Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-19 14:46:55    
Barua 0917

cri
 Msikilizaji wetu Edwin Mashola wa Lake sekondari, Mwanza Tanzania katika barua yake anatoa salamu nyingi kutoka nchi yenye amani na utulivu Tanzania, pia anatoa pole kwa wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili wa radio China Kimataifa kwa kazi kubwa ya kuwafikishia matangazo wasikilizaji wake kupitia idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

Anatushukuru kwa juhudi za kuendeleza lugha ya Kiswahili ambayo sasa ni moja kati ya lugha kubwa za kimataifa, anatoa shukrani za dhati kwa kuwafikishia habari motomoto, matukio yanayojiri, michezo na burudani na pia anatoa shukrani kwa kuanzisha kituo cha matangazo cha FM jijini Nairobi. Vilevile Bw Mshola anatoa ombi ili kuyawezesha matangazo ya CRI yaweze kurushwa hewani kupitia masafa ya FM nchini Tanzania.

Anasema pia alitaka kutuambia kuwa alisoma habari njema ya Kiswahili rais wa China Hu Jintao alipotembelea Marekani alionana na mkurugenzi na mmiliki wa kampuni ya Microsoft Bw Bill Gates na kupata mlo wa jioni. Waliongea mambo mengi, mojawapo ni mpango wa kutengeneza programu za Microsoft, anasema hakuna kinachompa raha kama kutembelea tovuti ya Radio China kimataifa. Anatoa wito kwa Radio China kimataifa kuendelea kumpatia yeye na wasikilizaji wengine habari motomoto kupitia mtandao wenu, kwani una habari za kuvutia. Anasema kuwa anasubiri siku moja kusikia matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kupitia masafa ya FM ya radio Tanzania na sauti ya Radio Zanzibar, atafurahi sana matangazo haya yakiwa na usikivu mkubwa zaidi.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Edwin Mashola kwa barua yake ambayo ametueleza usikilizaji wake wa matangazo ya Radio China na kimataifa na kuvutiwa na tovuti yetu ya Kiswahili kwenye internet, tunaahidi kuwa tutaendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu na wasomaji wetu.

Msikilizaji wetu Zaharani Mohamedal-Rujabi wa S.L.P 868 Ruwi, Oman anapenda kujitambulisha kuwa yeye ni msikilizaji wa Radio China Kimataifa tokea mwaka 1966 yaani miaka 40 iliyopita enzi za Hayati Mao ZeDong, wakati huyo yeye alikuwa anaishi nchini Tanzania, alikuwa bado hajaanza kuishi nchini Oman. Wakati ule yeye alikuwa anawasiliana sana na Radio Peking na alikuwa akipata zawadi nyingi sana kama vile kalenda nzuri sana, kitabu kidogo chenye rangi nyekundu kiitwacho "Quotations of Mao Tse Tung" na beji nyekundu ya Mao ya kuvaa kifuani. Anasema bado anapenda kuwasiliana na idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa na anapenda kuitembelea nchi nzuri sana ya China. Mwisho anashukuru kwa matangazo mazuri ya Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Zaharani Mohamedal-Rujabi ambaye amekuwa akisikiliza matangazo yetu tangu zamani sana, amesikiliza matangazo yetu na kuwa na mawasiliano barabara na Radio China kimataifa, barua yake imetukumbusha mambo yaliyopita, tunaona urafiki kati yetu ni wa kudumu. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo yake ili kutusaidia kuboresha vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Sheale Charles wa S.l.P 548 Bwera-Kasere Uganda anatoa salamu nyingi kwa wafanyakazi na wasikilizaji wote wa Radio china Kimataifa. Kwanza anashukuru kwa barua zote na pia zawadi alizopata kutoka kwa Radio China kimataifa, na pia angeomba Radio China Kimataifa imtafutie marafiki wa kalamu, marafiki hao wawe wanafunzi au wafanyakazi, pia atafurahi sana kama Radio China kimataifa itamtumia CD za nyimbo, VCD au DVD za michezo ya kichina.

Wasikilizaji wetu Ishengoma Ismail na Kulwa Mwendapole wa S.L.P 152 Tabora, Tanzania wametuletea barua wakitoa salamu zao za dhati kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, pia wanatoa pongezi kwa wasikilizaji wote wa Radio China Kimataifa kwa kuonesha ushirikiano wao katika ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya Radio China Kimataifa, kwani radio China inawajenga sana.

Ndugu Ishengoma Mwendapole anaiomba Radio China Kimataifa iongeze muda wake wa matangazo hasa katika kipindi cha salamu zenu, pia anaomba uboreshaji zaidi wa mitambo ya kurusha matangazo kwani bado kuna baadhi ya sehemu kama vile mkoani Tabora, wasikilizaji wanapata matangazo kwa shida.

Wasikilizaji wetu hawa pia wanatoa shukrani kwa Radio China Kimataifa kutangaza matokeo yenye haki kwa washindi wa chemsha bongo iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana. Wanawapa hongera wasikilizaji wote walioibuka washindi katika chemsha bongo hiyo, na wale walioshindwa wanawapa pole na wanawaambia wasikate tamaa kwani bado kuna mashindano mengine.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Sharif anayetunziwa barua zake na Jendeka Goldah wa S.L.P 172 Bungoma, Kenya anatoa shukrani pamoja na Pongezi kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa hapa Beijing, hasa anatoa pongezi kwa vipindi ambavyo vinafundisha na kuelimisha na ambavyo vinamsaidia yeye na wasikilizaji wengine kujenga ufahamu bora ambao umewawezesha kuanzisha miradi kadha wa kadha mjini Bungoma.

Bwana Mutanda pia anazungumzia ziara ya rais Hu Jintao ambayo aliifanya nchini Kenya, anasema anaishukuru sana Radio China kimataifa kwa kuwapatia habari kabla ya ziara hiyo ambapo wasikilizaji wengi wao wasio na huduma ya umeme, walijiandaa kwa kununua betri na wale wanaotumia jenereta walinunua petroli na dizeli ya kutosha ili waweze kupata habari za ziara hiyo na kutizama ziara hiyo kupitia runinga zao bila matatizo.

Bwana Mutanda anasema anafahamu kuwa China ni nchi kubwa na iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo katika nyanja zote, ikiwemo siasa, uchumi, sayansi na teknolojia, na ni nchi inayodumisha uhuru na amani nchini mwake na inatafuta amani ya dunia nzima.

Kuanzishwa kwa Radio China Kimataifa ilikuwa ni changamoto kubwa kwa china, kwani sasa China imeweza kutambulika duniani kote na imeweza kutoa ajira kwa watu mbalimbali duniani, kwani sasa Radio China Kimataifa inatangaza kwa lugha 43 zikiwemo 39 za kigeni, hivyo ni wazi kuwa watu kutoka sehemu mbalimbali duniani wamepata ajira kutokana na matangazo hayo. Mwisho anampongeza rais Hu Jintao kwa kuitembelea Kenya na anaishukuru serikali ya watu wa China kupitia Radio China Kimataifa kwa kuanzisha kituo cha FM Jijini Nairobi nchini Kenya.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Mutanda Ayub Sharif kwa barua yake, kweli kila mara anatuletea barua na kutuelezea mambo mbalimbali ya kufurahisha na kututia moyo.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-19