Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China tarehe 28 alitangaza kuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wu Dawei, ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa China wa mazungumzo ya pande 6 alialikwa Korea ya Kusini tarehe 29 ili kufanya majadiliano na Korea ya Kusini na kubadilishana maoni kuhusu kuanzisha tena mazungumzo ya pande 6 na masuala mengine yanayofuatiliwa kwa pamoja na pande hizo mbili.
Wizara ya mambo ya nje na biashara ya Korea ya Kusini tarehe 28 ilisema, katika ziara yake ya tarehe 29 Septemba hadi tarehe 1 Oktoba, Bw. Wu Dawei atakutana na waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya Kusini Bw. Ban Ki-moon, pia atafanya majadiliano na naibu waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya Kusini na mkuu wa ujumbe wa Korea ya Kusini wa mazungumzo hayo, ambapo watabadilishana maoni kuhusu "mpango mpya wa mawasiliano ya pande zote" wa kuanzisha tena mazungumzo ya pande 6 uliotolewa na rais Roh Moo-hyun wa Korea ya Kusini kwa rais Bush wa Marekani alipofanya ziara nchini Marekani katikati ya mwezi huu. Rais Roh Moo-hyun tarehe 28 alisema, rais Bush amekubali mpango huo, na serikali ya Korea ya Kusini itatangaza mpango huo unaokubaliwa na Marekani na Korea ya Kaskazini.
Tarehe 19 Septemba mwaka jana, katika duru la 4 la mazungumzo ya pande sita, pande husika zilisaini taarifa ya pamoja, na kuthibitisha kutimiza lengo na kanuni ya kutokuwa na silaha za nyuklia katika peninsula ya Korea kwa amani. Lakini muda mfupi baadaye, Marekani iliiwekea Korea ya Kaskazini vikwazo vya kifedha kwa kudai kuwa Korea ya Kaskazini inatengeneza dola za kimarekani za bandia, hivyo Korea ya Kaskazini ilikataa kurudi kwenye mazungumzo ya pande 6, na kuchukulia kuondoa vikwazo hivyo kuwa ni sharti la kurudi kwake kwenye mazungumzo ya pande 6. Mwaka huu, Marekani ilikataa mwaliko wa Korea ya Kaskazini uliotolewa kwa mkuu wa ujumbe wa Marekani wa mazungumzo ya pande 6, jambo ambalo pia lilileta athari mbaya katika kuanzishwa tena mazungumzo hayo. Korea ya Kaskazini pia ilikataa kupokea azimio lililopitishwa tarehe 15 Julai na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo linafuatilia na kulaani majaribio ya makombora ya Korea ya Kaskazini, na kutoa mwito wa kuanzisha tena mazungumzo mapema.
Hivi sasa misimamo ya Marekani na Korea ya Kaskazini inapingana. Baada ya Korea ya Kaskazini kufanya majaribio ya makombora, Marekani ilizidi kuiwekea vikwazo Korea ya Kaskazini. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea ya Kaskazini tarehe 26 kwenye majadiliano ya baraza kuu la 61 la Umoja wa Mataifa alisema, kutokana na kitendo cha Marekani, hivi sasa Korea ya Kaskazini haitarudi kwenye mazungumzo ya pande 6.
Tofauti na Marekani, China na Korea ya Kusini siku zote zinafanya juhudi ili kuanzisha tena mazungumzo ya pande 6. China siku zote inasisitiza kutatua masuala kwa njia ya mazungumzo, na kupinga kuweka vikwazo. China inaona kuwa, hivi sasa hali ya peninsula ya Korea ni ya utatanishi, na pande zote zinapaswa kuweka mkazo katika namna ya kupunguza hali ya kukwama na kuhimiza pande 6 zianzishe tena mazungumzo mapema; inazitaka pande mbalimbali husika zizingatie zaidi amani na utulivu wa peninsula ya Korea na sehemu kaskazini mashariki ya Asia na kujizuia, ili kuepusha hali kuwepo kwa utatanishi tena, na kuweza kuanzisha tena mazungumzo mapema. China inawasiliana na kushirikiana na pande zote husika ili kuhimiza mazungumzo hayo yaweze kuanzishwa tena mapema.
Ingawa serikali ya Korea ya Kusini ilisita kutoa misaada ya kiuchumi kwa Korea ya Kaskazini baada ya Korea ya Kaskazini kufanya majaribio ya makombora, lakini Korea ya Kusini inapinga kuzidi kuiwekea vikwazo Korea ya Kaskazini. Korea ya Kusini inapendekeza Marekani ichukue msimamo wa unyumbufu, na kufanya mazungumzo na Korea ya Kaskazini moja kwa moja. Rais Roh Moo-hyun tarehe 28 alipohojiwa na vyombo vya habari alisema, China imefanya juhudi nyingi ili kuishawishi Korea ya Kaskazini irudi kwenye mazungumzo, na Korea ya Kusini pia inajaribu kuishawishi Marekani. Pia alisema Korea ya Kaskazini na Marekani zinapaswa kuaminiana.
Rais Roh Moo-hyun pia alisisitiza, taarifa ya pamoja iliyotolewa na duru la 4 la mazungumzo ya pande 6 sio tu ni mpango wa kutatua suala la nyuklia la peninsuala ya Korea, bali pia ina maana, kuwa mfumo wa usalama wa pande nyingi yaani mazungumzo ya pande 6 utahakikisha amani na ustawi wa sehemu za kaskazini mashariki ya Asia.
China na Korea ya Kusini zimefanya kazi nyingi za kiujenzi kwa mazungumzo hayo. Sasa jambo muhimi ni misimamo ya Marekani na Korea ya Kaskazini. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice tarehe 26 alisema, atafanya ziara katika nchi husika za Asia, ili kufahamu kama kuna mahitaji ya kufanya juhudi za mwisho au la, na kuna matumaini kuwa atafanya kazi kwa kuanzisha tena mazungumzo ya pande 6 katika ziara yake barani Asia.
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-29
|