Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-19 20:08:55    
Nchi zinazoendelea kuwa na sauti kubwa katika shirika la fedha duniani

cri

Nchi wanachama 184 wa shirika la Fedha duniani tarehe 18 usiku mwezi huu zilipiga kura huko Singapore kuzipa China, Korea ya Kusini, México, na Uturuki haki kubwa zaidi katika upigaji kura. Mageuzi hayo yatazisaidia nchi za Asia na nchi zinazoendelea kutoa mchango muhimu zaidi katika shirika hilo.

Habari zinasema 90.6% ya nchi wanachama zilipiga kura za ndiyo. Hadi hivi sasa China imechukua nafasi ya 3.72% ya haki ya upigaji kura kutoka 2.98% ya hapo zamani katika shirika hilo. Haki za upigaji kura za Korea ya Kusini, México na Uturuki pia zimeongezeka hadi 1.35%, 1.45% na 0.55%, hayo ni mageuzi makubwa zaidi ya shirika la utoaji misaada ya fedha duniani katika miaka 60 iliyopita.

Shirika la fedha duniani lilianzishwa na serikali za nchi nyingi duniani tarehe 27, mwezi Desemba mwaka 1945, tokea muda mrefu uliopita haki nyingi za upigaji kura za shirika hilo zilikuwa mikononi mwa nchi zilizoendelea, Marekani, Ulaya, Japan na Canada zina 63% ya haki za upigaji kura, hivyo zina nafasi kubwa kabisa ya kuamua sera muhimu za shirika hilo. Lakini Asia, ambayo inachukua 25% ya jumla ya pato la dunia, ina 10% tu ya haki ya upigaji kura. Ingawa pato la China katika mwaka uliopita lilichukua nafasi ya 4 duniani, ambalo ni mara 2 za jumla ya mapato ya Ubelgiji na Uholanzi, lakini haki za upigaji kura za nchi mbili za Ubelgiji na Uholanzi ni mara 1.5 kuliko ile ya China.

Hali hiyo inaonesha kuwa ugawaji wa haki za upigaji kura wa shirika hilo hauwezi kuonesha vilivyo hali halisi ya uchumi wa dunia ya hivi sasa. Mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha duniani Bw. Rodrigo Rato amesema, sasa kuna haja kwa shirika hilo kufanya marekebisho kuhusu haki za upigaji kura. Safari hii mkutano wa Singapore wa shirika la utoaji misaada ya fedha duniani ulifanya uamuzi wa kuongeza haki za upigaji kura za nchi 4 za China, Korea ya Kusini, México na Uturuki, kitendo ambacho kinaendana na hali ya dunia. Bila shaka ongezeko la haki za upigaji kura za nchi 4 za China, Korea ya kusini, México na Uturuki litafanya nchi hizo kuwa na sauti kubwa zaidi katika shirika la fedha duniani na kuweza kupata misaada mingi zaidi ya fedha kutoka kwenye shirika hilo.

Kwanza kanuni za shirika hilo zinasema, kwa kufuata mpango wa utoaji mikopo ya akiba na mikopo ya muda wa wastani, kila nchi mwanachama inaweza kupata mikopo isiyozidi 300% ya mgao wake. Kuwa na mgao mkubwa zaidi kunamaanisha nchi inaweza kupata mikopo mingi zaidi ya shirika hilo. Pili, nchi hizo zimekuwa na haki nyingi zaidi za upigaji kura na kuwa na sauti kubwa zaidi katika kuamua sera za shirika hilo na kufanya mwongozo wa shirika la utoaji misaada ya fedha duniani kuweza kutekelezwa vizuri zaidi na kwa ukamilifu zaidi.

Kwa China ambayo hivi sasa bado ni nchi inayoendelea, ina maslahi mengi ya pamoja na nchi nyingine zinazoendelea, endapo China itashirikiana na nchi nyingine zinazoendelea katika upigaji kura, zinaweza kufanya kazi muhimu zaidi. China inaweza kutumia ongezeko la haki ya upigaji kura kuhimiza utaratibu wa utungaji sera wa shirika hilo kuwa mwafaka zaidi kati ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea.

Ni dhahiri kuwa mageuzi yaliyofanyika kuhusu haki za upigaji kura za shirika la fedha duniani bado hayatoshi kabisa, nchi zilizoendelea, hususan Marekani bado inamiliki hali bora sana ya kuongoza. Hivyo mageuzi lazima yaendelezwe katika siku za baadaye. Kutokana na madai ya nchi zinazoendelea shirika la fedha duniani limebuni mpango wa mageuzi. Watu wanatarajia kuwa shirika la utoaji misaada ya fedha duniani litapiga hatua kubwa zaidi katika mageuzi ya haki za upigaji kura kwa haraka zaidi ili kuendana na mabadiliko ya muundo wa uchumi wa dunia.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-19