Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-18 16:22:15    
Wachapishaji wa vitabu wa nchi za nje wamimina kwenye tamasha la kimataifa la vitabu mjini Beijing

cri

Tamasha la 13 la kimataifa la vitabu lilifanyika mjini Beijing kuanzia tarehe 30 Agosti hadi tarehe 2 Septemba, wachapichaji wa vitabu 1,700 kutoka nchi 50 walishiriki kwenye tamasha hilo. Idadi hiyo ni karibu maradufu kuliko tamasha lililotangulia.

Tamasha la kimataifa la vitabu lilianzishwa mwaka 1986, kuanzia mwaka 2002 linafanyika kila mwaka badala ya kila miaka miwili kama ilivyokuwa hapo awali. Tamasha hilo linaandaliwa na Idara Kuu ya Uchapishaji ya China na Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China, mada ya tamasha hilo ni "Kuingiza vitabu vizuri duniani nchini China na kuvieneza vitabu vya China duniani". Katika muda wa miaka 20 iliyopita tamasha la kimataifa la vitabu limestawi na kuwa tamasha kubwa katika biashara ya haki za kunakili, biashara ya vitabu, maonesho ya vitabu na mabadilishano ya habari kuhusu uchapishaji.

Maendeleo makubwa ya tamasha hilo yanaonekana zaidi katika biashara ya haki za kunakili. Hapo mwanzo biashara hiyo ilikuwa na vitabu mia kadha tu, lakini mwaka jana biashara hiyo ilifikia vitabu 9,000. Idadi ya washiriki wa tamasha la mwaka huu ni maradufu kuliko mwaka jana, na kati yao 1200 walitoka nchi za nje. Kutokana na hali hiyo, kwa makadirio biashara na mikataba ya biashara ya haki za kunakili hakika itakuwa kubwa kuliko mwaka jana.

Bw. Huw Alexander ni mwakilishi wa Sage Publications, shirika kubwa la uchapishaji duniani, mwaka huu ni mara ya kwanza kwa shirika hilo kushiriki kwenye tamasha hilo. Bwana huyo alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, mchapishaji yeyote wa kimataifa hatapuuza soko kubwa la China. Alisema,

"Niliwahi kushiriki kwenye tamasha la vitabu huko London na Frankfurt, lakini naona tamasha hili ni bora zaidi. Nimekuja mwaka huu na nitakuja mwaka kesho, kwani tumepata wateja wengi hapa, nimewauzia wachapichaji wa China haki nyingi za kunakili. Soko la vitabu la China ni kubwa kabisa duniani, tunatumai tutakuwa na ushirikiano mkubwa zaidi na wachapishaji wa China."

Washiriki wa tamasha hilo hawakukosea kutambua soko la vitabu nchini China, hivi sasa watoto wa shuleni na wanafunzi katika vyuo vikuu wamefikia milioni 20, kufuatia maendeleo ya uchumi wa China na maisha yanavyokuwa bora, pesa zitakazotumika kununua vitabu hakika zitaongezeka. Biashara ya haki za kunakili za vitabu vya kufundishia pia ni sekta muhimu katika biashara ya haki ya kunakili kati ya China na nchi za nje. Bi. Regina Schinner wa kitengo cha haki ya kunakili katika shirika la uchapichaji la Harcoutr aliwaambia waandishi wa habari, alisema,

"Hii ni mara ya pili kwangu kushiriki kwenye tamasha hili, nimeleta vitabu aina mia sita, kati ya vitabu hivyo kuna vitabu vya watoto na pia kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Hili tamasha limeandaliwa vizuri sana, labda umuhimu wake sio mkubwa kuliko tamasha la Frankfurt lakini kabisa ni muhimu sana barani Asia, natumai nitapata ushirikiano wa uchapishaji wa vitabu vya kufundishia."

Kuanzia mwaka jana, tamasha la kimataifa la vitabu limeweka nchi mgeni mkuu. Mwaka huu ni "Mwaka wa China na Russia", nchi mgeni mkuu wa tamasha hilo ni Russia. Mashirika zaidi ya mia moja ya uchapishaji ya Russia yalishiriki kwenye tamasha hilo yakiwa na mada ya "pekua vitabu vipya na uifahamu Russia ya leo" kuonesha maendeleo ya uchapishaji wa Russia. Katika siku za tamasha hilo, wachapishaji wa China na Russia watafanya kongamano. Sambamba na hayo, waandishi watano wakubwa wa vitabu watakutana na wasomaji na kuzungumza nao ana kwa ana. Meneja mkuu wa Shirika la Uchapishaji wa Vitabu vya Kirusi, ambaye ni mara yake ya kwanza kushiriki kwenye tamasha hilo Bi. Svetlana Yu. Remizova alifurahia sana tamasha hilo, alisema,

"Tumeleta vitabu vingi vinavyofundisha Kirusi vikiwalenga watu wanaojifunza Kirusi katika ngazi tofauti. Kwa sasa sijaweza kusema maonesho yetu yatakuwaje lakini tamasha hili limetupatia fursa nzuri ya kutuwezesha kuwasiliana moja kwa moja na wasomaji wetu."

Tamasha hilo liligawanyika katika vipindi viwili, kipindi cha kwanza ni siku tatu za mwanzo, hiki ni kipindi cha maonesho kwa ajili ya watu wanaoshuhgulikia biashara ya vitabu na haki za kunakili, na katika siku ya mwisho ya tamasha hilo ilikuwa ni kipindi cha maonesho ya wazi kwa watu wote wakiwa ni pamoja na wakazi na wanafunzi. Katika siku za tamasha, lilifanyika kongamano la kimataifa la uchapishaji na wataalamu watajadili kuhusu "teknolojia mpya na mustakbali wa uchapishaji".

Msimamizi mwandamizi wa Chama cha Wachapishaji wa China ambaye pia ni mhariri mkuu wa Shirika la Uchapishaji la China Bw. Li Yan alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, baada ya miaka 20 kupita, sasa tamasha la kimataifa la vitabu mjini Beijing limekuwa tamasha muhimu katika bara la Asia na athari yake pia imekuwa kubwa duniani, hali hiyo imeleta manufaa kwa biashara ya haki ya kunakili ya China. Alisema,

"Kabla ya hapo, tuliingiza vitabu vingi na haki nyingi za kunakili kutoka nje, lakini sasa kiasi chetu cha kuuza vitabu na haki za kunakili kimeongezeka. Tuseme kwenye shirika letu kiasi cha kuuza vitabu na haki za kunakili kimekuwa kikubwa kuliko kiasi cha kuingiza. Katika mchakato wa kutoka nchi kubwa ya uchapishaji hadi nchi yenye nguvu kubwa ya uchapishaji, China imevutia wachapishaji wengi wa nchi za nje mwaka hadi mwaka. Tamasha hilo la kimataifa la uchapishaji mjini Beijing limekuwa na taathira kubwa duniani."

Bw. Li Yan aliongeza, kushiriki kwa wachapishaji wengi wa nchi za nje sio tu kumesukuma mbele maendeleo ya uchapishaji wa nchini China na nchi za nje, bali pia kumewaletea ufahamu mpya wachapishaji wa China ili wainue kiwango cha uchapishaji.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-18