Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-02 18:43:52    
Sikukuu ya Mwezi ya Wachina

cri

Tarehe 5 Oktoba ni tarehe 15 Agosti kwa kalenda ya mwezi ya Kichina, katika siku hiyo jamaa hujiunga pamoja na kuisherehekea siku hiyo na kuburudika kwa mwezi wa mviringo kabisa katika mwaka mzima.

Katika historia ya China, kila mwaka katika siku hiyo wafalme walikwenda kwenye madhabahu ya kuabudu mwezi. Desturi hiyo ilianzia Enzi ya Qi miaka zaidi ya 2000 iliyopita hadi enzi ya kifalme ya mwisho, Enzi ya Qing. Hata raia pia walikuwa na namna yao ya kuabudu mwezi yaani waliandaa matunda na keki zilizopikwa kwa duara kama mwezi. Desturi hiyo inayoendelea hadi leo imekuwa ya kuburudika kwa mwezi tu. Mwezi unapokuwa mbinguni, familia yote huburudika kwa mwezi huo kwa pamoja huku wakiongea na kula matunda na keki za mwezi. Katika siku hiyo watoto hufurahi sana kwa sababu wanaweza kupata keki tamu za mwezi. Kutokana na kumbukumbu za historia, desturi ya kula keki za mwezi ilianzia Enzi ya Tang, miaka 1500 iliyopita. Keki za hivi leo za mwezi zimekuwa za aina nyingi, ambapo kila sehemu nchini China huwa na keki zake kutokana na mapishi tofauti.

Hali ya hewa nchini China inagawanyika katika majira manne wazi. Sababu ya Wachina kuchagua tarehe na mwezi huo ni kuwa hali ya hewa katika majira ya baridi inakuwa ni baridi sana, haifurahishi kuufurahia mwezi nje ya nyumba; katika majira ya joto mawingu hutanda mbinguni yakiziba mwezi; na majira ya mchipuko yaani Spring ni msimu wa shughuli nyingi za kilimo, watu hawana muda wa kuufurahia mwezi; ila tu majira ya kipupwe yaani Autumn ambapo hakuna joto wala baridi, mbingu hutakata na pia ni majira ya kuvuna, matunda hukomaa, watu baada ya kufanya kazi za kilimo mwaka mzima sasa wanaweza kuufurahia mwezi na kufaidi mazao yao.

Wachina wanaona kwamba sikukuu ya mwezi ni siku ya kuungana kwa familia. Siku hiyo kama mtu akishindwa kuungana na jamaa zake hujiona mpweke na kujiona yuko katika hali ambayo aliieleza mshairi mashuhuri Li Bai alivyoandika katika shairi lake, "kuinua kichwa kuangalia mwezi na kuinamisha kichwa kukumbuka maskani", mshairi mkubwa Zhang Jiuling pia aliandika, "Mwezi wachomoza baharini, ni wakati wa pamoja kwa Wachina wote duniani."

Mwanzoni mwa mwaka huu, sikukuu ya mwezi ya Wachina iliorodheshwa katika urithi wa utamaduni usioonekana nchini China, wakati sikukuu hiyo ya jadi ya Wachina inapofika tunawatakia afya njema na furaha ya kuishi pamoja na jamaa zenu.

Idhaa ya Kiswahili 2006-10-02