Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-20 20:57:16    
Mapinduzi ya kijeshi yatokea nchini Thailand

cri

Maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la Thailand wamevunja baraza la mawaziri lililoongozwa na waziri mkuu Bw. Thaksin Shinawatra usiku wa tarehe 19, na kuifanya nchi hiyo iwe chini ya utawala wa kamati moja ya kijeshi iitwayo Kamati ya usimamizi na mageuzi ya taifa. Hii ni mara ya kwanza kwa mapinduzi ya kijeshi kutokea nchini Thailand katika miaka 15 iliyopita.

Tarehe 19 msemaji wa wanajeshi waliofanya mapinduzi akiwahutubia wananchi kwa njia ya televisheni na radio, alisema "Kamati ya usimamizi na mageuzi ya taifa inaundwa na viongozi wa jeshi na polisi. Ili kulinda sheria na utulivu wa taifa, tumeshadhibiti mji wa Bangkok na sehemu zilizoko karibu. Katika mchakato huo haukutokea upinzani. Tunawataka wananchi wote wa Thailand wawe na uelewa kuhusu tukio hilo, tunawaomba radhi kuhusu matatizo mbalimbali yaliyosababishwa na tukio hilo."

Msemaji huyo pia alitangaza kubatilisha katiba, kuvunja mabaraza mawili ya bunge na mahakama ya katiba. Akifafanua sababu za kufanya mapinduzi, alisema hali ya machafuko imetokea katika mambo ya siasa nchini Thailand, ambapo matatizo mbalimbali yameshindwa kutatuliwa, hivyo jeshi la Thailand na kikosi cha polisi wameamua kuchukua madaraka.

Inasemekana kuwa mapinduzi hayo ya kijeshi yaliongozwa na kamanda mkuu wa jeshi la nchi kavu la Thailand jenerali Sonthi Boonyaratkalin. Baada ya mapinduzi hayo waziri mkuu wa nchi hiyo Bw. Thaksin Shinawatra aliyeko Marekani kuhudhuria mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, alitangaza hali ya hatari nchini kote kwa kupitia kituo cha namba 9 cha televisheni kinachodhibitiwa na serikali yake. Msemaji wa serikali yake aliyefuatana na Bw. Shinawatra kwenye mkutano huo Bw. Surapong Suebwaonglee aliwaambia waandishi wa habari kuwa, "Mapinduzi hayo ni jaribio la baadhi ya maafisa wa kijeshi tu, tunaamini kuwa hawafanikiwa. Demokrasia imeingia katika kipindi cha kupevuka nchini Thailand, ambapo hakuna mwananchi anayekubali mapinduzi ya kijeshi."

Alfajiri wa tarehe 20 wanajeshi waliofanya mapinduzi wametangaza kumteua Bw. Sonthi Boonyaratkalin kuwa waziri mkuu wa muda. Vile vile waliondoa amri ya hali ya hatari iliyowekwa na waziri mkuu aliyepinduliwa Bw. Thaksin hapo awali, kupiga marufuku kutembea katika mji mkuu Bangkok, na kuwataka wananchi wa nchi hiyo wawe watulivu.

Je, watu wa Thailand wana maoni gani kuhusu tukio hilo la mapinduzi? Mkazi mmoja wa Bangkok aliyeshtushwa na kutokea kwa ghafla kwa askari barabarani, alisema "Sijui ni kwanini askari wengi namna hii wamejitokeza na wala sijui wanavyofanya nini."

Mtalii mmoja wa kigeni alieleza wasiwasi wake akisema, "Natarajia kuondoka nchi hiyo, kama uwanja wa ndege utafungwa itakuwa tatizo kubwa."

Na vyama vya upinzani nchini Thailand vinaonaje kuhusu mapinduzi hayo? Kiongozi wa Chama cha muungano wa umma wa kidemokrasia Bw. Sondhi Limthongkul alisema "Kutokana na amri ya kupiga marufuku watu kutembea, maandamano dhidi ya Bw. Thaksin yamefutwa, lakini endapo amri hiyo itaondolewa tutaendelea na maandamano hayo."

Mapinduzi hayo ya kijeshi yanafuatiliwa na jumuiya ya kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan tarehe 19 alitoa wito kuwatawa watu wa Thailand wawe watulivu, na kurejesha kwa haraka utaratibu katika nchi yao. Marekani imeeleza kuwataka watu wa Thailand watatue migongano ya kisiasa kwa njia ya amani, na kwa kufuatia kanuni za kidemokrasia na sheria.

Hivi sasa wanajeshi waliofanya mapinduzi wamesema Bw. Thaksin aliyeko mjini New York amekubali kujiuzulu. Lakini habari hiyo bado haijathibitishwa na Bw. Thaksin mwenyewe. Sasa bado kuna utatanishi kuhusu hali nchini Thailand na athari ya mapinduzi hayo ya kijeshi kwa mambo ya kisiasa ya nchi hiyo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-20