Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-28 16:26:19    
Kinyang'anyiro cha kuwatafuta warembo wa makabila mbalimbali ya China

cri

China ina makabila 56. Hivi karibuni kinyang'nyiro cha kuwatafuta warembo wa makabila hayo kilifanyika hapa Beijing, ambapo makabila hayo 56 kila moja lilimchagua msichana mmoja mwerevu apewe sifa ya mrembo wa kabila lake. 

 Mnaosikia ni wimbo wa kabila la Wamongolia uitwao "peponi". Msichana mmoja wa kabila hilo Dada Qiqige alikuwa anacheza ngoma kwa kufuata mdundo wa wimbo huo. Wamongolia hujulikana kama kabila la mbugani, wengi wao wanaishi kwenye mkoa wa Mongolia ya ndani nchini China, ambapo kizazi baada ya kizazi Wamongolia wanajishughulisha na ufugaji. Akizungumzia kabila lake, Dada Qiqige alionesha imani na fahari. Alisema "Kabila langu lina historia ndefu na utamaduni imara. Sisi Wamongolia tuna damu ya Genghis Khan. Sisi ni wakarimu, na wenye moyo shujaa na imara."

Msichana huyo alisema ni fahari kubwa kwake kuchaguliwa kuwa mrembo wa kuwakilisha kabila lake la Wamongolia. Aliongeza kuwa, hivi sasa kuna watu wengi ambao hawatilii maanani utamaduni wa kabila lao, idadi ya makazi ya jadi ya Kimongolia inapungua siku hadi siku, ambapo watu wengi zaidi wanahamia mijini. Dada huyo alieleza matumaini yake kuwa, atajitahidi kuwafahamisha watu wengine kabila la Wamongolia na mbuga ili aweze kustahili sifa hiyo ya mrembo wa kabila la Wamongolia.

Dada Lin Jing mwenye umri wa miaka 19 anatoka kabila la Wahani wanaoishi mkoani Yunnan, kusini magharibi mwa China. Alisema  "Naona shughuli hizo za kuwachagua warembo wa makabila mbalimbali zina maana sana, ambazo hazitilii maanani tu urembo, kwani katika shughuli hizo tunaweza kueneza utamaduni wa makabila mbalimbali, kuwafanya watu wengi zaidi wafuatilie makabila hayo, na kusaidia kuleta maendeleo ya makabila hayo."

Msichana huyo Lin Jing alieleza maoni yake kuwa, kutokana na maendeleo ya uchumi wa China, watu wengi zaidi wameondoka vijijini na kuhamia mijini. Licha ya kupata uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi, nguvu ya ushawishi ya utamaduni wa jadi wa kabila la Wahani inapungua siku hadi siku. Alisema atafanya kila awezalo kueneza utamaduni wa kabila lake.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa shughuli hizo za kuwachagua warembo wa makabila mbalimbali kufanyika nchini China. Vigezo muhimu zaidi ni ujuzi walio nao wasichana hao, pamoja na ufahamu na upendo wao kuhusu makabila yao, kwani kila msichana aliyepewa sifa ya mrembo wa kabila anawakilisha kabila lake badala ya yeye binafsi, na kila mrembo anatakiwa kuwa mrithi wa utamaduni wa kabila lake.

Mratibu mkuu wa shughuli hizo Bw. Zhang Huaizhong alisema kufanyika kwa shughuli hizo kuna lengo la kuwafanya watu wafuatilie na kuhifadhi utamaduni wa asili wa makabila madogomadogo ya China. Alisema  "Hivi sasa kutokana na maendeleo ya uchumi wa kisasa, utamaduni wa makabila kadhaa madogomadogo upo hatarini kupotea kabisa. Nchini China makabila madogomadogo yamepata maendeleo na kuwa ya kisasa, kwa upande wa mambo ya kiuchumi hali hii inawafurahisha watu, lakini kwa upande wa mambo ya kiutamaduni, naweza kusema hayo ni maafa."

Sehemu nyingi wanakoishi watu wa makabila madogomadogo nchini China bado zina hali duni ya maendeleo, Bw. Zhang Huaizhong akichambua sababu zake alieleza kuwa, mbali na matatizo ya kijiogrofia, sababu nyingine kubwa ni watu hodari wa makabila hayo kutokuwa na fursa za kuonesha uhodari wao. Kwa hiyo shughuli hizo za kuwachagua warembo wa makabila mbalimbali zinawaandalia jukwaa la kufanya mawasiliano na watu wa sehemu nyingine. Aliongeza kuwa, "Naona utamaduni wa China una umaalumu wake, na kila kabila lina utamaduni maalumu. Umaalumu huo unastahili kuoneshwa duniani, na utamaduni wa China pia ni mali za binadamu wote. Kama hivi sasa hatutachukua hatua za kuokoa utamaduni huo, baada ya vizazi fulani au miongo kadhaa, labda utaoneshwa tu kwenye majumba ya makumbusho."

Mtengenezaji wa filamu Bw. Zhu Zhizhong alisema anakubaliana na maoni ya Bw. Zhang Huaizhong. Alisema katika shughuli za kuwachagua warembo wa makabila mbalimbali, wasichana hao walionesha umaalumu wa utamaduni wa makabila yao. Alisema "Nilishuhudia jinsi wasichana hao walivyotoa hotuba na maelezo kwa uchangamfu mkubwa, ili kuonesha uzuri wa makabila yao, naona moyo wa namna hii ni muhimu zaidi, na moyo huo unaweza kuleta ufufuaji na ustawi wa utamaduni wa China."

Idhaa ya kiswahili 2006-09-28