Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-06 16:39:56    
China yasaidia nchi zinazoendelea kuwaandaa wapimaji wa usalama wa chakula

cri
Watu wanaoshughulikia upimaji wa usalama wa chakula kutoka nchi 23 zinazoendelea walirudi katika nchi zao hivi karibuni baada ya kupata mafunzo kwa mwezi mmoja hapa Beijing China. Walioshiriki kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Beijing kuanzia mwanzoni mwa mwezi Agosti walitoka katika nchi za Albania, Cuba, Ecuador, Myanmar, Vietnam, Nepal na Philippines. Wakati walipokuwa Beijing walishiriki kwenye "Semina ya kimataifa kuhusu teknolojia ya upimaji wa usalama wa chakula kwa nchi zinazoendelea" iliyoendeshwa na Wizara ya biashara ya China, na wataalamu wa China walitoa mafunzo kuwaelezea teknolojia na zana za China katika upimaji wa usalama wa chakula, pia waliwafahamisha mbinu za kisasa za Marekani na Umoja wa Ulaya katika upimaji na uthibitishaji wa vyakula vya jenetiki, na kutoa fursa kwao kufanya ukaguzi katika sehemu mbalimbali nchini China.

Sherehe ya kufunga mafunzo hayo ilifanyika tarehe 23, Agosti ambapo ofisa wa Wizara ya biashara ya China aliyeshiriki kwenye sherehe hiyo alisema semina hiyo imepata mafanikio. Ofisa aliyeshughulikia semina hiyo Bw. Chen Xuezhong aliwaambia watu walioshiriki kwenye semina hiyo kuwa, China inapenda sana kuwasiliana na nchi nyingine kuhusu uzoefu wake mzuri katika upimaji wa usalama wa chakula. Alisema:

"Natumai kwa dhati kuwa mafunzo haya yatasaidia maendeleo ya nchi mbalimbali katika shughuli za teknolojia ya upimaji wa usalama wa chakula, pia natumai kuwa semina hiyo itatoa fursa ya kufanya mawasiliano ya kimataifa katika nyanja hiyo, na kuhimiza teknolojia ya upimaji wa usalama wa chakula ya China kuenea katika nchi nyingi zaidi zinazoihitaji teknolojia hiyo."

Bw. Chen Xuezhong alisema katika miaka ya hivi karibuni, magonjwa mengi makubwa yameleta athari mbaya kwa maendeleo ya uchumi na jamii za nchi mbalimbali duniani, na nchi nyingi ikiwemo China zimeweka kwa makini kanuni na vipimo katika teknolojia ya usalama wa chakula.

Bw. Chen alieleza kuwa hivi sasa katika mfumo wa teknolojia ya upimaji wa usalama wa chakula wa China kuna mbinu 200 za kufanya upimaji katika maabara, ambapo China imetafiti na kupata dawa karibu aina mia moja zinazotumika katika kupima sifa ya chakula, pia imeanzisha mtandao wa usimamizi na utaratibu wa utoaji onyo kwa usalama wa chakula, na kwa vyakula vinavyouza nje na kuagizwa kutoka nje.

Bw. Chen alisema hivi sasa China inafanya juhudi kuboresha utaratibu wa upimaji wa usalama wa chakula, na pia inapenda kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea kwa kuwapa mafunzo wapimaji wa usalama wa chakula, na kuwasiliana nao kuhusu uzoefu mzuri wa China. Bw. Chen alisema watu wengi walioshiriki kwenye semina hiyo walieleza matumaini yao ya kufanya ushirikiano katika nyanja hiyo, na Benin, Vietnam na Burundi pia zilisaini waraka wa kufanya ushirikiano na China.

Bw. Sakiusa Biaukula kutoka Wizara ya kilimo ya Fiji alitoa shukurani kwa China kuandaa semina hiyo akisema:

"Ikiwa ni nchi inayoendelea, Fiji iko nyuma zaidi katika nyanja ya teknolojia ya upimaji wa usalama wa chakula ikilinganishwa na China na nchi nyingine. China iliandaa semina hiyo muhimu ili kuisaidia Fiji kuinua kiwango cha teknolojia, na Fiji inapenda kutumia fursa hiyo kujifunza uzoefu mzuri wa China katika nyanja hiyo."

Bw. Kiyuku Prosper kutoka Chuo kikuu cha Burundi alisema, hii ni mara yake ya kwanza kushiriki kwenye semina iliyoandaliwa na serikali ya China, na semina hiyo iliwasaidia sana:

"Semina hii ni nzuri, na wataalamu wana ujuzi mkubwa, ambapo wametuonesha zana zenye teknolojia ya juu ya upimaji, natumai kuwa mafunzo hayo yatanisaidia mimi na wenzangu kuinua kiwango katika kazi ya upimaji wa usalama wa chakula."

Kwenye sherehe ya kufunga mafunzo hayo, washiriki wengi walisema watarudi nyumba kwao na teknolojia mpya katika kazi zao, ili kuzisaidia nchi zao kuinua kiwango cha upimaji wa usalama wa chakula.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-06