Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-18 16:20:22    
Mtu mashuhuri katika China ya kale, Zheng Chenggong

cri

Zheng Chenggong ni shujaa wa taifa la China. Katika karne ya 17 aliongoza msafara wa merikebu kuvuka mlango wa bahari na kufika kisiwani Taiwan, aliwatimua wakoloni wa Uholanzi waliokalia huko kwa miaka 38 na kurudisha ardhi ya China.

Zheng Chenggong alizaliwa mwaka 1624 katika mji wa Nanan wa mkoa wa pwani Fujian, mashariki mwa China. Mama yake alikuwa Mjapani na baba yake Zheng Zhilong alikuwa kamanda wa jeshi katika sehemu fulani nchini China.

Zheng Chenggong ailiishi katika kipindi ambapo China ilikuwa katika historia ya mabadiliko ya utawala wa enzi na uvamizi wa wakoloni wa nchi za magharibi. Duniani nchi za viwanda za magharibi zilikuwa katika hali ya kugombea makoloni, na Uholanzi ilikikalia kisiwa cha Taiwan cha China. Wakoloni wa Uholanzi waliwanyanyasa na kuwanyonya vibaya wakazi wa kisiwani na mara kwa mara walifanya mashambulizi kwenye mikoa ya mwambao ya Fujian na Guangdong na waliwafanya wakazi wa huko wawe na chuki na hasira kubwa. Hapa nchini China, kabila la Waman lililoko kaskazini mwa China lilikuwa limetangaza utawala wa Enzi yake ya Qing na lilikuwa linaendelea kupambana na jeshi lililobaki la Enzi ya Ming iliyopinduliwa katika sehemu za kati na kusini za China. Kwa kuwa Enzi ya Ming ilikuwa ya kabila la Wahan, kwa hiyo vita dhidi ya askari wa Enzi ya Ming vilikuwa sio tu vita kati ya enzi mbili bali pia ni vita kati ya makabila mawili.

China ni nchi yenye makabila mengi, lakini katika historia ya umwinyi ya miaka zaidi ya elfu mbili kabila la Wahan lilitawala kwa muda mrefu sana, katika miaka ya mabadiliko ya enzi wasomi wa kabila la Wahan na watu wa tabaka la juu katika jamii walikuwa na chuki dhidi ya utawala wa kabila jingine, kwa hiyo walitokea watu wengi ambao hawakubali kushindwa na walikuwa tayari hata kufa. Katika karne ya 13 kabila la Wamongolia liliishambulia sehemu ya ndani ya China, pia walipingwa sana na wasomi. Hadi kufikia karne ya 17 kabila la Waman liliponyakua utawala na kuanzisha Enzi ya Qing wasomi walifanya vivyo hivyo.

Mwaka 1646 jeshi la Enzi ya Qing lilianza mashambulizi dhidi ya vikosi vya Enzi ya Ming vilivyotaka kurudisha utawala wa Enzi ya Ming kwenye sehemu za mwambao. Baba wa Zheng Chenggong alisalim amri kwa Enzi ya Qing, lakini mtoto wake Zheng Chenggong aliongoza askari wake kutoroka akiwa na nia ya kuupindua utawala wa Enzi ya Qing. Katika muda wa miaka kadhaa Zheng Chenggong alikuwa na askari zaidi ya laki moja na merikebu mia kadhaa, alikuwa amedhibiti sehemu za mwambao za kusini na kusini mashariki, alikuwa tayari kupambana na utawala wa Enzi ya Qing na kurudisha utawala wa Enzi ya Ming.

Ili kupata kituo cha jeshi lake ili aweze kupambana na utawala wa Enzi ya Qing kwa muda mrefu, Zheng Chenggong aliamua kurudisha kisiwa cha Taiwan. Alichagua askari hodari kwa vita na uwezo wa kuogelea kuunda kikosi muhimu cha mapambano. Mwaka 1661 Zheng Chenggong aliongoza askari elfu 25 kwa merikebu mia kadhaa kuelekea kwenye kisiwa hicho, kutokana na msaada wa wakazi wa kisiwa hicho askari hao walitumia muda wa saa mbili tu wakaingia ndani kabisa kisiwani, walijitokeza kwa ghafla mbele ya wakoloni wa Uholanzi, askari wa Uholanzi walishituka na kumaka, "Askari washuka mbinguni!"

Vita dhidi ya wakoloni wa Uholanzi viliungwa mkono sana na wakazi wa Taiwan, waliwakaribisha kwa chakula, na vijana wengi wa huko walijiunga na jeshi la Zheng Chenggong, hata baadhi ya watumwa weusi wa Uholanzi huko kisiwani pia walijiunga na jeshi hilo. Katika muda wa mwaka mmoja wa vita askari elfu mbili wa Uholanzi waliuawa. Tarehe mosi Februari mwaka 1662 jeshi la Uholanzi lilisalim amri, kisiwa kilichokaliwa na wakoloni wa Uholanzi kwa miaka 38 kilikuwa kimerudishwa nchini China.

Tokea hapo, Zheng Chenggong alianza kustawisha kisiwa hicho, kwa kuboresha mfumo wa utawala, kuanzisha shule, kustawisha kilimo na kuendeleza biashara kati yake na nchi za nje na kilikuwa na uhusiano wa kibiashara na nchi za Japan, Singapore, Vietnam na Indonesia. Kwa sababu watu wa mkoa wa Fujian na watu wa kisiwa cha Taiwan ni wa kabila moja, sera alizotunga Zheng Chenggong ziliungwa mkono na wakazi wa kisiwani, maendeleo ya kisiwani yalimpatia sifa na heshima kubwa miongoni mwa wakazi wa Taiwan.

Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba muda mfupi baada ya kukirudisha kisiwa cha Taiwan, Zheng Chenggong alifariki dunia katika kisiwa hicho, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 39 tu. Hivi sasa kwenye mlima wa Tizhanshan wilayani Taizhong kisiwani Taiwan bado kuna sanamu ya Zheng Chenggong, sanamu hiyo inaikabili bahari ikielekea China bara. Huku katika China bara mjini Xiamen mkoani Fujian mpaka sasa bado kuna mabaki ya vitu alivyoacha Zheng Chenggong alipowafundisha askari wake mazoezi ya kijeshi.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-18