Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-28 16:24:25    
Wanafunzi wa Taiwan wafurahia kuitembelea China Bara

cri

Hivi sasa katika nusu ya sehemu ya kaskazini ya dunia yetu, majira ya joto yamekwisha, ambapo likizo ya majira ya joto kwa wanafunzi pia imemalizika. Hapo awali wanafunzi wa Taiwan walikuwa wanapenda kwenda Marekani na nchi za Ulaya kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kambi za majira ya joto, lakini hivi sasa wanafunzi hao wanavutiwa zaidi kuja China Bara. Katika likizo hiyo ya mwaka huu, wanafunzi zaidi ya 1,300 kutoka sehemu ya Taiwan, China walishiriki kwenye shughuli za kambi ya majira ya joto zilizoandaliwa na Shirika la ndugu wa Taiwan la China. Kwa wengi kati ya wanafunzi hao hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kukanyaga ardhi ya China Bara, na safari hiyo iliwavutia sana.

Katika safari hiyo vijana hao kutoka Taiwan waligawanywa katika makundi zaidi ya 10, ambapo makundi hayo yalitembelea sehemu mbalimbali za China kwa nyakati tofauti kabla ya kufika kituo cha mwisho cha Beijing.

Kijiogrofia China Bara na Taiwan zipo katika kando mbili za mlango bahari wa Taiwan wenye upana wa kilomita 556 hivi, lakini kutokana na sababu mbalimbali vijana wa Taiwan hawana ufahamu mkubwa kuhusu China Bara. Mwanafunzi mmoja kutoka Taiwan alisema kabla ya safari hiyo, alikuwa hajui kama mji wa Chengdu ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Sichuan uliopo kusini magharibi mwa China, ambao una ustawi mkubwa unaofanana na mji wa Taipei huko Taiwan, na wala alikuwa hafahamu kama kasri la kifalme la mjini Beijing ni kubwa na zuri namna alivyoliona, na kumbe wanafunzi wa China Bara ni wachangamfu na wakarimu kama wanafunzi wa Taiwan walivyo.

Wang Zheng anayesoma kwenye chuo kikuu cha ualimu cha Taiwan alieleza kuwa, anapenda kusoma vitabu kuhusu historia ya China tangu utotoni mwake, na safari hiyo ya China Bara ilimpa fursa ya kuongeza ufahamu wake kwa utamaduni wa China. Alisema "Awali tulisoma vitabu tu, hatukuweza kutembelea na kutazama wenyewe sehemu mbalimbali zenye mabaki ya kale. Lakini sasa tumeshuhudia vitu hivyo vilivyotajwa kwenye vitabu vya masomo, tunaweza kuhisi historia ndefu ya miaka elfu 5 ya China, na utamaduni wake wa aina mbalimbali."

Katika safari hiyo ya China Bara, pamoja na kutembelea sehemu mbalimbali zenye vivutio na mabaki ya kale, wanafunzi wa Taiwan pia walipata fursa ya kushuhudia na kujifunza ufundi wa jadi wa China wa kutengeneza vitu kwa mikono.

Mbali na matembezi hayo, vijana hao kutoka Taiwan pia walikuwa na hamu ya kubadilishana maoni na vijana wa China Bara kuhusu masuala mengi yanayofuatiliwa na vijana kwa pamoja.

Katika chuo kikuu cha makabila cha China kilichopo sehemu ya magharibi ya mji wa Beijing, vijana hao wa Taiwan walikaribishwa na wanafunzi wa chuo kikuu hicho kutoka makabila mbalimbali ya China.

Wanafunzi wawili waliwasalimu kwa lugha ya kabila lao. Walisema "Mimi naitwa Pakeyizhati. Jina langu ni Hasitieer. Sisi ni wa kabila la Wakhazak, tunatoka mkoa wa Xinjiang. Tunawakaribisha kwenye chuo kikuu cha makabila cha China. Hii ni mila ya kabila letu la Wakhazak ya kuwalaki wageni, yaani tutasambaza peremende hizi, watu watakaopokea peremende hizi watapata baraka, furaha na neema. Tunawatakia bahati njema."

Chuo kikuu cha makabila cha China kinajulikana kwa kuwaandikisha wanafunzi wa makabila madogomadogo, na migononi mwa vijana hao wa Taiwan waliokwenda kutembelea chuo kikuu hicho wengi wanatoka kwenye makabila madogomadogo. Watu wa makabila hayo ni hodari katika kuimba nyimbo na kucheza ngoma, kwa hiyo muziki na ngoma zilikuwa ni njia mwafaka kwa vijana hao kuwasiliana.

Kijana wa Taiwan Hu Zhenggui anatoka kwenye kabila dogo. Alisema katika maskani yake kila mtu anafahamu wimbo mmoja, na watu wanapoimba wimbo huo wanakaa pamoja, wakiimba huku wakicheza ngoma. Kwa hiyo vijana wenzake wakimwiga, walishikana mikono na kuimba wimbo huo kwa pamoja.

Katika chuo kikuu hicho vijana wa Taiwan pia walitembelea jumba la makumbusho la makabila. Katika jumba hilo kwa mara ya kwanza walitazama vitu vinavyohusu makabila madogomadogo nchini China, yakiwemo makabila huko Taiwan. Walifurahia kuona kuwa vitu hivyo vinahifadhiwa vizuri na kuoneshwa kwa umma huku China Bara.

Licha ya kutizama vijana wengi wa Taiwan pia walifikiri masuala mbalimbali katika safari hiyo. Kwa mfano baadhi ya vijana wanasomea kozi ya utawala bora, ambao walipotembelea Beijing walitafiti mpango wa ujenzi wa mji huo, huku wengine walijadiliana jinsi China Bara ilivyoendeleza uchumi wake kwa kasi katika muda mfupi. Vijana hao wa Taiwan pia walieleza nia ya kushiriki kwenye maendeleo ya China Bara. Bw. Wang Zheng alisema marafiki zake wengi wa Taiwan wanatumai kuja China Bara kusoma au kupata ajira, na yeye mwenyewe anafuatilia sana michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa hapa Beijing mwaka 2008.

Alisema  "Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 inakaribia. Kwa maoni yangu kuna masuala mawili ambayo yangepewa kipaumbele. Moja ni mawasiliano ya mji wa Beijing, na lingine ni mafunzo ya lugha za kigeni. Naona masuala hayo mawili yanatakiwa kuzingatiwa katika maandalizi ya michezo ya Olimpiki."

Shughuli za kambi ya majira ya joto ziliwaletea vijana hao wa Taiwan furaha kubwa, hata hivyo muda wake ulikuwa mfupi. Katika siku hizo vijana wengi wa China Bara na Taiwan walijenga urafiki, na kabla ya kuagana walibadilishana anuani za barua pepe na kuahidi kuwasiliana katika siku zijazo.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-28