Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-25 14:58:19    
Mwongoza filamu Jia Zhangke

cri

Katika Tamasha la 63 la Filamu la Kimataifa lililofungwa hivi karibuni mjini Venice, mwongoza filamu kijana Jia Zhangke alipata "tuzo ya simba" kwa filamu yake "Raia Wema katika Magenge Matatu ya Mto Changjiang", na kuwa mwongoza filamu wa tano wa China aliyepata tuzo hiyo na pia ni mwongoza filamu wa pili aliyepata tuzo hiyo baada ya mwongoza filamu mashuhuri Zhang Yimou kupata tuzo hiyo kwa filamu yake inayoitwa "Asiachwe Hata Mtoto Mmoja Kukatisha Masomo" mwaka 1999.

Filamu inayoitwa "Raia Wema katika Magenge Matatu ya Mto Changjiang" ni filamu yenye hadithi mbili, hadithi moja inaeleza kwamba katika mji mdogo katika maeneo ya Magenge Matatu ya Mto Changjiang wachumba wawili toka walipofahamiana, kuelewana na mwishowe kuoana, hadithi nyingine pia inaeleza wachumba wawili, lakini waliachana kutoka na kufahamiana sana. Wachumba hao wote wamepata ufahamu wao kuhusu maisha yao. Mwenyekiti wa kundi la waamuzi wa tamasha hilo, mwigizaji mashuhuri wa Ufaransa Bw. Catherine Deneuve kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya sherehe ya kutoa tuzo alisema, "Sisi waamuzi tulishangazwa baada ya kutazama filamu hiyo, picha za mazingira ni nzuri, hadithi ni ya kuvutia, hakika filamu hiyo siyo ya kawaida."

Jia Zhangke ana umri wa miaka 36, alizaliwa wilayani Fenyang mkoani Shanxi. Baba yake ni mwalimu wa lugha na fasihi ya Kichina na mama yake ni muuza duka. Alipokuwa katika shule ya sekondari ya chini Jia Zhangke hakufikiri mambo mengine zaidi ya kusoma, kila siku alikuwa anakwenda shuleni na kurudi nyumbani na kuandaa mtihani. Lakini alipokuwa katika sekondari ya juu alibadilika kuwa mtukutu. Mwanzoni alikuwa anapenda sana muziki, kisha akawa mpenda break dance, mara kwa mara alikuwa anacheza pamoja na wanafunzi wenzake zaidi ya kumi. Mwaka 1993, Jia Zhangke alijiunga na Chuo Kikuu cha Filamu cha Beijing, baada ya miaka mitatu akawa mtengenezaji wa filamu. Hadi sasa ametengeneza filamu tano za hadithi, kati ya filamu hizo, filamu inayoitwa "Jukwaa la Kituo cha Garimoshi" iliyopigwa mwaka 2000 na filamu inayoitwa "Dunia" iliyopigwa mwaka 2004 na filamu iliyopigwa mwaka huu ya "Raia Wema katika Magenge Matatu ya Mto Changjiang" zilishiriki kwenye Tamasha la Filamu la Kimataifa Mjini Venice.

Jia Zhangke aliyetoka kwenye mji mdogo ulio mbali na kuja kwenye mji mkubwa Beijing hakuhisi vizuri. Katika mwaka wa kwanza karibu nusu mwaka alikaa makwao au mahali pengine, muda wake wa kukaa mjini Beijing ulikuwa mdogo sana kwa sababu katika mji huu mkubwa aliona yeye ni kama mtu wa pembeni. Filamu yake inayoitwa "Dunia" ni filamu inayomwelezea kibarua mmoja aliyetoka vijijini kwenda kufanya kazi katika mji mkubwa alivyoishi kwa kuwa na wasiwasi na upweke, furaha na matumaini bila kujua hatima yake iweje. Jia Zhaengke aliona yeye alikuwa mtu wa namna hiyo. Alisema,

"Tokea Beijing ipate nafasi ya kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki mwaka 2008 watu kutoka sehemu mbalimbali nchini China wanamiminikia Beijing, na mimi ni mmojawapo. Filamu yangu ya Dunia inaeleza watu hao jinsi wanavyokabiliwa na matatizo, shinikizo, mahangaiko na kuwa na matumaini."

Filamu za Jia Zhangke huwa zinaonesha maisha halisi, anatumia watu wa kawaida kuigiza badala ya waigizaji halisi, na kuonesha maisha halisi ya makabwera katika jamii. Filamu yake ya "Kijana Xiao Wu" inaeleza maisha halisi ya kijana mmoja aliyekuwa nyumbani kwao. Filamu hiyo ilipata tuzo katika Tamasha la 48 la Kimataifa la Filamu mjini Berlin. Makala kwenye jarida la filamu la Ufaransa ilisema, "Filamu hiyo iko tofauti naq upigaji filamu wa kawaida wa China, ni filamu inayoashiria kufufuka na kuimarika kwa filamu za China." Jia Zhangke alisema,

"Napenda kuonesha maisha moja kwa moja, na maisha halisi yanahitaji kuoneshwa na watu wenye maisha yenyewe."

Jia Zhangke pamoja na waongoza filamu wengine wenye umri wa miaka thelathini hivi wanaitwa "waongoza filamu wa kizazi cha sita". Watu hao walipoanza kutengenza filamu ilikuwa ni miaka ambapo filamu za China zilikuwa zimeanza kuingia kwenye soko huria. Watu hao kwa upande mmoja wanashikilia msimamo wao kuhusu namna ya kutengeneza filamu, kwa upande mwingine wanakabiliwa na tatizo la kupata mapato ya tikti za filamu zao. Jia Zhangke anashikilia msimamo wake wa kuonesha maisha halisi ya akina yakhe.

Jia Zhangke alieleza sifa ya waongoza filamu wa awamu ya sita. Alisema,

"Filamu zilizotengenezwa na waongoza filamu wa awamu ya sita huonesha hisia za mtu binafsi jinsi anavyofahamu dunia, na anavyopima watu. Naona kuwa haja ya kuonesha mambo au kumbukumbu za mtu mmoja mmoja nchini China, naona sanaa kama hiyo ni ya thamani kubwa."

Jia Zhangke alipotengeneza filamu inayoitwa "Raia Wema katika Magenge Matatu ya Mto Changjiang" amefahamu kwamba pengine sanaa haitasaidia chochote, lakini inaweza kuwapatia heshima watu waliopuuzwa."

Idhaa ya kiswahili 2006-09-25