Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-14 19:39:47    
Mkutano wa viongozi wa nchi zisizofungamana na upande wowote wafuatiliwa

cri

Mkutano wa 14 wa viongozi wa nchi zisizofungamana na upande wowote utafunguliwa tarehe 15 Septemba huko Havana. Huu ni mwaka wa 45 tokea harakati ya kutofungamana na upande wowote ianzishwe. Licha ya kuwa mkutano huo utajadili masuala muhimu ya kimataifa yaliyopo sasa, pia utajadili namna harakati hiyo itakavyotoa mchango mkubwa zaidi katika mazingira ya hivi sasa ya kimataifa. Kwa hiyo mkutano huo unafuatiliwa sana duniani.

Harakati ya kutofungamana na upande wowote ilianzishwa mwaka 1961, ni jumuyia muhimu ya nchi zinazoendelea yenye lengo la kujiimarisha na kushirikiana katika mambo ya kimataifa. Hivi sasa jumuyia hiyo ina nchi wanachama 116. Habari kutoka Cuba zinasema marais au wawakilishi wao kutoka nchi 115, na wajumbe kutoka nchi 15 wachunguzi  na wajumbe kutoka nchi 31 zilizoalikwa mahsusi na jumuyia 23 za kimataifa akiwemo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan watahudhuria mkutano huo. Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Yang Jiechi ataongoza ujumbe wa China kuhudhuria mkutano huo.

Huu ni mkutano unaofanyika wakati ambapo hali ya suala la nyuklia la Iran inazidi kuwa mbaya. Mkutano huo utaonesha msimamo wa kuunga mkono Iran kuendeleza nishati ya nyuklia kwa lengo la matumizi ya amani. Kabla ya mkutano huo, kwenye mkutano wa viongozi na mawaziri wa mambo ya nje washiriki wote wameona kuwa kuendeleza, kutafiti na kuzalisha nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani ni haki ya kimsingi kwa nchi zote, na haki hiyo haistahiki kunyimwa. Mashambulizi na matishio yoyote dhidi ya miundombinu ya nyuklia inayotumika kwa ajili ya matumizi ya amani ni ukiukaji wa wazi dhidi ya sheria za kimataifa, katiba ya Umoja wa Mataifa na kanuni husika za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki.

Suala la ugaidi litakuwa mada nyingine muhimu itakayojadiliwa katika mkutano huo. Hivi sasa tishio la ugaidi limekuwa changamoto mpya kwa harakati za kutofungamana na upande wowote. Kabla ya mkutano huo, kwenye mkutano wa viongozi na mawaziri wa mambo ya nje, washiriki wengi walitaka kuwa na tafsiri bayana ya "ugaidi". Waliona kwamba uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq na uvamizi wa Israel dhidi ya Lebanon, wote unastahili kuchukuliwa kama ni ugaidi, na waliikosoa Marekani kwa kutumia vigezo tofauti katika vita dhidi ya ugaidi. Mswada wa taarifa ya pamoja uliotayarishwa na washiriki wa mkutano huo kwa ajili ya mkutano wa viongozi wa nchi zisizofungamana na upande wowote unalaani aina yoyote ya ugaidi na hasa vitendo vya mauaji dhidi ya raia, na unasema nchi zisizofungamana na upande wo wote "zinapinga kabisa nchi fulani kushutumu nchi nyingine kuwa ni 'nchi za uhuni' kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi".

Mada nyingine ya mkutano huo ni namna ya kupatia uhai kama zamani harakati ya kutofungamana na upande wo wote. Katika kipindi cha vita vya baridi harakati hiyo zilikuwa na taathira kubwa, lakini baada ya kumalizika kwa vita hivyo, kutokana na sababu fulani harakati hiyo imefifia. Lakini lengo kuu la harakati hiyo bado linaungwa mkono, katika mazingira ya sasa ya kimataifa kazi yake inafaa kuimarishwa. Waziri wa mambo ya nje wa Cuba Bw. Felipe Perez Roque kwenye ufunguzi wa mkutano wa viongozi na mawaziri wa mambo ya nje uliofanyika tarehe 11 alisema, uhai wa harakati ya kutofungamana upande wowote unapaswa kurudishwa ili harakati hiyo iwe na umoja zaidi na itoe mchango mkubwa zaidi katika mambo ya kimataifa.

Licha ya mada hizo mkutano huo utajadili suala la Palestina, kuanzisha mfumo mpya wa kiuchumi duniani na mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Kwenye mkutano huo nchi za Haiti na Saint Kitts and Nevis zitapokelewa rasmi kuwa nchi wanachama wa hatakati ya kutofungamana na upande wowote.