Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-14 15:53:08    
Wachina wanaoishi ng'ambo wafuatilia maendeleo ya vijiji vya China

cri

Hivi karibuni katika kijiji cha Dacheng mkoani Henan, katikati ya China watu waliwazungumzia sana wazee wawili waliokuja kutembelea kijiji hicho. Wazee hao ni wakalimani wenye uzoefu mkubwa wa Umoja wa Mataifa, Bw. Hua Junxiong kutoka Taiwan, China na Bw. Liu Dazheng kutoka Hong Kong, China. Hivi sasa wazee hao wawili wameteuliwa kuwa wakuu wa heshima wa kijiji cha Dacheng.

Siku moja mwezi Juni mwaka huu, kijiji cha Dacheng kilijaa furaha, watu wa huko walicheza ngoma ya simba kama wanavyofanya wakati wa sikukuu. Wanakijiji walisubiri kando ya barabara kuwasalimu wazee hao wawili, ambao ni Bw. Hua Junxiong na Bw. Liu Dazheng wanaofanya kazi ya ukalimani katika Umoja wa Mataifa. Safari hii walifika kwenye kijiji cha Dacheng kuwatembelea jamaa zao kutoka New York, Marekani.

Wazee hao wawili walitoka Taiwan na Hong Kong, lakini mbona jamaa zao wapo katika kijiji hicho? Ili kupata ufahamu kuhusu jambo hilo, hebu kwanza tumfahamu mkalimani mwenzao Bw. Cao Guozhong. Bw. Cao Guozhong mwenye umri wa miaka 37 alizaliwa na kukulia katika kijiji cha Dacheng. Mpaka sasa amefanya kazi katika Umoja wa Mataifa kwa miaka minane, na amejenga urafiki mkubwa na wazee hao wawili.

Bw. Cao Guozhong yupo mbali na maskani yake, lakini hajasahau ndugu zake kijijini. Anatuma fedha zake mara kwa mara ili kuchangia maendeleo ya kijiji hicho. Wazee hao wawili walifurahishwa na moyo wake wa kutoa mchango.

Bw. Hua Junxiong alisema "Mimi na Liu Dazheng sote tulizaliwa kwenye familia maskini. Tunapenda kutoa mchango kwa sehemu ya vijiji yenye hali duni ya maendeleo. Cao Guozhong alifahamishwa nia yetu, akatuelezea hali ya kijiji hicho, tukaona hii ni fursa nzuri ya kutimiza matumaini yetu."

Kijiji cha Dacheng ni kijiji maskini kikilinganishwa na vijiji jirani, ambavyo vilianza kupata maendeleo katika miaka ya hivi karibuni. Lakini kijiji cha Dacheng bado kina hali duni ya maendeleo, ambapo hakuna barabara nzuri, na shule ya msingi ya huko ina zana mbovu.

Wazee hao wawili walipofahamishwa hali ya kijiji hicho, walishauriana na kukubaliana kutoa dola za kimarekani elfu 10 kila mmoja, kukisaidia kijiji hicho kujenga barabara na kukarabati shule. Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, fedha hizo zilizotumwa kutoka Marekani zilifika kwenye kijiji hicho. Sehemu ya fedha hizo zilitumiwa kununua kompyuta kwa ajili ya shule ya msingi, na nyingine zilitumika katika ujenzi wa barabara kijijini.

Wanakijiji walitiwa moyo na mchango wa wazee hao wawili wanaoishi mjini New York. Mwanakijiji Bw. Zuo Canzhang alisema "Nilifurahi sana hata nilitokwa na machozi, kwani jambo la namna hii halijawahi kutokea katika siku zilizopita. Kijiji chetu ni maskini. Kitendo cha wazee hao wawili wenye asili ya China kutoa mchango kusaidia maendeleo ya kijiji chetu, kimenifurahisha kiasi kwamba nashindwa hata kufafanua."

Mbali na msaada wa fedha, wazee hao wawili pia wamewaletea wanakijiji kitu kingine. Mkuu wa kijiji hicho Bw. Li Guangle alieleza kuwa, awali wanakijiji walikuwa hawana mshikamano, walikuwa hawafurahii kushiriki kwenye shughuli za umma. Baada ya kufahamishwa kuwa wazee wawili waliopo mbali sana wanafuatilia maendeleo ya kijiji hicho, mabadiliko yalianza kutokea miongoni mwa wanakijiji. Hivi sasa wakimaliza kazi waliyopewa, wanahiari kufanya kazi za kujitolea. Katika ujenzi wa barabara ya kijiji, wanakijiji wote wenye nguvu ya kufanya kazi walishiriki kwenye ujenzi huo. Bw. Li Guangle alisema, mabadiliko hayo yaliletwa na wazee hao wawili. Alisema "Safari hii walikuja, si kama tu walituletea msaada wa fedha, bali pia walitusaidia kutatua matatizo mbalimbali. Jambo muhimu zaidi ni moyo wao wa kuwasaidia wengine. Sisi Wachina tunasema ukipata maendeleo unapaswa kuwasaidia wenzako, hii ni tabia nzuri ya Wachina. Wazee hao wawili wameonesha tabia ya kupenda taifa na wananchi wenzao, tabia hiyo ni kitu kinachothaminiwa sana."

Kutokana na nguvu ya ushawishi ya wazee wawili kwenye kijiji hicho, wanakijiji waliwateua kuwa wakuu wa heshima wa kijiji hicho, na kuwaalika kutembela kijiji hicho. Wazee hao wawili walikubali mwaliko huo.

Katika ziara hiyo, Bw. Liu Dazheng alipohojiwa alisema  "Kwetu hii vile vile ni fursa ya kujifunza. Tunatumai kupata fursa ya kuwasiliana na Wachina wa kawaida, kusikiliza maoni yao, kufahamishwa wanavyotaka, shida zao, matatizo yanayowakabili na sisi tunaoishi kwenye nchi ya kigeni tunaweza kuwasaidia vipi. Tunafurahia kupata ufahamu mwingi zaidi kuhusu sehemu ya vijiji ya China kwa kushiriki kwenye mambo halisi."

Ili kutoa shukrani wanakijiji walikubaliana kuwapa wazee wawili viwanja viwili vya kujenga makazi. Lakini wazee hao waliamua viwanja hivyo vitumike kujenga maktaba au kituo cha kufanyia mazoezi ya kujenga mwili kwa wazee. Walieleza kuwa wakiwa wakuu wa heshima wa kijiji hicho, wanapaswa kufanya kila wawezalo kuwanufaisha wanakijiji wa huko.

Wazee hao wawili wana imani kubwa na mustakabali wa kijiji cha Dacheng. Mzee Liu Dazheng alisema "Tulichofanya ni kutoa mchango mdogo, huu ni mwanzo tu. Tungependa kushiriki, kufuatilia na kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya kijiji hicho kwa muda mrefu ujao. Labda baada ya miaka mitano au kumi ijayo, kijiji cha Dacheng kitaonesha sura mpya na kuweka mfano miongoni mwa vijiji vya mkoani Henan."

Idhaa ya kiswahili 2006-09-14