Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-07 16:35:16    
Li Xianhui, kijana anayejitolea kutoa mchango kwa maendeleo ya Tibet

cri

Mkoa unaojiendesha wa Tibet, China unajulikana kwa mandhari nzuri ya uwanda wa juu na utamaduni wa kabila la Watibet. Kutokana na watu wanaoishi kwenye sehemu za tambarare hawajisikii vizuri kwenye uwanda wa juu, watu wengi wanafanya matembezi ya muda mfupi tu mkoani Tibet. Lakini kuanzia mwaka 2003 baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu waliokua kwenye sehemu za tambarare walijitolea kufanya kazi mkoani Tibet, kijana Li Xianhui ni mmoja kati yao.

Sura ya mkoa unaojiendesha wa Tibet ni kama ulivyoimbwa kwenye wimbo huo, kwamba ardhi pana iliyoko kwenye uwanda wa juu wenye mwinuko mkubwa. Wastani wa mwinuko wa huko ni mita elfu 4 kutoka usawa wa bahari, ambapo kiasi cha hewa ya Oxygen ni theluthi mbili tu ya sehemu za tambarare. Ugumu wa hali ya maumbile ni tatizo la kukwama kwa maendeleo ya mkoa wa Tibet.

Tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita, serikali ya China ilianza kutekeleza sera ya mikoa mingine zaidi ya 30 kuusaidia mkoa wa Tibet, hatua ambayo ilileta maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii mkoani Tibet. Zaidi ya hayo ili kutatua tatizo la upungufu wa watu wenye ujuzi linaloikabili sehemu ya magharibi mwa China, ikiwemo Tibet, miaka mitatu iliyopita Umoja wa kikomunisti wa vijana wa China na wizara ya elimu ya China zilishirikiana kuanzisha mpango wa wanafunzi wa vyuo vikuu kujitolea kufanya kazi kwenye sehemu ya magharibi. Kutokana na mpango huo, wahitimu wa vyuo vikuu wanajitolea kwenda kwenye sehemu ya magharibi kufanya kazi kwa kipindi cha miaka miwili, wakimaliza muda huo wanahamasishwa kubaki huko. Mpango huo umewavutia wanafunzi wengi wa vyuo vikuu, akiwemo Li Xianhui mwenye umri wa miaka 28.

Huko Lhasa, mji mkuu wa Tibet mwandishi wetu wa habari alikutana na Bw. Li Xianhui. Kijana huyo aliyezaliwa na kukua katika sehemu ya pwani mashariki mwa China, ana sura nyeusi kutokana na jua kali la uwanda wa juu. Macho yake yanaonesha kuwa huyu ni mwenye akili na mchangamfu, suti yake ya kibluu inamfanya aonekane kuwa mwendesha mashtaka mwenye heshima.

Mwaka jana kabla ya kupata shahada la pili kwenye chuo kikuu cha Beijing ambacho ni chuo maarufu nchini China, kijana Li Xianhui alipata ajira ya wakati wa mapumziko katika kampuni moja ya uwakili hapa Beijing. Alipopata habari kuhusu mpango wa kuwataka wahitimu wa vyuo vikuu wanaojitolea kwenda kufanya kazi katika sehemu ya magharibi, kijana huyo alikabiliwa na njia mbili, moja ni kuingia mkataba na kampuni hiyo ya uwakili ambapo angelipwa mshahara wa Yuan zaidi ya elfu 10 kwa mwezi, na njia nyingine ni kuwa mtu anayejitolea na kulipwa mshahara usiopungua Yuan elfu moja kwa mwezi. Li Xianhui alichagua kwenda Tibet. Alisema "Tibet inanipa hisia maalumu, naona ina siri nyingi na utamaduni mkubwa wa kidini. Tibet ni mahala nilipochagua nikishiriki kwenye mpango huo wa kufanya kazi kwenye sehemu ya magharibi."

Ingawa Li Xianhui alikuwa anataka kufanya kazi mitaani, kijana huyo aliyehitimu kutoka chuo kikuu maarufu alipewa kazi katika idara ya uendeshaji wa mashtaka ya mji wa Lhasa. Kazi yake ni kutoa mafunzo ya nadharia za kisheria kwa watumishi wa idara hiyo na wa idara za uendeshaji wa mashtaka za wilayani.

Mwanzoni alipofika Tibet alikuwa hasikii vizuri kutokana na kushindwa kuzoea hali ya uwanda wa juu. Hata hivyo aliamua kuongeza muda wa kazi ili kuwapa ujuzi mwingi zaidi wanafunzi wake katika mafunzo hayo.

Mbali na kutoa mafunzo, Li Xianhui aliwekwa katika ofisi muhimu ya kuandaa mashtaka mbalimbali, pia aliteuliwa kuwa mwendeshaji mashtaka msaidizi na kuwa na madaraka ya kushughulikia kesi peke yake. Katika kazi yake kijana huyo anapenda kushughulikia kesi ngumu ambazo wengine wanaziepuka. Mwenzake wa kabila la Watibet Bw. Tsering Droje alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, "Hapa kwetu hatuna watu wenye ujuzi wa taaluma aliyosomea. Kwa mfano anashughulikia kesi za kiuchumi mara kwa mara, lakini hapa kuna watu wachache wanaoweza kushughulikia kesi za namna hii. Sisi hatutaki kuzishughulikia kesi za kiuchumi isipokuwa yeye, anaomba kesi hizo na kuzishughulikia vizuri."

Katika muda wa mwaka mmoja uliopita Bw. Li Xianhui ameshughulikia peke yake kesi zaidi ya 10. Mahakamani kesi hizo zilisikilizwa bila kusimamishwa kutokana na kosa au kukosa ushahidi wa kutosha. Kazi yake inasifiwa na viongozi na watumishi wanzake wa idara ya uendeshaji wa mashtaka. Naibu mwendeshaji mashtaka wa idara ya uendeshaji wa mashtaka ya mji wa Lhasa Bw. Liu Jiayun alimsifu akisema  "Katika kesi alizoshughulikia, alionesha msingi imara wa ujuzi wa sheria. Anachambua kwa kina na kwa makini katika kutambulisha uhalifu na adhabu zinazostahili. Mpaka sasa amefanikisha kesi zaidi ya 10."

Awali kijana huyo alipanga kufanya kazi mkoani Tibet kwa mwaka mmoja tu, na halafu arudi mjini Beijing kuendelea na kazi ya uwakili. Lakini muda wa mwaka mmoja ulipomalizika, Li Xianhui alipenda kuendelea kufanya kazi mkoani Tibet.

Alisema  "Naona mazingira ya huko yananifaa, naweza kutumia uwezo wangu ipasavyo. Nafurahia kazi hiyo. Kwa hiyo viongozi wa idara yetu waliponiomba nibaki, nikaamua kubaki."

Hivi sasa Li Xianhui ameamua kubaki na kuendelea na kazi mkoani Tibet katika siku zijazo. Mwanzoni alipokuja Tibet alikuwa mtu aliyejitokea kusaidia maendeleo ya Tibet, hivi sasa amebadilika kuwa mwendesha mashtaka.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-07