Mkutano wa 6 wa wakuu wa Asia na Umoja wa Ulaya ulifungwa tarehe 11 huko Helsinki, mkutano huo umejumuisha maarifa na mafanikio yaliyopatikana katika mikutano ya Asia na Umoja wa Ulaya katika miaka 10 iliyopita, na kupanga mpango wa maendeleo ya siku zijazo.
Mkutano huo umetangaza kupokea nchi za Bulgaria, Romania, India, Pakistan, Mongolia na sekretarieti ya Umoja wa Asia ya kusini mashariki kuwa wanachama wapya wa Baraza la Asia na Umoja wa Ulaya. Waziri mkuu wa Finland ambayo ni nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya Bwana Matti Vanhanen alitoa hotuba kwenye sherehe ya ufungaji wa mkutano akisema:
Mkutano wa wakuu wa Helsinki umetandika njia kwa ajili ya kupanua zaidi njia ya ushirikiano kati ya Asia na Umoja wa Ulaya. Tumetoa uamuzi mkubwa kuhusu upanuzi wa baraza hilo, wanachama wapya kujiunga na baraza hilo, jambo hili limeonesha kuwa Baraza la Asia na Umoja wa Ulaya ni mchakato uliojaa nguvu ya uhai, na hakika utawavuta wanachama wengi zaidi kujiunga. Kwenye mkutano huo tumepitisha taarifa ya mwenyekiti wa mkutano wa 6 wa wakuu wa Asia na Umoja wa Ulaya na taarifa nyingine mbili muhimu. Kati ya hizo taarifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa imetoa ishara yenye nguvu kwa dunia, yaani nchi wanachama wa Baraza la Asia na Umoja wa Ulaya zitashinda kwa pamoja matishio yatakayoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa kwa maendeleo endelevu. Taarifa ya Helsinki kuhusu maendeleo ya siku zijazo ya Baraza la Asia na Umoja wa Ulaya imethibitisha kanuni za jumla ili kusukuma mbele maendeleo ya mchakato wa Baraza la Asia na Umoja wa Ulaya na kuhimiza Asia na Umoja wa Ulaya ziendeleze uhusiano ulio wa karibu zaidi .
Waziri mkuu wa China Wen Jiabao alifafanua msimamo wa China kuhusu mada mbalimbali kwenye mkutano huo. Kuhusu kuimarisha ushirikiano wa pande mbalimbali na kukabiliana na tishio dhidi ya usalama duniani, waziri mkuu Wen Jiabao alisema, lazima kuimarisha uwezo wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na tishio jipya na changamoto mpya, kuondoa hatari dhidi ya usalama wa kote duniani, kushikilia mazungumzo ili kuondoa migogoro ya duniani, kupinga kutumia nguvu au kutishia kutumia nguvu, kuzidisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi na kupinga kutumia vigezo vya aina mbili katika mapambano hayo, kuanzisha mfumo wa usimamizi wa uuzaji wa silaha ili kuzuia kutoeneza silaha kwa pande zote, kuimarisha utekelezaji wa sheria na kuanzisha ushirikiano katika kinga na tiba ya magonjwa ya maambukizi.
Ili kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa kiwenzi wa aina mpya, waziri mkuu Wen Jiabao pia alitoa mapendekezo mbalimbali kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya kampuni zenye ukubwa wa kati au kampuni ndogo, kuzuia kwa pamoja ugonjwa wa homa ya mafua ya ndege na magonjwa mengine kote duniani, na kutunga mikakati ya jumla ya maendeleo ya vijiji. Alisisitiza pia kuwa nchi zilizoendelea zinapaswa kuzisaidia nchi zinazoendelea katika sekta za usalama wa nafaka na kupunguza umaskini, pia ameahidi kuwa China itachukua hatua zenye juhudi kutimiza lengo la kupunguza matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira.
Mapendekezo hayo yamekubaliwa na pande nyingi zilizohudhuria mkutano huo, ambapo nchi hizo zina imani kubwa ya kuendeleza uhusiano kati yao na China.
Mkutano wa awamu ijayo yaani mkutano wa 7 wa wakuu wa Asia na Umoja wa Ulaya utafanyika Beijing mwezi Oktoba mwaka 2008. Waziri mkuu Wen Jiabao ana matarajio makubwa juu ya mkutano huo alisema: Natarajia kufanya juhudi pamoja na viongozi wa nchi mbalimbali kwa kuongeza mazungumzo ya kimkakati kati ya Asia na Umoja wa Ulaya, kusukuma mbele ushirikiano halisi kwenye sekta za uchumi na biashara, kuanzisha maingiliano na mazungumzo kuhusu utamaduni na ustaarabu wenye tofauti, ili kutoa mchango mkubwa zaidi kwa ajili ya kuimarisha na kuzidisha uhusiano wa kiwenzi wa aina mpya kati ya Asia na Umoja wa Ulaya.
|