Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-13 19:55:03    
Wataalamu wa matibabu ya jadi ya kichina waeleza madhara yanayoweza kutokana na dawa za mitishamba za kichina

cri

Hivi karibuni idara ya usalama wa dawa ya Uingereza ilitangaza matukio ya wagonjwa kupatwa na madhara baada ya kutumia dawa za mitishamba za kichina, na kuwaonya raia wa nchi hiyo wasitumie ovyo dawa hizo ovyo. Aina moja ya dawa ya jadi ya kichina iliyotengenezwa kwa aloe inasadikiwa kuwa na hydrargyrum kupita kiasi ikilinganishwa na vigezo vya nchi hiyo, aina nyingine ya dawa ya mitishamba inayoitwa kitaaluma Polygonum multiflorum inadhaniwa kuwa inaweza kusababisha ugonjwa wa manjano. Kutokana na hali hiyo, watu wengi wameanza kuwa na mashaka kuhusu usalama wa kutumia dawa za mitishamba za kichina. Wataalamu wa matibabu ya kichina wanaeleza kuwa, inapaswa kufahamu waziwazi sumu na madhara yanayoweza kutokana na matumizi ya dawa za mitishamba za kichina, kusema moja kwa moja kuwa dawa hizo zina sumu au hazina sumu ni makosa.

Dawa za mitishamba za kichina ni "zenye sumu au la" kihalisi inamaanisha kama dawa hizo zinaleta madhara au la. Katika muda mrefu uliopita, watu wamekuwa wakiamini kuwa kwa kuwa dawa za mitishamba za kichina zinategenezwa kwa kutumia vitu vya kimaumbile, hivyo hazina madhara kwa afya ya binadamu. Kutokana na mtizamo huo, watu wanashangaa sana wanapoambiwa kuwa dawa hizo pia zinaweza kuwa na madhara. Mwanachama wa taasisi ya uhandisi ya China, ambaye pia ni mtafiti mkuu wa taasisi ya sayansi ya matibabu ya jadi ya kichina Bw. Li Lianda alisema,

"usemi kuwa dawa za mitishamba za kichina ni salama na hazina sumu si sahihi, dawa zote zina madhara ya kiasi fulani, huo ni ufahamu wa kawaida."

Kihalisi, dawa zote bila kujali dawa za mitishamba au dawa za kemikali za kimagharibi, zote zinaweza kuwa na madhara. Kwa mfano dawa inayotumiwa mara kwa mara penicillin inaweza kusababisha watu kuzirai. Kati ya dawa za mitishamba za kichina, dawa moja inayotunza ini inayoitwa Manchurian dutchmanspipe stem inaweza kudhuru vibaya figo za binadamu. madhara ya dawa hayaepukiki, wakati wagonjwa wanatibiwa kwa dawa, pia wanakabiliwa na hatari kadhaa wa kadhaa.

Wataalamu wanaona, baada ya kuacha mtizamo kuwa dawa za mitishamba za kichina hazina madhara, wagonjwa wanapaswa kufahamu kuwa, ingawa kuna hatari ya kutokea kwa madhara, lakini utafiti na uzalishaji wa dawa yoyote ya mitishamba ya kichina unahitaji kufanyiwa majaribio mbalimbali ili kuthibitisha usalama wake. Kabla ya kupita majaribio yote, dawa hairuhusiwi kutumika kwa binadamu, sembuse kuuzwa nchini na kwa nchi za nje. Hivyo usemi kuwa dawa za mitishamba za kichina zina sumu kali si sahihi. Wataalamu wanasema, hivi sasa bado kuna watu wengi wanaoelewa kwa makosa matumizi dawa za mitishamba za kichina na namna ya kuzitumia.

Kosa la kwanza ni kuwa madhara yanayotokana na matumizi mabaya ya dawa hizo yanachukuliwa kuwa dawa hizo zina sumu kali. Kuhusu hali hiyo, mkurugenzi wa idara ya kutathmini usalama wa dawa za mitishamba za kichina katika taasisi ya matibabu ya jadi ya China Bi. Liang Aihua alisema, kuna tofauti za kimsingi kati ya matumizi ya dawa za magharibi na dawa za mitishamba za kichina, kutokana na kuwa madaktari wengi wa nchi za nje hawaelewi nadharia ya matibabu ya jadi ya kichina, hivyo ni vigumu kwao kuelekeza wagonjwa watumie dawa za mitishamba za kichina kwa njia sahihi, na makosa mbalimbali hutokea mara kwa mara. Bi. Liang Aihua alisema:

"hivi sasa katika baadhi ya zahanati za nchi za nje, madaktari wanaoshughulikia matibabu ya jadi ya kichina wanakosa uzoefu, hivyo idadi ya matukio ya kutokea kwa madhara baada ya kutumia dawa za mitishamba za kichina inazidi kwa kiasi kikubwa ile ya nchini China. Kuhusu matukio kadhaa makubwa ya madhara yaliyotokea nchi za nje, yanatokana na kuwa wanakosea kutumia dawa au kukosea kiwango na jinsi ya kutumia dawa."

Mgongano wa pili kuhusu usalama wa dawa za mitishamba za kichina ni kuwa dawa hizo zenyewe zina vitu vyenye sumu. Uchunguzi umethibitisha kuwa, baadhi ya dawa za mitishamba za kichina kweli zina hydrargyrum au kemikali zenye sumu, au chembechembe za mitishamba na wadudu wenye sumu. Kwa mujibu wa nadharia ya matibabu ya magharibi, vitu hivyo bila shaka vinasababisha madhara kwa binadamu. Lakini nadharia ya matibabu ya jadi ya kichina inasisitiza kushughulikia na kutumia kwa njia mwafaka vitu hivyo vyenye sumu, kutumia sumu hizo kutibu magonjwa, na kuondoa au kupunguza sumu kufikia kiwango cha usalama kwa binadamu kwa njia ya kuzichanganya dawa mbalimbali. Kidhahiri, matibabu ya magharibi na matibabu ya jadi ya kichina ni mifumo miwili tofauti ya matibabu, nadharia ya matibabu ya jadi ya kichina kuhusu sumu haiwezi kuungwa mkono na matibabu ya magharibi.

Mwandishi wetu wa habari aliwahoji wataalamu husika kuhusu dawa hizo mbili zilizotangazwa kuwa "sio salama" kwa matumizi ya binadamu na idara husika ya Uingereza. Mtaalamu wa taasisi ya matibabu na dawa za mitishamba za kichina alisema, hydrargyrum iliyopo kwenye dawa hiyo imeshughulikiwa na kuwa na sumu ya kiwango cha chini. Majaribio mengi yamethibitisha kuwa, dawa hiyo ni salama kwa binadamu ikitumiwa kwa njia sahihi na kiwango mwafaka.

Lakini wataalamu wa matibabu ya jadi wa China pia wamedhihirisha kuwa, kutokana na kuwa uzalishaji wa dawa za mitishamba za kichina unahitaji ufundi wa kiwango cha juu, hivi sasa bado kuna dawa kadhaa ambazo haziwezi kufikia vigezo vinavyotakiwa. mkurugenzi wa elimu ya dawa za mitishamba za kichina wa shule ya udaktari ya Beijing Bw. Jin Shiyuan alieleza kuwa, utaalamu wa kushughulikia malighafi ya dawa za mitishamba za kichina unaathiri sana ubora na usalama wa dawa hizo. Hivyo makampuni ya dawa yanapaswa kutilia maanani katika kuinua kiwango cha utaalamu.

Wasikilizaji wapendwa, matibabu ya jadi ya kichina ambao ni urithi muhimu kwa China yana nadharia nyingi na uzoefu uliokusanywa katika milenia kadhaa zilizopita, na yanaaminiwa na kupendwa na watu wa China na nchi za nje kutokana na ufanisi wake mzuri. Kwa hivyo haifai kusisitiza na kutia chumvi kuwa dawa za mitishamba za kichina zina sumu, na hata kukataa ufanisi na usalama wa dawa hizo. Hata kama hivyo, matibabu ya jadi ya kichina pia yanapaswa kuendelea kuimarisha utafiti wa kisayansi, ili kuinua zaidi sifa wake.