Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-18 18:22:17    
Mkutano wa 14 wa wakuu wa wanachama wa harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote wafungwa

cri

Mkutano wa 14 wa harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote ulimalizika alfajiri ya tarehe 17 mwezi huu huko Havana, mji mkuu wa Cuba. Mkutano huo ulipitisha "Azimio kuhusu mwongozo, kanuni na umuhimu wa harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote katika hali mpya", "Waraka wa mwisho" na "Waraka kuhusu mbinu za kazi". Kwenye mkutano huo, washiriki walijitahidi kuipa uhai mpya harakati hiyo ya nchi zisizofungamana na upande wowote.

Moja ya mada muhimu za mkutano huo ni kujadili namna ya kufanya kazi muhimu kwa ajili ya harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote katika hali mpya na kuwa na hamasa mpya. Hadi hivi leo, harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote imekuwepo kwa miaka 45. Tangu harakati hiyo ianzishwe mwaka 1961, nchi wanachama zilifuata sera za kidiplomasia za kujiamulia mambo na zisizo za makundi, na zikawa nguvu ya tatu ya kisiasa duniani mbali na ncha mbili za Marekani na Urusi ya zamani. Baada ya kumalizika kwa vita baridi, umuhimu wa harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote ulianza kufifia.

Kwenye mkutano huo washiriki walisisitiza kuwa mwongozo na kanuni za harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote bado zina nguvu kubwa ya uhai. "Azimio kuhusu mwongozo, kanuni na umuhimu wa harakati ya kutofungamana na upande wowote katika hali mpya" lililopitishwa kwenye mkutano limefafanua zaidi kuhusu mwongozo, kanuni na umuhimu wa harakati hiyo katika hali mpya ya dunia. Azimio hilo linasistiza, katika hali mpya ya dunia, mwongozo wa harakati hiyo haujapitwa na wakati, na wala hautapitwa na wakati, hivyo umuhimu wa harakati ya kutofungamana na upande wowote unatakiwa kuimarishwa zaidi na wala siyo kudhoofishwa, na nchi wanachama za harakati hiyo zinatakiwa kutumia uwezo wake ambao bado haujatumika kwa mbinu ya kushikamana, kuwa na ushirikiano na kufanya mageuzi ili kuifanya harakati hiyo iwe na nguvu kubwa zaidi.

Washiriki pia walikuwa na majadiliano kuhusu masuala nyeti ya duniani na kulinda haki za nchi zinazoendelea. Taarifa iliyopitishwa mkutanoni inaunga mkono Iran kutumia nishati ya nyukilia kwa amani, na pia imeeleza matarajio yake kuwa suala la nyukilia la Iran litatatuliwa kwa njia ya kidiplomasia. Mbali na hayo, mkutano huo pia ulieleza uungaji mkono wake kwa jitihada za haki za watu wa Palestina.

"Waraka wa mwisho" umeonesha msimamo wa harakati ya kutofungamana na upande wowote kuhusu masuala muhimu kadha wa kadha ya kimataifa. Waraka huo umeilaani Israel kwa kushambulia sehemu ya kusini mwa Lebanon, kuunga mkono serikali na watu wa Lebanon na kuitaka Israel itoe fidia kwa hasara iliyosababishwa na mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya serikali na watu wa Lebanon; Kuunga mkono watu wa Cuba na kutaka Marekani iondoe vikwazo ilivyoweka dhidi ya uchumi wa Cuba.

Aidha, mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote unazingatia sana suala la ugaidi. "Waraka wa mwisho" unalaani aina zote za ugaidi, hususan mashambulizi ya kisilaha dhidi ya watu wa kawaida. Kwenye mkutano wa maofisa wa ngazi ya juu na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje uliofanyika kabla ya mkutano wa wakuu wa nchi, washiriki wengi walitaka kuthibitisha wazi maana ya "ugaidi", na waliikosoa Marekani kutumia vigezo viwili katika mapambano na ugaidi. "Waraka wa mwisho" unasema nchi wanachama wa harakati ya kutofungamana na upande wowote zinapinga kithabiti nchi fulani kuchukulia baadhi ya nchi kuwa ni 'kiini cha uovu' kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Jambo lingine muhimu ni kuwa mkutano wa wakuu wa nchi wa mwaka huu ulitoa nafasi ya mazungumzo ya amani kati ya India na Pakistan. Katika muda wa kufanyika kwa mkutano huo, rais Pervez Musharraf wa Pakistan alikuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa India Bw. Mannohan Singh, taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo ya pande hizo mbili inasema, nchi hizi mbili zitaanzisha upya mazungumzo ya amani kuhusu utatuzi wa suala la Kashmir. Hayo ni mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu kati ya viongozi wa nchi hizo mbili baada ya mfululizo wa milipuko iliyotokea tarehe 11 mwezi Julai huko Bombay, India. Rais Musharraf alisema mazungumzo hayo yamepata mafanikio ya amani.

Mwaka huu miaka 45 imetimia tangu harakati ya kutofungamana na upande wowote ianzishwe, hivyo mkutano huo ulifuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Wakuu wa nchi viongozi au wawakilishi wa serikali za nchi 115 pamoja na wawakilishi wa nchi 15 za wachunguzi, nchi 31 zilizoalikwa mahsusi na jumuiya 23 za kimataifa zilishiriki kwenye mkutano huo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-18