Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-14 15:51:49    
Watu wa kabila la Wanu wapata maendeleo kwa kujishugulisha na utalii

cri
Kabila la Wanu ni kabila lenye watu wachache nchini China. Wanu wengi wanaishi kando ya bonde la mto wa Nujiang, mkoani Yunnan, kusini magharibi mwa China. Eneo hilo la milima lina hali duni ya mawasiliano, hali ambayo imefanya kabila hilo liwe nyuma kimaendeleo. Hivi sasa watu kadhaa wa kabila la Wanu wakisaidiwa na serikali ya huko, wameanza kujishughulisha na utalii na kupata maendeleo.

Mwandishi wetu wa habari alipanda basi kutoka Kunming, mji mkuu wa mkoa wa Yunnan kuelekea kwenye wilaya inayojiendesha ya kabila la Wanu na kabila la Wadulong la Gongshan. Safari hiyo ilichukua karibu saa 18. Baadaye basi hilo lilisafiri kwa zaidi ya saa moja kando ya bonde la mto wa Nujiang kabla ya kuwasili kwenye kijiji cha Jiasheng, wanakoishi watu wa kabila la Wanu.

Kuangalia kutoka mbali, kijiji hicho kinazungukwa na milima na misitu. Basi liliingia kwenye kijiji hicho, ambapo kando ya barabara, nyumba mpya za mbao za mtindo wa kabila la Wanu zimepangwa vizuri, nyimbo za Wanu zinasikika kutoka kwenye nyumba hizo.

Katika nyumba ya mwanakijiji Liu Yanghai, mwandishi wetu wa habari aliona vyombo mbalimbali vya umeme vya nyumbani vikiwemo televisheni, jokofu na mashine ya kufulia nguo. Vyombo hivyo vya kisasa kuwepo katika nyumba za wakulima zilizoko milimani na mbali na mji, hali ambayo imeonesha tofauti kabisa na picha ya umaskini aliyopata mwandishi wetu wa habari kabla ya kufanya ziara hiyo.

Bw. Liu Yanghai alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hapo awali familia yake ilikuwa maskini, lakini maisha yalianza kuboreshwa tangu alipoanza kujishughulisha na utalii. Alisema  "Kabla ya kuanza kujishughulisha na shughuli za utalii, tulikuwa na pato dogo na hatukuwa na vyanzo vingi vya mapato, ambapo tulitegemea shughuli za kilimo na kufuga kuku, na maisha yalikuwa magumu."

Miaka 6 iliyopita katika juhudi za kuondokana na umaskini, serikali ya huko iliamua kuwasaidia watu wa kijiji hicho kuendeleza shughuli za utalii kwa kuzingatia ipasavyo sifa maalum za sehemu ya mtiririko wa Mto Nujiang. Bw. Liu Yanghai alikopa kutoka kwa jamaa na marafiki, kujenga nyumba kadhaa za kulala wageni ili kuwavutia watalii kutembelea kijiji hicho. Kuanzia hapo wageni wengi kutoka wilaya na miji walimiminikia kwenye kijiji hicho, kula chakula cha mtindo wa kabila la Wanu na kuburudishwa kwa ngoma na nyimbo za kabila hilo.

Bw. Liu Yanghai alisema aina moja ya mapishi iliyoandaliwa na mke wake inawafurahisha sana wageni. Aliongeza kuwa katika miaka 6 iliyopita tangu aanze kujishughulisha na utalii, pato la familia yake liliongezeka kati ya Yuan elfu 10 na 20 kwa mwaka, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani kati ya 1,250 na 2,500. Mpaka sasa mbali na kulipa madeni yote, amenunua vyombo kadhaa vya umeme vya nyumbani, na pia ameweka akiba ya fedha.

Katika mazungumzo na mwandishi wetu wa habari, simu yake ilikuwa inaita, ambapo bwana huyo alijibu  "Ni usiku wa leo? andaa meza moja? Mtafika saa ngapi? Sawa, hamna shida."

Akimaliza bwana huyo alimwambia mwandishi wetu wa habari kwa tabasamu kuwa, simu hiyo ya kuagiza chakula ilipigwa kutoka wilayani, na wageni watakuja nyumbani kwake usiku. Kwa hiyo mwandishi wetu wa habari alimwaga Bw. Liu akiwa na pilika pilika za maandalizi.

Katika nyumba ya jirani msichana mmoja aliyekuwa amevaa nguo za kabila la Wanu aliwavutia watu macho. Nguo hizo zilishonwa kwa vitambaa vya maua vilivyotengenezwa na Wanu kwa mikono. Ua wa nyumba anayoishi msichana huyo ni mkubwa zaidi kuliko ule wa jirani yake, ambapo limechimbwa shimo na kulimbikizwa mlima mdogo wa bandia. Kando ya shimo hilo kuna kibanda kimoja cha mapumziko.

Msichana huyo anaitwa Kai Chu, ana umri wa miaka 23. Sawa na Bw. Liu Yanghai, familia ya msichana huyo pia ilianza kujishughulisha na utalii mwaka 2000. Hapo awali baba yake alikuwa anafanya kazi wilayani na mama yake alikuwa anaendesha duka moja dogo kijijini, Dada Kai Chu mwenyewe alikuwa anafanya kazi za vibarua nje ya kijiji hicho. Ingawa familia hiyo ilikuwa ina uwezo mkubwa zaidi kuliko wanakijiji wenzake, lakini maisha hayakuwa mazuri sana. Hali hiyo ilianza kubadilika baada ya kuanza kujishughulisha na mambo ya utalii. Kutokana na kuwa biashara ilikuwa inapamba moto siku hadi siku, Dada Kai Chu alirudi kwenye maskani yake. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, shughuli za utalii si kama tu ziliongeza pato la wanakijiji, bali pia zilisaidia kueneza na kuhifadhi utamaduni wa kabila la Wanu, kwani wageni walijionea mila na desturi za kabila hilo.  Msichana huyo aliimba wimbo huo wa kabila la Wanu na kutoa pombe zilizotengenezwa na watu wa huko. Alisema mbali na kuwaandalia wageni chakula cha mtindo wa kabila la Wanu, wasichana wa kijiji hicho pia walionesha ngoma maalumu wa kabila hilo. Utamaduni wa kabila la Wanu unawavutia watalii wengi zaidi.

Msichana huyo alieleza mpango wake, akisema  "Kama idadi ya watalii itaongezeka, nina mpango wa kuanzisha kundi la sanaa kufanya maonesho katika nyumba za kulala kwa wageni, ambapo wanakijiji wataweza kupata pesa nyingi zaidi. Vile vile ninataka kujenga upya nyumba zenye umaalumu wa kabila la Wanu. Mpango wa tatu ni kuwaandalia wageni nyumba za kulala na mboga, ambapo wataweza kujipikia chakula na kuona jinsi watu wa kabila la Wanu wanavyoishi."

Kijiji hicho kina familia zaidi ya 50. Ofisa wa huko anayeshughulikia mambo ya makabila madogomadogo Bw. Feng Weixiang alisema, serikali itaandaa mazingira mazuri zaidi, ili kuwashirikisha wanakijiji wengi wa kabila la Wanu kwenye mambo ya utalii na kupata maendeleo.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-14