Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-27 19:30:14    
Kujumuisha mazoezi ya kazi na masomo umekuwa utaratibu mpya wa mafunzo ya ufundi wa kazi nchini China

cri

Utaratibu mpya wa mafunzo ya ufundi wa kazi unaenezwa kote nchini China, utaratibu huo unaojumuisha mazoezi ya kazi na masomo unaweza kuwapa wanafunzi fursa za kufanya mazoezi ya kazi viwandani wakati wanapojifunza ufundi wa kazi shuleni. Wanafunzi wahitimu wa shule za ufundi wa kazi zinazofuata utaratibu huo wana uwezo mkubwa zaidi wa jumla na wa kufanya kazi, pia makampuni yanapenda sana kuwaajiri wahitimu hao.

Hivi sasa utaratibu huo unatekelezwa kwenye shule za mafunzo ya ufundi wa kazi katika wilaya na miji 38 iliyoko katikati ya mkoa wa Hunan. Wanafunzi wa shule hizo wanaweza kuchagua kwa hiari yao mchepuo mmoja miongoni mwa michepuo 14 ikiwemo usimamizi wa hoteli, utengenezaji wa vipuri, na usambazaji wa bidhaa. Katika muda wa mafunzo wa miaka mitatu, kila baada ya nusu ya mwakawa masomo, wanafunzi watapelekwa kwenye viwanda kufanya mazoezi ya kazi kwa nusu mwaka huku wakilipwa. Baada ya miaka hiyo mitatu, wanafunzi hao watapewa cheti cha sekondari ya juu cha ufundi wa kazi, na wanaweza kuajiriwa moja kwa moja na viwanda vilivyosaini mkataba na shule hiyo.

Mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi wa sanyasi na teknolojia cha mkoa wa Hunan Bw. Yang Dongliang alisema, hivi sasa chuo hicho kimesaini mkataba wa ushirikiano na makampuni matano. Bw. Yang Dongliang alisema:

"tumeweka mpango wa mafunzo kutokana na mahitaji ya makampuni, hivyo wanafunzi wa chuo chetu wameshaandaliwa nafasi za ajira kabla hawajahitimu. Tunapanga kuwasajili wanafunzi 2000 hivi mwakani."

Kutokana na kuwa wanafunzi walioandaliwa kwa kufuata utaratibu huo wana uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi, makampuni mbalimbali yanapenda kuwaajiri wanafunzi hao. Kampuni moja inayoendesha mikahawa ya mji wa Changsha ilisaini mkataba wa kuajiri wahitimu wa chuo hicho. Maneja mkuu wa kampuni hiyo Bi. Cai Yan alisema:

"kampuni yetu pia itatuma wataalamu wa elimu ya nguvu kazi kutoa mafunzo kwa wanafunzi kwenye chuo hicho, kwa hivyo wanafunzi wa chuo hicho wanaweza kuizoea haraka kwenye kampuni yetu."

Hali hiyo kwa upande mmoja imeonesha tatizo linaloikabili elimu ya mafunzo ya ufundi wa kazi ya China, yaani kutenganisha mafunzo ya nadharia na mazoezi ya kazi halisi. Wanafunzi wengi wamejifunza nadharia nyingi za kimsingi, lakini wamepewa fursa chache tu kufanya mazoezi ya kazi halisi. Hivyo wanafunzi kama hao wanakosa uozefu wa kutenda kazi, na ni vigumu kwao kukidhi mahitaji ya makampuni katika muda mfupi. Hili ni tatizo linalotatuliwa kwa utaratibu mpya wa mafunzo ya ufundi wa kazi. Utaratibu huo umeyapunguzia makampuni kwa kiasi kikubwa gharama za kutoa mafunzo kwa wahitmu baada ya kuwaajiri. Hivyo utaratibu huo umeanza kukubalika na kuenezwa nchini China.

Katika wilaya ya Fengkai iliyoko kusini mashariki mwa mkoa wa Guangdong, makampuni 9 ya Taiwan yalisaini makubaliano na chuo kikuu cha mafunzo ya ufundi wa kazi cha huko kuhusu kutoa mafunzo kwa kufuata utaratibu huo. Mkuu wa shule ya mafunzo ya ufundi wa kazi ya wilaya hiyo Bw. Qin Huanzhao alieleza, wanafunzi wanasoma kwa nusu mwaka, na kufanya mazoezi ya kazi yenye mshahara kwa nusu mwaka, wanafunzi wanaweza kulipa ada za shule kwa pato hilo, na mazoezi hayo pia ni sehemu ya mtihani kwa wanafunzi.

Kwenye sehemu inayojiendesha ya wauygur ya Xinjiang, mchepuo wa usimamizi wa hoteli wa chuo cha mafunzo ya ufundi wa kazi cha Kelamayi umekuwa mchepuo wa kwanza kutekeleza utaratibu huo. Chuo hicho kilirekebisha mpango wa mafunzo kutokana na mahitaji ya sekta ya hoteli, na kuwapeleka wanafunzi kufanya mazoezi kwenye hoteli za ngazi ya nyota tano za huko, na kuwapa yuan 300 kila mwezi. Baada ya mazoezi ya nusu mwaka, wanafunzi wanarudi darasani na kuendelea na masomo yao ya nadharia.

Kutokana na utaratibu huo, wanafunzi wengi wamekuwa na ustadi mkubwa wa kufanya kazi kabla hawajahitimu, mbali na hayo, pia wamejifunza utaratibu wa makampuni. Wanafunzi kama hao wote wanaajiriwa mara baada ya kuhitimu masomo. Mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari mafunzo ya ufundi wa kazi ya wilaya ya Fengkai mkoani Guangdong anayeitwa Yan Hui alisema,

"Siku hizi si rahisi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kupata ajira, sisi tunasoma shuleni pamoja na kufanya mazoezi ya kazi viwandani, itakuwa ni rahisi zaidi kwetu kupata ajira baada ya kuhitimu."

Imefahamika kuwa, utaratibu wa kujumuisha masomo na mazoezi ya kazi umekuwa na historia zaidi ya miaka mia moja katika nchi zilizoendelea. Nchini Ujerumani, kila wiki wanafunzi wanafanya kazi kwa siku tatu na kuingia darasani kwa siku mbili, asilimia 60 ya wanafunzi wanapewa mafunzo ya utaratibu huo. Wataalamu wanasema, utaratibu huo wa mafunzo unaweza kuinua kiwango cha wanafunzi cha kufanya mazoezi ya kazi halisi, kupunguza uwekezaji wa shule katika vifaa na mafunzo kwa walimu, pia unaweza kupunguza mzigo wa kiuchumi kwa familia za wanafunzi.

Lakini hivi sasa, nchini China utekelezaji wa utaratibu wa kujumuisha masomo na mazoezi ya vitendo bado bado unakabiliana na matatizo kadhaa wa kadhaa. Kwa mfano, mitizamo ya elimu ya kijadi ya China inayozingatia mafunzo ya nadharia na kupuuza mafunzo ya ufundi bado ipo. Kwa hivyo mpango wa masomo katika shule au vyuo mbalimbali bado unapendelea mafunzo ya nadharia na kuwapa fursa kidogo ya kufanya mazoezi ya vitendo. Kuhusu hali hiyo, mtaalamu wa taasisi ya kituo cha mafunzo ya kazi katika wizara ya elimu ya China Bw. Yu Zuguang alisema, wakati wa kuweka mkazo katika kuendeleza elimu ya juu na kuandaa watalaamu wa kiwango cha juu, China pia inapaswa kutilia maanani kuandaa mafundi wa sekta mbalimbali. Utaratibu wa kujumuisha masomo na mazoezi ya kazi unastahili kuenezwa kwenye shule za mafunzo ya ufundi wa kazi kote nchini China. Bw. Yu Zuguang alisema:

"kwa jumla, utaratibu huo ni mwelekeo wa kisasa, hasa unalenga kutoa elimu ya kudumu maishani."

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza maelezo kuhusu Utaratibu wa kujumuisha mazoezi ya vitendo na masomo ambao umekuwa utaratibu mpya wa mafunzo ya ufundi wa kazi nchini China. Asanteni kwa kutusikiliza. Kwa herini!

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-27