Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-02 19:11:49    
Makundi ya Hamas na Fatah yafanya mapambano makali ya kijeshi

cri

Kundi la Hamas na Kundi Fatah ya Palestina yalifanya mapambano makali ya kijeshi tarehe 1 Oktoba kwenye ukanda wa Gaza, ambapo watu zaidi ya wanane waliuawa, na wengine zaidi ya 70 walijeruhiwa. Hayo ni mapambano makali zaidi ya kijeshi kutokea ndani ya Palestina tangu kundi la Hamas lishike madaraka ya utawala mwezi Machi mwaka huu.

Kikosi cha usalama cha Palestina kinacholitii Kundi la Fatah siku hiyo kilifanya maandamano kwenye ukanda wa Gaza, kikiilaani serikali ya Hamas kuchelewesha mishahara kwa watumishi wa serikali katika nusu mwaka uliopita. Waandamanaji walifunga njia kuu kwenye ukanda wa Gaza, na kuchoma moto matairi na kuweka takataka katikati ya barabara. Ili kuwafukuza waandamanaji, idara husika ya Kundi la Hamas iliweka wanajeshi elfu kadhaa kwenye sehemu hiyo, na baadaye pande hizo mbili zilifanya mapambano ya kumwaga damu. Watu walioshuhudia mapambano hayo walisema, mapambano makali zaidi kati ya pande hizo mbili yalitokea karibu na Jengo la bunge mjini Gaza ambapo watu wanne waliuawa, wakiwemo watoto wawili.

Mapambano kati ya Kundi la Fatah na Kundi la Hamas pia yalienea kwenye sehemu ya kando la magharibi la Mto Jordan. Waungaji mkono wa Kundi la Fatah waliingia kwenye jengo la serikali ya utawala wa Palestina huko Ramallah, ambapo ofisi za mawaziri kadha wa kadha wa Hamas na kamati ya utungaji wa sheria ya Palestina zilichomwa moto na kuteketezwa. Huko Nablus mji ulioko magharibi ya Mto Jordan, wanajeshi kumi kadhaa wa Fatah walifyatua risasi angani wakidai kuwa watalipiza kisasi juu ya mashambulizi ya Hamas.

Ili kuzuia mgogoro usizidi kupanuliwa, pande mbalimbali za Palestina zimetaka mgogoro huo ukomeshwe mara moja. Kiongozi wa Kundi la Fatah Bwana Mahmoud Abbas siku hiyo alitoa hotuba kwa njia ya televisheni akilaani vikali mgogoro huo, na kuzitaka pande mbalimbali zitulie ili kukwepa kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Bwana Abbas pia alitoa amri ya kuwataka watu wote wa kikosi cha usalama warudi kambini, na ametaka uchunguzi ufanyike juu ya mgogoro huo. Na waziri mkuu wa serikali ya utawala wa Palestina ambaye pia ni kiongozi wa Kundi la Hamas Bwana Ismail Haniyeh amewataka wapalestina waondolee mbali migongano kati yao, na kudumisha umoja wa kitaifa. Bwana Haniyeh tarehe 1 usiku aliongea kwa njia ya simu na Bwana Abbas akitaka hatua za pamoja zichukuliwe ili kukomesha mgogoro huo na kuanza tena mazungumzo ya kuunda pamoja baraza la mawaziri.

Lakini wachambuzi wanaona kuwa, mgogoro huo wa kijeshi umeisogeza tena Palestina kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tokea Kundi la Hamas lishike madaraka mwanzoni mwa mwaka huu, kutokana na vikwazo vya kiuchumi vya nchi za magharibi, serikali ya Hamas siku zote iko katika mgogoro mbaya wa fedha, hivyo katika nusu ya mwaka uliopita serikali hiyo haikuweza kutoa mishahara kwa watumishi wa serikali, hivyo watu wengi walifanya maandamano mara kwa mara. Mapambano ya kimabavu yaliyotokea tarehe 1 Oktoba ni mapambano makali zaidi kuliko mengine, lakini Bwana Abbas tarehe 1 alisema akiwa kiongozi wa Palestina kamwe hataruhusu kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, Kundi la Fatah na Kundi la Hamas yalitangaza kuwa yataunda baraza la mawaziri kwa pamoja. Lakini kutokana na kuwa Kundi la Hamas kukataa kuitambua Israel, mazungumzo kuhusu kuunda baraza la mawaziri hayakupata maendeleo. Mapambano ya kimabavu yaliyotokea tarehe 1 Oktoba yamezidisha zaidi migongano kati ya pande hizo mbili, kuanzisha tena mazungumzo hayo kutakabiliwa na taabu kubwa zaidi.

Idhaa ya Kiswahili 2006-10-02