Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-13 19:57:44    
Teknolojia mpya zafuatiliwa katika shughuli za uchapishaji za China na nchi za nje

cri
Maonesho ya vitabu ya kimataifa yalifanyika hivi karibuni hapa Beijing, na baraza la uchapishaji la kimataifa la Beijing lilifanyika tarehe 28, Agosti, na teknolojia mpya imekuwa suala muhimu lililofuatiliwa na wafanyabiashara wa uchapishaji wa nchini na wa kutoka nchi za nje.

Mwaka huu baraza la uchapishaji la kimataifa linaendeshwa na Idara kuu ya habari na uchapishaji ya China na Ofisi ya habari ya Baraza la serikali la China, na kauli mbiu ya baraza hilo ni "mustakabali wa teknolojia mpya na sekta ya uchapishaji." Maofisa na wataalamu mia kadhaa wa idara za uchapishaji za China na nchi za nje walifanya majadiliano kuhusu changamoto na fursa zinazoletwa na teknolojia za tarakimu, mtandao wa Internet na upashanaji wa habari kwa shughuli za jadi za uchapishaji. Naibu mkuu wa Ofisi kuu ya habari na uchapishaji ya China Bw. Yu Yongzhan alitoa hotuba akieleza kuwa, teknolojia mpya imeleta fursa nyingi mpya kwa shughuli za uchapishaji, kwani sayansi na teknolojia mpya na ya hali ya juu zimeinua kiwango cha uendeshaji wa shughuli za jadi za uchapishaji, kama vile: utandawazi wa upashanaji habari katika mashirika ya uchapishaji, kufanya uchapishaji kutokana na mahitaji halisi, maduka ya vitabu kwenye mtandao wa Internet, na uendeshaji na mauzo ya vitabu kwa kutumia mtandao wa Internet, hali ambayo imepunguza gharama za shughuli za jadi za uchapishaji, na kuongeza ma uzo ya vitabu, lakini kwa upande mwingine, teknolojia mpya vilevile imeleta athari mbaya kwa shughuli za jadi za uchapishaji, Bw. Yu anasema:

"Teknolojia za tarakimu na mtandao wa Internet vilevile zimeleta changamoto kubwa kwa shughuli za jadi za uchapishaji, ambapo teknolojia mpya imepunguza masharti ya kufanya uchapishaji, aidha njia mpya ya matangazo pia imetoa vikwazo kwa njia ya jadi ya uchapishaji. Watu wanaweza kusoma mambo yaliyowekwa kwenye mtandao wa Internet bila ya kulipa, hali ambayo imefanya ushindani mkubwa katika shughuli za jadi za uchapishaji zinavyopata faida kutokana na uchapishaji wa vitabu."

Bw. Yu Yongzhan alisema, katika utaratibu wa jadi wa upashanaji wa habari, uchapishaji wa vitabu unategemea uwekaji mipango wa Shirika la uchapishaji. Lakini baada ya kutokea kwa teknolojia ya tarakimu, mtu yeyote anayefahamu ujuzi wa kimsingi wa kompyuta au mwenye kompyuta wanaweza kushughulikia kazi hiyo, na mtu yeyote anaweza kuweka makala zake katika mtandao wa Internet. Kutokana na hali hiyo, shirika la uchapishaji si chombo muhimu kwenye utaratibu wa kufanya uchapishaji, na maduka ya vitabu si chombo muhimu katika utaratibu wa biashara ya vitabu, hali ambayo imeleta ushindani mkubwa na shinikizo kubwa kwa shughuli za jadi za uchapishaji.

Lakini teknolojia mpya vilevile zimeleta fursa mpya za biashara. Mkuu wa kampuni ya uchapishaji ya Harper Collins bibi Jane Friedman alisema, kampuni yake ikiwa kampuni kubwa ya tatu ya uchapishaji wa vitabu ya Kiingereza duniani, imebadilisha njia ya jadi ya uchapishaji kwa kutumia mtandao wa Internet, simu za mkononi, na Video. Bibi Friedman ana imani kubwa juu ya mustakabali wa soko la uchapishaji nchini China akisema:

"Kampuni ya Harper Collins inafanya juhudi za kufanya uchapishaji kwa kutumia teknolojia ya tarakimu, na kupanua soko nchini China na India. Takwimu zinaonesha kuwa, vijana wa Marekani hutembea mtandao wa Internet kabla ya kununua vitabu dukani, na idadi ya wachina wanaosoma kwenye mtandao wa Internet inaongezeka katika miaka kadhaa iliyopita."

Mkuu wa Shirika la uchapishaji wa pamoja la Hongkong Bw. Chen Wanxiong pia anaona kuwa, mageuzi makubwa yatafanyika katika sekta ya uchapishaji katika miaka kumi ijayo, akisema:

"Katika miaka 15 iliyopita, teknolojia mpya zimesukuma mbele mageuzi ya shughuli za kijadi za uchapishaji, na miaka 10 ijayo itakuwa ni kipindi muhimu kwa shughuli hizo."

Lakini Bw. Chen Wanxiong pia anaona kuwa, hivi sasa uendeshaji wa shughuli za uchapishaji kwa kutumia teknolojia ya tarakimu bado haujaenea duniani, hali ambayo inahusiana na kutokamilika kwa teknlojia mpya, na kutolingana kwa jamii na shughuli mbali mbali za biashara.

Kauli mbiu ya baraza hilo ni teknolojia mpya, na hii inahusiana na soko kubwa la matumizi ya bidhaa za tarakimu nchini China. Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia mwezi uliopita, idadi ya wachina wanaotembea mtandao wa Internet imefikia milioni 123, na wanaotumia simu za mkononi ni zaidi ya milioni 440. Serikali ya China imetoa mwito wa kuunganisha vyombo vya kijadi na mawasiliano ya mtandao wa Internet, hali ambayo imeweka hali nzuri kwa shughuli za jadi za uchapishaji kutumia teknolojia mpya. Naibu mkuu wa Idara kuu ya habari na uchapishaji ya China Bw. Yu Yongzhan anasema:

"Tunafahamu sana hali ya ushindani, migongano na kupatana kwa aina tofauti za uchapishaji, hivyo tunahimiza shughuli za jadi za uchapishaji zitumie teknolojia mpya ili kukabiliana na changamoto zinazoletwa na mtandao wa Internet na teknolojia ya tarakimu, pia idara yetu imetoa sera na kanuni kadhaa ili kuhimiza maendeleo ya uchapishaji kwa kutumia mtandao wa Internet."

Bw. Yu Yongzhan alisema China inafanya uvumbuzi kwa kujitegemea na kupata teknolojia mbalimbali mpya, lakini pia ameeleza kuwa hali ya matumizi ya teknolojia mpya katika mashirika zaidi ya 500 ya uchapishaji nchini China hailingani, na bado kuna pengo kubwa kati ya China na nchi zilizoendelea katika sekta hiyo, kwani China inahitaji kiasi kikubwa cha vitabu vyenye bei ya chini, na mashirika mengi ya uchapishaji hayajafuatilia vya kutosha teknolojia mpya.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-13