Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-03 20:53:50    
Ngono za utotoni ni kuporomoka kwa maadili ?

cri

Tatizo la watoto kujihusisha na ngono wakiwa katika umri mdogo limekuwa likizungumzwa kila siku katika maisha ya Watanzania.

Wanaolizungumzia ni pamoja na wana harakati wa haki za watoto ambao pia wamekuwa wakieleza sababu mbali mbali zinazolifanya tatizo hilo kuendelea kuwa tabia katika jamii.

Kimsingi tatizo hili ni kubwa katika jamii na linatokana na sababu mbali mbali ikiwa ni pamoja na umaskini katika familia.

Hali kadhalika, wazazi kushindwa kuwaeleza watoto kuhusu mabadiliko ya kimwili hasa wanapokaribia balehe. Kwa vyovyote vile, tatizo hili ni la hatari mno katika makuzi ya watoto na hasa wale wa kike ambao mara nyingi ndiyo wanaonekana kuwa wanajiingiza katika vitendo hivyo mapema zaidi.

Katika ripoti yake ya mwaka huu, Shirika la Kazi Duniani (ILO) linasema kuwa watoto wengi katika nchi za Afrika, wanajihusisha na ngono wakiwa bado katika umri mdogo.

Limetoa mfano wa Rwanda kuwa ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye idadi kubwa ya watoto wanajihusisha na biashara ya ngono.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi kubwa ya watoto hao ni wale ambao ni yatima na kwamba wanafanya hivyo kama njia ya kuwawezesha kupata kipato cha kuwawezesha kuendesha maisha.

Ripoti inasema katika ukanda wa nchi za Afrika Magharibi, watoto wapatao 35,000 wanajihusisha na biashara ya ngono wakiwa bado na umri mdogo.

Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) linasema zaidi ya watoto milioni mbili duniani kote wanajihusisha na biashara ya ngono.

Biashara ya ngono ni miongoni mwa biashara zinazopigiwa kelele ili kuokoa maisha ya watoto wengi ambayo yako hatarini.

Kama ilivyodokezwa, kiini cha tatizo hili ni ama umaskini uliokithiri katika jamii au wazazi kuchelewa kuwapa watoto elimu ya kuwawezesha kujitambua kuhusu mabadiliko ya miili yao.

Kwa maneno mengine kuna umuhimu mkubwa kwa wazazi kuwapa watoto elimu ya stadi ya maisha ili kuwawezesha kujitambua na hata kuachana na tamaa.

Tatizo la watoto kukosa elimu linachangia katika kuwafanya waamue kujiingiza katika ngono za utotoni kwa lengo la kujipatia kipato .

Shirika la Kazi Ulimwenguni, limetahadharisha kuwa ngono za utotoni, zinawaweka watoto katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na Ukimwi.

Lakini pia linasababisha wasichana wadogo kupata mimba wakiwa bado na umri mdogo na hata kukatisha masomo.

Vitendo vya watoto kujiingiza katika ngono za utotoni, pia zinachangia katika kuwafanya baadhi ya watu kuwatumia watoto hao na kujipatia vipato haramu.

Hapa Tanzania tumeshawahi kusikia ripoti zikisema baadhi ya watu wamediriki hata kwenda vijijini na kuwakusanya wasichana wadogo na kuwapeleka mijini ambako wamekuwa wakiwatumia katika biashara ya ngono inayowanufaisha watu hao.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Maendeleo ya wanawake na watoto Bi. Justa Mwaituka anasema kuwa,kuna sababu mbalimbali zinazofanya watoto wajiingize kwenye ngono za utotoni.

Kama watu wengine, anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja umaskini na watoto kukosa elimu kuhusu makuzi yao.

"Tamaduni nyingi za kiafrika hazina kawaida ya kumkalisha chini mtoto na kumueleza mabadiliko ya mwili wake na changamoto ziinazomkabili badala yake watoto wengi wamekuwa wakipata taarifa kutoka kwa wenzao" anasema.

Anasema kusambaratika kwa ndoa pia kunawafanya watoto kujiingiza katika ngono za utotoni kwa sababu watoto wanakosa ulinzi kutoka kwa wazazi.

Anasema kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo hilo na athari zake kwa watoto, kuna umuhimu kwa wazazi kubadilika na kuwaeleza watoto wao mambo yanayohusu mabadiliko ya miili yao.

Anasema kufanya hivyo kutasaidia katika kuwaandaa kukabiliana na changamoto zilizoko mbele yao.

" Watoto wengine wanakuwa na hamu ya kutaka kujaribu na kujikuta tayari wamekwisha ingia kwenye ngono za utotoni" anasema Bi Mwaituka.

Anasema watoto lazima wapewe elimu ya standi za maisha ili wawe na ujarisi wa kuthamini miili yao na kwa wale waliowahi kufanya mapenzi wapewe ujasiri wa kujizuia.

"Wale ambao hawajawahi kufanya mapenzi wafundishwe namna ya kujitunza na namna ya kukabiliana na tamaa za mwili," anasema Mkurugenzi huyo.

Watoto hao pia wanakabiliwa na hatari ya kurubuniwa na watu wazima ambao wanafanya nao mapenzi na kuhatarisha afya zao.

"Kielimu watoto wa kike ambao ni wanafunzi wanaojitumbukiza katika ngono za utotoni, maendeleo yao si mazuri." anasema.

Anasema kwa msingi huo kuna haja ya kuwafundisha watoto namna ya kuwatambua watu wanaowataka kimapenzi na kuwapa mbinu za kuwakwepa watu hao .

Mkurugenzi huyo anasema pamoja na mambo mengine, kufanya hivyo kutasaidia katika kupunguza kasi ya maambukizi ya Ukimwi na mimba za utotoni.

Lakini pia kuna umuhimu wa kuwapa watoto mbinu ili waweze kuepukana na vishawishi vinavyowavuta kujiingiza katika ngono za utotoni.

Hali kadhalika ni vyema watoto wakafundishwa juu ya umuhimu wa kutoa taarifa zinazohusu watu wanaowataka kimapenzi ili wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia jamii ihakikishe kuwa watoto wanapatiwa haki zao za kimsingi na wazazi watimize wajibu wao wa kulea familia ili kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.

Kila mtu katika jamii ashiriki katika kuwaelimisha watoto ili wawe na maadili mema ambayo yatasaidia kupunguza vishawishi kutokana na watoto hao kujua jinsi ya kuthamini miili yao.

Idhaa ya Kiswahili 2006-10-03