mwatuandalia

Hongera Radio China kwa huduma zenu nzuri.

Mwatufunza na kutufahamisha, hatua za kimaendeleo

Katika safari nchini China, tunaelewa uchina

Mwatufunza kuzungumza, na kuelewa kichina

Hongera Radio China kwa huduma zenu nzuri.

shindano la chemsha bongo, tunapanua bongo zetu

Pia mnatuzawadia, kwa vipawa mashindanoni

Mwatutia ari, ya uandishi na usomaji

Hongera Radio China kwa huduma zenu nzuri.

Mwatupa nafasi sawa, masikini na matajiri

Mmejitolea kutuma barua, na bahasha bure kwetu

Ili tuendelee kuwasiliana, bila tatizo lolote

Hongera Radio China kwa huduma zenu nzuri.

Mwishoni nimefika, pongezi nyingi sana

Uzuri wenu uwazi, kwa kila mkenya

Juhudi zenu Radio China, tunazipongeza wakenya

Radio China kimataifa, wenu mtandao mzuri

Hongera Radio China, kwa huduma zenu nzuri.

Msikilizaji wetu Erick Chemonges Klabu ya salamu ya eneo la sabaot, sanduku la posta 295 Kitale Kenya, katika barua yake ameanza kwa salamu kwa wasikilizaji na watangazaji, pia anasema watafurahi sana na ni matumaini yao kuwa kadi zao za salamu walizotuma zitasomwa hivi karibuni. Anasema wao ni wageni kwa kutuma barua pamoja na kadi za salamu ambazo wamepewa na Bwana Ayub Mutanda ambaye aliwaelezea mengi kuhusu idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Anasema wanawasalimu Erick Chemonges wa Kitale, Protus Chemor wa kitale, Lenard Chemor wa Kitale, Brenda Chemonges wa Kitale, watafurahi sana iwapo salamu zao zitasikika kwenye idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa hivi karibuni

Msikilizaji wetu Naiti Mutanda wa sanduku la posta 2099 kwenye barua yake aliyotuandikia ameanza kwa salamu kwa wasikilizaji wenzake na watangazaji, na pia anatoa pongezi kwa kazi zinazofanyika kwenye idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Matumaini yake ni kwamba sisi sote ni wazima na tuna nguvu ya kuendelea kuchapa kazi siku baada ya siku.

Anasema yeye hanabudi kusema jambo hili, japokuwa amefahimishwa mara nyingi kuhusu idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Kila siku yeye humwuliza ndugu Mutanda Ayub kama ameshasikia taarifa ya habari au hapana? Kwa mara nyingine yeye huwa hana nafasi, lakini kutokana na kipindi cha salamu zenu cha idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, ameona ana kiu na hamu ya kusikiliza matangazo ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Anasema kweli kuna watu wanaojitolea, lakini Bw. Mutanda Ayub Shariff amewapa changamoto wasikilizaji wenzake, amejitolea kupita kiasi kushughulikia idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, kwa sasa nyumbani kwake kila mahali kuna nembo ya CRI, na kwenye duka mjini Bungoma wateja wote wakifika wanasikia matangazo ya Radio China kimataifa. Bwana Ayub hafanyi hivyo kutokana na kulipwa, yeye kwake huo ni moyo wa kujitolea. Yeye mwenyewe anasema alifunga ndoa na idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa na wala hataipa talaka hata inyeshe mvua ya mawe.

Na msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff S.L.P 172 Bungoma, Kenya anasema katika barua yake kuwa ana furaha kutuhakikishia kuwa iwapo mola atampa nguvu na uwezo zaidi, atajitahidi kuitangaza zaidi Radio China kimataifa kwa kila mtu, wazee, akina mama, vijana, wanafunzi, watoto na hata watoto wanaorandaranda mjini mpaka kila mtu aweze kuelimika na kupata marafiki wazuri wa Radio China Kimataifa kama yeye.

Anasema ana furaha isiyo na kifani, tarehe kumi na sita 16/6/2006 furaha ilitiririka moyoni na mwili mwake wakati alipopokea zawadi yake kutoka kwa shirika la posta na simu Bungoma Kenya. Anatushukuru kumpa zawadi ya radio ambayo hajawahi kuiona huko Bungoma, angependa kutufahamisha kuwa inafanya kazi vizuri sana bila vipingamizi. Hakufurahi pekee yake bali familia yake kwa jumla. Na sasa ana sababu ya kujivunia kwa nini amejitolea kuiunga Radio China kimataifa. Anasema kuwa ataendelea kuhakikisha kuwa uhusiano kati yake na Radio China Kimataifa unaendelea, na atajitahidi kuwafahamisha watu wengi zaidi kuhusu matangazo ya Radio China kimataifa!

Tunamshukuru kwa dhati sana msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff kwa juhudi zake kubwa za kuitangaza Radio China kimataifa, juhudi zake kweli zinatutia moyo sana, ambazo zimetusaidia kupata wasikilizaji wengi na kutuwezesha tuone kuwa hatukuchapa kazi bure, kwani wasikilizaji wetu wengi wanatusikiliza kila siku, na kutuhimiza tuendelee na juhudi zaidi ili kuboresha vipindi vyetu. Hapa tunawashukuru wasikilizaji wetu wote popote walipo kwa uungaji mkono wao kwa kazi za idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-05