Msemaji wa Umoja wa Afrika Assan Ba alitangaza tarehe 25 huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia kuwa, Umoja wa Afrika umeamua kuongeza askari 4000 wa kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur, Sudan. Hii ni hatua nyingine kubwa iliyochukuliwa na Umoja wa Afrika kuhusu suala la Darfur baada ya kutoa uamuzi tarehe 20 mwezi huu kuhusu kurefusha muda wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika katika huko Darfur, Sudan hadi mwishoni mwa mwaka huu.
Bwana Assan Ba siku hiyo alisema, "Baraza la amani na usalama" la Umoja wa Afrika limeamua kuwa, kwenye msingi wa hivi sasa ambao jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika kwenye sehemu ya Darafur, Sudan lina askari 7000 hivi, Umoja wa Afrika umeamua kuongeza askari 4000, ambao watatoka kwenye nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kama vile Nigeria, Rwanda, Afrika ya kusini na Senegal, ambazo zimeshiriki kwenye harakati za kulinda amani. Wachambuzi wanaona kuwa, Umoja wa Afrika umeamua tena kuongeza askari wa kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur ni kutokana na sababu kadhaa mbalimbali.
Kwanza ni kutokana na mahitaji ya kutekeleza jukumu la kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur. Mwezi Mei mwaka huu serikali ya Sudan na kundi la Minni Arcua Minnawi la jeshi la upinzani la Sudan vilisaini makubaliano ya amani huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria, lakini namna ya kusimamia kwa ufanisi usimamishaji wa vita wa pande hizo mbili ili hatimaye kukomesha mgogoro kati ya pande hizo mbili, haiwezi kutegemea tu jeshi la kulinda amani lenye askari 7000, ndiyo maana Umoja wa Afrika unapaswa kuongeza askari ili kutekeleza jukumu la kusimamia usimamishaji wa vita na kulinda amani huko Darfur.
Aidha hatua hiyo imeonesha nia ya Umoja wa Afrika ya kuimarisha vitendo vya kulinda amani. Baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya kusimamisha vita kati ya serikali ya Sudan na jeshi la upinzani la Darfur mwezi Aprili mwaka 2004 huko N'djamena mji mkuu wa Chad, kwa mara ya kwanza Umoja wa Afrika ulituma jeshi la kulinda amani lenye askari 7000 kwa sehemu ya Darfur, tena mwezi Machi mwaka huu Umoja wa Afrika uliamua kurefusha muda wake wa kulinda amani hadi tarehe 31 Septemba. Lakini kutokana na hali duni ya silaha na zana za jeshi hilo na ukosefu wa fedha, harakati za kulinda amani za Umoja wa Afrika zilikumbwa na vizuizi mbalimbali huko Darfur, na kulaaniwa mara kwa mara na Marekani na nchi nyingine za magharibi. Hivyo Umoja wa Afrika umeamua kuongeza tena askari wa kulinda amani huko Darfur, ili kuonesha nia yake ya kuimarisha zaidi jukumu la kulinda amani katika sehemu ya Darfur, Sudan.
Tokea mgogoro wa Darfur, Sudan utokee mwezi Februari mwaka 2003, Marekani siku zote inajipenyeza katika suala la Darfur, ikalihimiza Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe azimio la No. 1706 mwishoni mwa mwezi Agosti kuhusu kutuma jeshi la kulinda amani lenye askari elfu 20 kwenye sehemu ya Darfur badala ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika, lakini azimio hilo lilipingwa vikali na serikali ya Sudan. Viongozi wa nchi za Afrika walitoa taarifa tarehe 9 usiku huko Surd, Libya wakiiunga mkono serikali ya Sudan kwa msimamo wake wa kukataa jeshi la kimataifa kuingia Darfur bila idhini yake, pia walisisitiza kukataa kulifanya suala la Darfur liwe suala la kimataifa. Na rais Omar Al Bashir wa Sudan pia ameeleza wazi kuunga mkono vitendo vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika huko Sudan, alisema Umoja wa Mataifa unaweza kutoa misaada ya kimali kwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika. Rais Bashir aliilaani Marekani kujaribu kudhibiti hali ya kutuma jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa ili kuifanya Sudan iwe "Iraq" nyingine. Alisema serikali ya Sudan itahamasisha nguvu zote za kisiasa nchini Sudan ili kuzuia jeshi la kimataifa lisiingie nchini humo.
Wachambuzi wanaona kuwa msimamo wa Rais Bashir umeonesha kuwa, serikali ya Sudan inashikilia msimamo wazi wa kupinga jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa lisiingie kwenye sehemu Darfur, katika hali hiyo Umoja wa Afrika kuamua kuongeza askari wake huko Darfur, hakika ni hatua mwafaka ya kutuliza hali ya sehemu hiyo.
|