Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-26 19:33:53    
Barua 0924

cri

Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.B 1067 Kahama, Shinyanga nchini Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, asubuhi na mapema ya tarehe 3 mwezi wa 12 mwaka 2006 itakuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 65 tangu Radio China Kimataifa ianzishwe. Hana shaka kuwa wafanyakazi, wageni waalikwa na wasikilizaji wa Radio China kimataifa popote duniani watajumuika katika sherehe hizo. Anawapongeza wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa kwa maadhimisho hayo ya miaka 65 ya CRI.

Pia Bwana Kumalija anaishukuru sana Radio China Kimataifa kwa kuwapa habari zinazotokea duniani katika nyanja mbalimbali za siasa, utamaduni, uchumi, michezo na burudani. Anasema Radio China Kimataifa inaimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya China na Nchi nyingine. Vile vile anaupongeza ushirikiano wa wafanyakazi wa Radio China kimataifa ambao hauna ubaguzi wa rangi, dini wala kabila, na hiyo ndiyo siri ya kufanikisha vipindi bora vinavyokidhi matakwa ya wasikilizaji wa Radio China Kimataifa. Mwisho anaipongeza Hongera Radio China Kimataifa kwa kuadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwake.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija kwa barua yake ya kupongeza miaka 65 ya Radio China kimataifa, kweli siku hizi Radio China kimataifa inafanya maandalizi ya kuadhimisha siku hiyo, hakika siku za baadaye tutawaelezea zaidi kuhusu shughuli hizo za maadhimisho, ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu wataendelea kutuunga mkono ili Radio China kimataifa ipige hatua kubwa katika matangazo yake ya kila siku pamoja na shughuli nyingine mbalimbali.

Msikilizaji wetu Kisandu Kusolwa wa S.L.B 430, Bongo Mela, Tabora nchini Tanzania ametuletea barua akianza kwa salamu kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili wa Radio China kimataifa, anasema anashukuru kwa zawadi alizozipata tarehe 16 mwezi wa 6 mwaka 2006 kutoka kwa Radio China Kimataifa, na amefurahi sana. Msikilizaji wetu huyo anaendelea kusema kuwa bado anayapata matangazo ya Radio China kimataifa bila wasiwasi wowote, na mwisho anawatakia watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kazi njema, na maisha mema na marefu.

Tunamshukuru Bwana Kisandu Kusolwa kwa barua yake, tunapenda kumwambia kuwa amepewa zawadi kutokana na juhudi zake za kuunga mkono kazi yetu, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo yake.

Msikilizaji wetu Andrew Pilla Opokwo wa Bunyore nchini Kenya ametuletea barua akiwasalimu wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, anasema yeye ni mzima na anaendelea kuvitegea sikio kila siku vipindi motomoto vya idhaa ya Kiswahili ya radio China kimataifa. Msikilizaji wetu huyu anaunga mkono mpangilio na utaratibu wa vipindi vyetu na anafurahi kwa kuwa wasikilizaji wengi wanapenda kuisikiliza idhaa ya Kiswahili ya radio China kimataifa.

Bwana Opokwo anatoa pongezi kwa Radio China Kimataifa kwa kuhudumia vizuri wasikilizaji wake kwa kuwaandikia barua na kuwajulisha hali ya maendeleo ya Radio China Kimataifa, pia anaipongeza sana Radio China kimataifa kwa kuwapa kidadisi wasikilizaji wake ili waweze kutoa maoni na mapendekezo yao.

Pia anasema anaomba kutumiwa jarida dogo la daraja la urafiki la mwaka 2004.Pia atafurahi sana kama atatumiwa fulana ya Radio China Kimataifa pamoja na kadi za salamu. Mwisho anawatakia wafanyakazi wote na wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kazi njema na waweze kufanikiwa katika malengo yote ya mwaka huu wa 2006.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayubu Shariff wa S.L.B 172 Bungoma, nchini Kenya ametuletea barua kwanza kabisa anawasalimu wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio china Kimataifa, pia anasema akiwa rafiki wa ndani kabisa wa Radio China Kimataifa anatoa pongezi za dhati kwa juhudi zinazofanywa na Radio China Kimataifa kwa wasikilizaji wote. Ana furaha kubwa kwa kufunguliwa kwa kituo kipya cha CRI huko Tibet pamoja na kuanza kutumika kwa reli mpya huko Tibet.

Anakamilisha barua yake kwa kusema anaishukuru serikali ya Kenya kwa kupunguza gharama za usafiri kwa wale ambao wana hamu ya kuja kuitembelea Kenya, hivyo anawakaribisha sana wachina, na anasema wasikilizaji wa Radio China Kimataifa mjini Bungoma wanawakaribisha watu wote katika sherehe ya kuadhimisha miaka 65 ya Radio China Kimataifa.

Msikilizaji wetu Nassir Kassim S.L.P 1304 Kakamega nchini Kenya anatoa salamu nyingi kwa wafanyakazi wote wa Radio china Kitaifa kutoka Kakamega. Awali ya yote anaomba msamaha kwa kuchelewa kujibu barua zetu, lakini anasema kuchelewa huko hakukuwa na maana kwamba ilikuwa mwisho wa kusikiliza vipindi vya Radio China kimataifa.

Bwana Nassir pia anashukuru sana kwa barua nzuri na ya kufurahisha, anasema hiyo ilikuwa ni barua ya pili kuipata tokea ajiunge na Radio China Kimataifa. Yeye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Shisasari akiwa ni mtahiniwa wa mwaka huu, anasema matangazo na vipindi vizuri vya CRI ndivyo vilimfanya ajiunge na Radio china kimataifa. Anasema ataendelea kuandika barua, anapenda kufahamu machache kuhusu Radio china Kimataifa na pia atafurahi kama atatumiwa kalenda ya Radio China Kimataifa.

Msikilizaji wetu huyu pia anasema alipokea kadi tatu za salamu, lakini hafahamu kama huwa zinatumwa zote kwa pamoja au anatakiwa kutuma moja moja tu, na mwisho anawatakia wafanyakazi wa Radio China kimataifa kazi njema na baraka tele. Kuhusu suala hilo tunaona kuwa anaweza kutoa kadi moja au zote kama apendavyo.

Msikilizaji wetu Ibrahim Kirusha wa S.L.B 772 Ujiji-Kigoma nchini Tanzania katika barua yake anatumai kuwa watayarishaji na watangazaji wa vipindi vya Radio China Kimataifa hatujambo na wanaendelea vyema na kazi. Lengo la barua yake ni kutoa pongezi za dhati kwa wafanyakazi wa Radio China kimataifa kwa kuweza kuwa pamoja na kuwasiliana na wasikilizaji kwa muda mrefu.

Anasema barua wanazopata huwafanunulia mambo mbalimbali na kujifunza kuhusu Radio China Kimataifa na China kwa ujumla, anatuomba tuendelee na uzi huu ili wasikilizaji waweze kunufaika zaidi. Vilevile anatuarifu sisi pamoja na wasikilizaji wengine kuwa sasa amehama Ulyakuru mjini Tabora na sasa yupo Ujiji mjini Kigoma. Hivyo sasa tutawasiliana kupitia kwa anuani mpya ya Ujiji Kigoma, na mwisho anatutakia wafanyakazi wote wa Radio china kimataifa kazi njema.

Tunawashukuru kwa dhati wasikilizaji wetu Nassir M. Kassim na Ibraheem Kirusha kwa barua walizotutumia na kututia moyo kuchapa kazi zaidi ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu. Katika idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, hivi sasa wako vijana wengi ambao walihitimu masomo miaka michache iliyopita, lakini siku hizi wanafanya bidii kubwa katika kutafsiri na kuandaa vipindi mbalimbali, siku baada ya siku hakika watapata maendeleo makubwa na kuchangia zaidi kwenye matangazo ya idhaa yetu.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-26