Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-22 16:38:42    
Barabara kati ya mji wa Accra na Kumasi

cri

Barabara yenye urefu wa kilomita 250 kati ya mji wa Accra na Kumasi ni barabara kuu inayounganisha sehemu za kusini na za kaskazini nchini Ghana, na magari mengi zaidi yanapita kwenye njia hiyo. Kumasi ni mji mkubwa wa pili kwenye sehemu ya kaskazini mwa Ghana. Hivyo barabara hii sio kama tu ina umuhimu wa kimkakati katika kuhimiza maendeleo ya uchumi wa Ghana, bali pia ni barabara muhimu ya uchukuzi na usafirishaji kwa nchi jirani za Ghana zikiwemo Mali, Burkina Faso na Nigeria.

Zamani barabara hiyo ilikuwa na njia mbili tu. Ilikuwa mbovu yenye matuta mengi kutokana na kutokarabatiwa kwa miaka mingi, hasa sehemu kati ya Avanko na Nsawamu kwenye barabara hiyo. Ofisa mmoja wa ofisi ya barabara ya Ghana alieleza kuwa, zamani magari yalipofika kwenye sehemu hiyo yaliweza kwenda polepole, na ajali na misongamano ya magari barabarani zilitokea mara kwa mara. Hali ambayo ilikuwa ni tatizo kubwa kwa maendeleo ya uchumi, lakini hali hiyo sasa imebadilika. Baada ya ukarabati wa barabara hiyo uliofanywa kwa msaada wa serikali ya China, barabara hiyo ina sura mpya, na ilijengwa kuwa ya ngazi ya kwanza yenye njia nne. Mabadiliko hayo yamepunguza kwa kiasi kikubwa muda wa magari kusafiri kati ya Accra na Kumasi. Kuboreshwa kwa barabara hiyo pia kutahimiza maendeleo ya biashara na makazi, na kutoa fursa nyingi kwa wenyeji huko na kuboresha maisha yao.

Tarehe 19 mwezi Juni mwaka 2006, waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao aliyefanya ziara nchini Ghana, yeye pamoja na rais Kuffour wa Ghana walishiriki kwenye sherehe ya ufunguzi wa barabara hiyo. Bw. Wen Jiabao alisifu barabara hiyo kama ishara nyingine ya ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Ghana, na daraja jipya la urafiki wa kijadi kati ya nchi hizi mbili. Rais Kuffour alisifu barabara hiyo akisema itatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa Ghana na nchi jirani za sehemu za Afrika ya magharibi. Rais Kuffor aliongeza kuwa anapaswa kuwaonya madereva wasipatwe na usingizi wanapoendesha magari kwenye barabara hii, kwa kuwa barabara hiyo imebadilika kuwa nzuri sana.

Watu wa China na Ghana wana urafiki wa jadi, na siku zote wanaungana mkono na kusaidiana. Ghana ni nchi ya pili kusini mwa Sahara iliyoanzisha mapema uhusiano wa kibalozi na China mpya. Kwa kushikilia kanuni ya kunufaishana na kutoingiliana mambo ya ndani, China toka mwanzoni ilitoa misaada ya dhati kwa ukombozi wa taifa la Ghana na maendeleo yake. Waziri mkuu wa zamani wa China Bw. Chou Enlai mwaka 1964 alitembelea nchini Ghana. Ziara hiyo ilikuwa ni jambo muhimu katika historia ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili.

Katika miaka mingi iliyopita Ghana inaiunga mkono kithabiti China katika masuala muhimu yakiwemo mambo ya haki za binadamu, suala la Taiwan na mengineyo. Mwaka 1971 Umoja wa Mataifa uliporejesha kiti kwa Jamhuri ya Watu wa China katika umoja huo, Ghana ilipiga kura moja muhimu ya kukubali. Katika miaka karibu 50 iliyopita, China na Ghana zilifanya ushirikiano mzuri katika nyanja za siasa, uchumi, biashara, afya, elimu na nyinginezo. Mradi wa kukarabati barabara kati ya Accra na Kumasi ni uthibitisho mwingine kwa ushirikiano huo.

Kutokana na juhudi kubwa za miaka mingi, Ghana imefutwa kutoka kwenye orodha ya nchi ambazo ziko nyuma kabisa kichumi duniani. Sasa nchi hiyo iko kwenye kipindi muhimu cha kuendelea, na inajitahidi kuvutia uwekezaji ili kuendeleza uchumi, kuboresha maisha ya wananchi na kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa. Hivi sasa makampuni mengi ya China yanashiriki kwenye kazi za ujenzi nchini Ghana. Makampuni hayo yanaisaidia nchi hiyo kujenga jumba la maonyesho, hospitali, barabara na miradi mingine.

China hivi sasa ina miradi mingi ya misaada ya ujenzi katika nchi mbalimbali barani Afrika. Umaalum wa pamoja wa miradi hiyo ni kwamba China inatilia maanani kusaidia nchi za Afrika kujiongezea uwezo wa kuendelea. Katika miradi hiyo, mbali na kutoa misaada ya fedha, China inatoa ushirikiano wa kiuchumi na wa kiteknolojia, na kutilia maanani sana sifa, faida, kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha ya watu.

Ili kutumia vizuri zaidi fedha katika mradi huu, serikali ya China ilichagua kwa makini kampuni moja nzuri katika makampuni mengi nchini China. Mradi huo ulianza rasmi mwezi Mei mwaka 2004, na kumalizika mwezi June mwaka huu. Katika muda wa miaka miwili, kampuni hiyo iliwachagua wataalam hodari, na kutunga mipango ya ujenzi kwa makini. Mwishoni si kama tu kampuni hiyo ya China ilimaliza ujenzi wa mradi huo mapema kuliko ilivyopangwa, bali pia iliufanya mradi uwe na sifa ya juu.

Walipokuwa wanaendelea na ujenzi wa mradi huo wafanyakazi wa China walitilia maanani sana kuhifadhi mazingira. Ili kupunguza athari ya ujenzi wa barabara kwa mazingira, na kuzuia mmomonyoko wa udongo, walipanda nyasi na miti kando na katikati ya barabara.

Methali ya kichina inasema ni vizuri zaidi kuwafundisha watu kuvua samaki kuliko kuwapa samaki. China inajenga miradi katika bara la Afrika, inatilia maanani sana kuwafundisha wafanyakazi wenyeji. Katika ujenzi wa mradi wa barabara kati ya Accra na Kumasi, kampuni ya China iliwapeleka wataalam wachache, na wafanyakazi wengine wengi waliajiriwa nchini Ghana. Kuanzia kipindi cha kutunga mpango, wafanyakazi wa nchi hizi mbili walishirikiana vizuri na kutatua matatizo kwa pamoja. Wafanyakazi wa Ghana walipata mafunzo mazuri sana hata baada ya kukabidhiwa barabara hii, wanaweza kuitunza vizuri.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-22