Nchi 15 wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 2 zilipiga kura kwa mara ya nne kuhusu uteuzi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya kusini Bwana Ban ki Moon amepata kura 14 za ndiyo, na ndio maana anatazamiwa kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Mataifa, mgombea wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anapaswa kupata zaidi ya kura 9 za ndiyo kutoka kwa nchi wajumbe wa Baraza la usalama, tena atateuliwa na Baraza la usalama bila kupingwa na wajumbe wa baraza la usalama. Katika maduru matatu ya upigaji kura za maoni, Bwana Ban Ki Moon kila mara alipata kura nyingi zaidi kuliko wengine. Katika duru la nne la upigaji kura, nchi 5 wajumbe wa kudumu wa Baraza la usalama China, Ufaransa, Marekani, Uingereza na Russia kwa mara ya kwanza zilitumia kura zenye rangi tofauti na zile za nchi zisizo wajumbe wa kudumu wa baraza hilo, ili kuonesha dhahiri nchi wajumbe wa kudumu zilipiga kura za ndiyo au la kura za hapana, kama mgombea fulani angepigiwa kura za hapana na nchi wajumbe wa kudumu basi angechujwa.
Kutokana na matokeo ya duru la nne la upigaji kura, hakuna nchi hata moja kati ya nchi 5 wajumbe wa kudumu iliyopiga kura ya hapana, hivyo Bwana Ban Ki Moon alipata kura 14 za ndiyo na kura moja "isiyoeleza maoni", hii inamaanisha kuwa Bwana Ban Ki Moon amekubaliwa na zaidi ya nchi 9 wajumbe wa Baraza la Usalama zikiwemo nchi 5 wajumbe wa kudumu.
Katika kazi za kubadilisha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa zilizofanyika katika awamu zilizopita, kazi za kumteua mtu huwa zinacheleweshwa sana, na zilikuwa zinaathiri mtu aliyeteuliwa kushika madaraka bila matatizo. Na hivi sasa ni wakati muhimu kwa mageuzi ya Umoja wa Mataifa na kutekeleza "nyaraka za matokeo" za mkutano wa wakuu wa mwaka 2005, hivyo pande mbalimbali zote zina matumaini kuwa Baraza la usalama litaweza kufikia kauli moja kuhusu uteuzi wa katibu mkuu mpya mwanzoni mwa mwezi Oktoba. Aidha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pia zina matumaini kuwa katibu mkuu mpya anatakiwa kuyaelewa zaidi mambo ya Umoja wa Mataifa, na ni bora ateuliwe kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa, ndiyo maana Bwana Ban Ki Moon amekubaliwa zaidi kuliko naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Shashi Tharoo mwenye uraia wa India. Na muhimu zaidi ni kuwa Bwana Ban Ki Moon ameungwa mkono na nchi 5 wajumbe wa kudumu wa Baraza la usalama, hasa China na Marekani.
Bwana Ban Ki Moon mwenye umri wa miaka 62 alihitimu kwenye kitivo cha mambo ya kidiplomasia katika Chuo kikuu cha Seoul cha Korea ya kusini, na alipata shahada ya pili ya elimu ya utawala ya Chuo cha siasa cha Kennedy katika Chuo kikuu cha Harvard cha Marekani. Mwaka 1970 alianza kufanya kazi katika wizara ya mambo ya nje na biashara ya Korea ya kusini, na aliwahi kufanya kazi katika ubalozi wa Korea ya kusini nchini India, katika ujumbe wa Korea ya kusini kwenye Umoja wa Mataifa na katika ubalozi wa Korea ya kusini nchini Marekani, baadaye alikuwa balozi wa Korea ya kusini nchini Austria ambaye pia alikuwa mwakilishi wa nchi hiyo katika ofisi za Umoja wa Mataifa huko Vienna na jumuiya nyingine za kimataifa, na mwezi Januari mwaka 2004 alianza kuwa waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya kusini.
Baada ya kutangaza kugombea wadhifa wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki Moon alitembelea nchi mbalimbali mara kwa mara, kwa kuwa anaonekana kuwa ni mtu mpole watu fulani walikuwa na mashaka kwamba yeye atashinda au la kufanya kazi ya katibu mkuu, aliwajibu kuwa, ingawa anaonekana ni mpole lakini kabisa hakosi nguvu ya kufanya maamuzi.
Idhaa ya Kiswahili 2006-10-03
|